Mtumiaji:Kipala/Macho angani 7-10

Wana-anga

Kilomita mia nne juu yetu, pasipo tena hewa, kuna watu. Hao ni wanaanga kutoka duniani waliorushwa juu kwa nguvu za roketi hadi kuingia katika anga-nje.

Siku hizi, kila wakati kuna wanaanga watatu wanaozunguka Dunia wakikaa kwenye Kituo cha Kimataifa cha Anga, maarufu kwa kifupi chake ISS. Waliopo sasa wamefika juu tarehe tisa Aprili. Watarudi kwetu duniani kwenye mwezi Oktoba na wengine watachukua nafasi yao.

Mtu wa kwanza kufika kwenye anga nje alikuwa Mrusi Yuri Gagarin. Tarehe 12 Aprili 1961 alirushwa juu akazunguka dunia yote mara moja kwa muda wa dakika 108. Gagarin alikaa ndani ya chombo kidogo kuliko gari la kawaida akaketi tu tangu kupanda kwenye kituo cha kurushia roketi hadi kurudi duniani.

Mwaka 1969 Wamarekani Neil Armstrong, Michael Collins na Buzz Aldrin nao walitumwa wakasafiri hadi kufika kwenye Mwezi. Chomboanga chao kiliitwa Apollo na humo hao watatu walibanana kwenye nafasi ya mita mraba 6; angalau waliweza kusimama, kulala chini na kutembea hatua chache. Katika hali hiyo, walisafiri siku 8 hadi kufika kwenye Mwezi.

Leo hii wanaanga wanaoelekea Kituo cha Kimataifa cha Anga wanarushwa na chomboanga kidogo kinachoitwa Soyuz. Soyuz hutengenezwa Urusi tangu miaka 40. Hicho chombo ni kama bajaji ya angani inayobeba abiria wake bila tatizo. Siku hizi safari ni masaa sita tu kuanzia kuruka hadi kufika kituoni. Zamani ilichukua siku mbili. Kwenye kimo cha kilomita 400 juu ya uso wa Dunia Soyuz inakaribia polepole kituo cha ISS na kupachika mlango wake kwenye mlango wa kituo kikubwa. Wanaanga wapya wanaingia kituoni, wale waliomaliza kipindi chao cha kazi wanaondoka na kuanza safari yao kuelekea nyumbani-Duniani.

Wanaanga wote wa kwanza walikuwa marubani wa kijeshi. Siku hizi masharti ni tofauti. Mwanaanga lazima awe na digrii ya sayansi au uhandisi. Akiwa na mafunzo ya urubani ni faida lakini si lazima tena. Lazima awe na afya nzuri. Kila mwanaanga anapaswa kujua au kujifunza lugha mbili za Kiingereza na Kirusi.

Baada ya kufika kwenye kituo cha ISS, wanaanga wana ratiba iliyojaa shughuli nyingi. Wakikaa pamoja kwa nusu mwaka lazima washirikiane vizuri. Kuna kazi nyingi za kisayansi. Vyuo vikuu huandaa majaribio yanayohitaji kutekelezwa katika mazingira pasipo graviti, yaani nguvu ya mvuto wa Dunia: je njegere huota jinsi gani huko angani? Metali na aloi huyeyuka na kuganda vipi? Fuwele huunda maumbo gani katika mazingira hayo? ISS pia ina sehemu ya maabara isiyo na hewa. Hapo wanaanga wanapaswa kuvaa suti ya anga na kupita kwenye mlango wa kuzuia hewa. Je, virusi na bakteria viwanaweza kudumu uko angani? Pamoja na majaribio hayo kuna pia kazi ya matengenezo na ukarabati wa kituo chenyewe. Vipuri vinahitaji kubadilishwa. Ratiba ya kazi ni masaa 10, kulala masaa 8, pia mazoezi ya kukimbia na kuimarisha misuli kwa masaa mawili kila mwanaanga. Hakuna uzito maana wanaishi pasipo graviti, lakini mambo si mepesi.

8. Makundinyota

Makundinyota – picha agani

Nyota angani ni nyingi sana, na kila usiku zinasogea polepole kutoka mashariki kuelekea magharibi. Wazee Waswahili walikumbuka nyota nyingi na kuzitaja kwa majina. Hasa mabaharia walitumia nyota kama msaada wa kutambua njia zao baharini wakati wa usiku. Walipanga nyota kwa makundi na kutaja sehemu ya anga kwa jina la kundinyota fulani. Hii ilirahisisha kazi ya kutofautisha nyota. Hali halisi nyota katika kundinyota hazina uhusiano kati yake, zinaonekana tu kama kundi kwa mtazamaji aliye duniani lakini haziko mahali pamoja katika anga-nje. Zinaweza kuwa mbali sana kutoka nyota nyingine inayoonekana iko ndani ya kundinyota lilelile.

Mpangilio wa nyota katika makundinyota ni elimu ya kale sana. Wazee katika zama pasipo umeme na taa waliweza kutazama anga na nyota zake vizuri kuliko sisi. Hasa tukiwa mjini penye mianga mingi. Waliona vitu wakitazama nyota zilizokaa pamoja na kuwaza mistari kati yao. Kwa njia hiyo waliweza kutambua picha nyingi angani, hivyo kuona picha za watu, wanyama au miungu yao. Makundinyota yanayojulikana sana ni kama vile Jabari (au O-ri-on), Nge (pia Akarabu, au Skor-pi-o), Mara (au An-dro-me-da) na Salibu (au Msalaba wa Kusini). Majina hayo yana historia ndefu na nzuri sana. Tutaigusa mara kwa mara katika vipindi vyetu.

Huo upangaji nyota kimakundi ulikuwa msaada kwa watu kukumbuka na kutambua nyota. Katika mwezi Mei tukiangalia anga mnamo saa 2 usiku tunaweza kuona pembenne ndogo, karibu katikati ya anga. Mnamo saa mbili nyota hizo nne ziko kidogo upande wa mashariki wa kitovu cha anga. Ziko kama kona za pembenne isiyo mraba. Nyota hizo nne ni kundinyota lililoitwa „Ghurabu“ na mabaharia Waswahili. Ghurabu ni neno lenye asili ya Kiarabu linalomaanisha ndege kama Kunguru. Jina la Kiingereza ni „Kor-vus“. Watu wa Babeli ya Kale walikuwa wa kwanza kuona ndege huyo na jina lao likapokelewa na mataifa mengine waliofuata elimu ya Kibabeli. Ukikaa mahali penye giza utaona nyota nyingine, wazee walihesabu nyota saba.

Karibu na Ghurabu liko kundinyota dogo ambalo ni mashuhuri sana. Hili ni “Salibu”, kwa Kiingereza “The Southern Cross”, yaani Msalaba wa Kusini. Utaliona upande wa kusini, mnamo saa 3 liko takriban kimo cha ngumi tatu hadi nne juu ya upeo wa macho. Ina nyota tano zinazoonekana vizuri; tatu ni angavu zaidi na ya nne inafanya kona nne za mikono ya msalaba. Kundinyota hili halionekana kutoka nchi za kaskazini duniani; wageni wengi wanaokuja Afrika Mashariki wameshasikia habari zake wakipenda kuwa na mwenyeji anayeweza kuwaonyesha sehemu hiyo ya anga. Salibu au Msalaba wa Kusini lilijulikana kote duniani kutokana na taarifa za mabaharia wa kimataifa waliozunguka Dunia yote; kundinyota hilo lilisaidia usafiri wa baharini maana mkono mrefu wa msalaba daima unaelekea kusini kabisa. Ukitaka kujua Kusini kuko wapi, angalia angani, utazame nyota za Salibu na ufuate mstari wa mkono mrefu wa msalaba huo; unaelekeza kusini kabisa. Kwa hiyo kwa mabaharia wa kusini kundinyota hilo lilikuwa sawa na nyota ya ncha ya kaskazini kwenye upande mwingine wa Dunia.


Mirihi – jirani mwekundu

Mirihi ni sayari ya nne inayozunguka Jua letu katika anga-nje. Kwa hiyo ni sayari yetu jirani, kama Zuhura; lakini Zuhura ina nafasi ya pili kutoka kwenye Jua hivyo iko karibu zaidi nalo ilhali Mirihi iko mbali zaidi.

Kimataifa Mirihi inajulikana zaidi kwa jina lake la Kilatini ambalo ni Mars. Mara nyingi inaitwa pia „sayari nyekundu“. Tukiiangalia kwenye anga nuru yake hung’aa kwa rangi nyekundu. Watu wa kale waliona nyota na sayari kama ishara ya miungu kwa hiyo Waroma wa Kale waliona hapo mungu wao wa vita – huyu ni Mars na jina hilo limeingia katika lugha za Ulaya. Mataifa mengine waliona rangi nyekundu kama ishara ya moto – hivyo Waarabu, Wahindi na Wachina waliita „sayari ya moto“. Hiyo ndiyo maana ya jina Mirihi lililobuniwa na Waarabu na kupokewa hivyo na mabaharia Waswahili.

Lakini hata kama rangi nyekundu ilisababisha jina hilo, hali halisi Mirihi ni baridi kuliko Dunia. Maana iko mbali zaidi kutoka Jua hivyo inapokea kiasi kidogo zaidi cha nuru. Halijoto kwenye uso wake unaweza kufika hadi nyuzijoto 30 lakini inashuka hadi 140 chini ya sifuri.

Mirihi ni ndogo kuliko Dunia. Kipenyo chake ni kilomita 6,800 hivyo nusu tu ya Dunia. Inajizungusha kwenye mhimili wake na siku moja ya Mirihi inafanana na siku ya kwetu, muda wake ni saa 24 na dakika 39. Ila mwaka wake ni mrefu maana ina njia ndefu zaidi ya kuzunguka Jua, hivyo mwaka wa Mirihi una siku 687.

Sayari hiyo ina angahewa ambayo ni nyepesi sana; inafanana na hewa jinsi ilivyo kilomita 35 juu ya uso wa Dunia. Kwa hiyo, kama siku moja waanaanga watafika kwenye Mirihi watapaswa kuvaa suti nzito inayofunika mwili wote na kutunza hewa ndani yake. Ila tu suti haitakuwa nzito mno kwa sababu sayari hiyo ni ndogo kuliko Dunia, hivyo pia graviti au mvutano wake ni theluthi moja tu ya hapa duniani.

Mirihi imeshatembelewa na vipimaanga na vyombo vya utafiti vingi vilivyorushwa kule na Urusi, Marekani, Uhindi na Umoja wa Ulaya. Hivyo tumeshajifunza mengi kuhusu jirani mwekundu katika anga-nje. Uso wa Mirihi ni kama jangwa kubwa la mchanga, mawe na vumbi. Rangi yake usoni ni kweli nyekundu, lakini si kwa sababu ya moto, ila ni kutu. Vumbi na miamba ya Mirihi ina chuma ndani yake kiliyoshikwa na kutu. Lakini hakuna jani wali nyasi. Kuna dalili nyingi kwamba uso wa sayari uliathiriwa zamani na maji na mito lakini sasa hakuna maji tena kwenye uso wake, yamepotea yote. Inaaminiwa kuwepo kwa barafu ya maji katika sehemu za baridi chini ya uso wa sayari. Kuna milima na mabonde, na mlima mrefu kabisa ulipewa jina la „Olimpus“ ukiwa na kimo cha kilomita zaidi ya 20.

Hadi sasa haijulikani kama Mirihi ilikuwa na uhai wowote. Lakini vipimaanga vingine vinaandaliwa ambayo vina kazi ya kufanyia utafiti swali hilo.


10 Mwakanuru - Mbali ni nini 2863n

Mwakanuru - Mbali ni nini?

Tumezoea kutaja umbali kwa kilomita. Dar es Salaam hadi Mbeya ni kilomita mia nane hamsini, hadi Cape Town nchini Afrika Kusini ni karibu kilomita elfu tano. Tukizunguka Dunia yote kwa ndege tunasafiri kilomita elfu arobaini. Watu wa kwanza waliofika juu ya Mwezi kwenye mwaka elfu moja mia tisa sitini na tisa walivuka umbali wa kilomita lakhi tatu au 300,000.

Lakini katika anga-nje njia kutoka Dunia hadi Mwezi ni umbali mdogo sana. Roketi inayorushwa hadi kwenye Jua inavuka njia ya kilomita milioni mia moja na hamsini. Ila tu Jua liko karibu nasi tukizingatia umbali wa nyota. Nyota iliyo karibu nasi inajulikana kama Alfa Centauri au kwa jina la Kiswahili „Rijili Kantori“. Umbali wake ni kilomita trilioni arobaini hivi. Lakini Rijili Kantori ni nyota jirani, tukijadili nyota za mbali tunafikia namba ambazo kwa kawaida hatuelewi tena. Au unajua wewe kwintilioni na sekstilioni ni nini? Tunaweza kuiandika kwenye karatasi lakini ni wachache wanaotambua namba kubwa ya aina hii.

Basi vipimo na vizio vilivyobuniwa kwa matumizi hapa duniani havifai kule angani. Wakati wanaastronomia walianza kutambua ukubwa wa anga-nje, walitafuta kipimo mbadala. Miaka mia moja sabini iliyopita Mjerumani mmoja alipendekeza kizio cha mwakanuru. Mwaka wa nuru au kifupi mwakanuru ni umbali unaopitiwa na nuru katika kipindi cha mwaka mmoja. Labda unashtuka, msikilizaji mpendwa, kwa sababu „mwaka“ ni kipimo cha wakati lakini sisi tunatafuta kipimo cha umbali. Ila huyu jamaa aliyeanzisha „mwakanuru“ aliishi kabla ya kubuniwa kwa magari, watu walizoea kutaja umbali kwa masaa yaliyohitajika kutembea hadi kufika. Mji ule ni njia ya masaa mawili. Kabla ya kujengwa kwa reli katika Tanganyika umbali kati ya Bagamoyo na Ujiji ulitajwa kuwa safari ya siku 90, yote kwa miguu. Basi, ili tutaje umbali wa nyota, Mjerumani huyo wa mwaka 1851 alipendekeza kutumia „mguu wa nuru“ unaokwenda haraka kuliko mguu wa binadamu.

Kama taa inawaka hapa petu tunaona mwanga wake mara moja. Lakini si mara moja kweli maana hata mwanga au nuru ina kasi yake. Inapita kilomita 300,000 kila sekunde ambayo ni sawa na umbali kati ya Dunia na Mwezi. Kama taa ingewaka juu ya Mwezi, tungeiona sekunde moja baadaye. Nuru ya Jua inahitaji dakika nane na nusu hadi kufika kwetu. Na nyota jirani ya Rijili Kantori iko katika umbali wa miakanuru minne hivi. Nikiitazama leo naiona jinsi ilivyokuwa miaka minne iliyopita.

Tena Rijili Kantori au Alfa Centauri ni nyota ya karibu. Nyota nyingine ziko mbali zaidi. Nyota nyingi tunazoziona ziko umbali wa miakanuru makumi, mamia, hata maelfu. Kwa kutumia darubini kubwa tunatambua nyota katika umbali wa miakanuru milioni. Mwanga ninaoona wa nyota ya mbali ulianza safari yake kufika kwetu miaka elfu kadhaa iliyopita. Tukizingatia hayo tunaweza kuelewa: kwa kweli elimu ya astronomia inatufungulia milango ya maajabu mengi.