Mzee Omari Kungubaya (1939 - 20 Oktoba 2016) alikuwa mwanamuziki maarufu wa muziki wa dansi kutoka nchini Tanzania. Alifahamika zaidi kwa kuwa mtunzi wa wimbo wa kipindi cha salam za wagonjwa katika redio ya taifa ya Tanzania (RTD).

Omari Kungubaya
Taarifa za awali
Jina la kuzaliwaOmari Kungubaya
Amezaliwa1939
Mgaza Vigolegole, Morogoro
Tanzania
Amekufa20 Oktoba, 2016
Njeteni, Mbezi ya Kimara, Dar es Salaam, Tanzania
Kazi yakeMwimbaji, mtunzi, mpiga gitaa
Miaka ya kazi1955-2016
Ameshirikiana naCuban Marimba

Historia

hariri

Maisha na muziki

hariri

Mzee Kungubaya ni matunda mengine ya hazina isiyokwisha kutoka mkoa wa Morogoro. Alizaliwa mwaka 1939 katika Kijiji cha Mgaza Vigolegole, Morogoro, ambapo alipata elimu yake ya msingi (darasa la nane) Msamvu Middle School mwaka 1955. Alishindwa kuendelea na masomo ya darasa la tisa kutokana na wazazi wake kushindwa kumlipia karo.

Historia yake kimuziki inaanzia mwaka wa 1955 akiwa shuleni Msamvu, ambapo wakati huo alikuwa na umri wa miaka 16 tu, na aliweza kuchaguliwa kuwa kiongozi wa bendi ya shule na mara baada ya kumaliza shule akajiunga rasmi na bendi ya Cuban Marimba iliyokuwa chini ya Salum Abdallah Yazidu ("Say"). Itakumbukwa kwamba, bendi hiyo iliyokuwa na maskani yake Nunge Welfare (sasa eneo hilo linajulikana kama Mji Mpya), Morogoro ilikuwa tishio kwa bendi nyingi za Dar es Salaam na ndiyo iliyoibua vipaji vya wanamuziki wengi. Kwa sasa bendi hiyo imetoweka katika ulimwengu wa muziki.

Katika mahojiano maalum, Mzee Kungubaya alimtaja Kibwana Katashingo, aliyekuwa dereva wa marehemu Salum Abdallah na pia mpiga drum wa bendi hiyo, kwamba ndiye aliyekuwa mwalimu wake wa kwanza katika muziki wakati alipojiunga na Cuban Marimba, ambapo yeye Kungubaya alikuwa akipiga gitaa la galatone lenye nyuzi sita. Mwaka 1960 Kungubaya alichanja mbuga na kuelekea Nairobi, Kenya kwa kile alichosema alikwenda kujiendeleza kimuziki.

Akiwa huko, alipokelewa na wanamuziki wakongwe wakiwemo akina John Ondolo Chacha, John Mwale na David Amunga, ambao wote walikuwa wakikung'uta magitaa ya galatone kwenye vilabu mbalimbali jijini humo. Hata hivyo, mwaka uliofuata alirejea Morogoro na kujiungan na bendi ya Kilosa Jazz Band iliyokuwa ikiundwa na akina Yahya Abbas na marehemu Abel Baltazar. Alidumu na bendi hiyo hadi mwaka 1963.

Baadaye aliamua kurejea tena Cuban Marimba, ambapo viongozi wa bendi hiyo wakampeleka kwa Mzee Mwaipungu aliyekuwa akiongoza bendi nyingine iliyokuwa tawi la Cuban Marimba, lakini mwaka 1969 akaondoka. Safari hii aliamua kuyaweka kando masuala ya muziki na kuwa "mshika fedha" katika vituo vya kuuza mafuta vya Capital Esso Services kilichopo Mtaa wa India na baadaye kituo cha Agip Centre cha Mwembesongo. Hiyo ilikuwa mwaka 1970.

Mwaka wa 1971, akaamua kurejea tena masuala ya muziki, ambapo mara hii alikuwa akijitegemea mwenyewe. Safari hii alikuwa akipiga gitaa moja tu la galatone, ambapo alihamia Dar es Salaam na kuanza kutumbuiza katika baa moja iliyokuwa ikimilikiwa na Mama Hamm huko Tandale, Manzese. Baadaye akawa na mapenzi na mkuu wake huyo mama na hatimaye wakafunga ndoa hadi kufa kwa mama huyo mnamo mwaka wa 1995, lakini hawakubatika kupata mtoto. Lakini mwaka 1974 tulinunua shamba kijijini Kwembe, na kuanzia hapo mpaka anafariki ndiko walikokuwa kijijin wanaishi hadi pia umauti wa Mzee Kungubaya unamkuta nae.

Kwa maeleoz ya "Mzee Kungubaya alisema kwamba", kabla mkewe huyo hajafariki alimpa ruksa ya kuoa mwanamke mwingine, ameoa, na wamebahatika kupata watoto watatu, ingawa mmoja alifariki.

Maisha ya kijijini, kilimo na muziki

hariri

Maisha yakawa ya kawaida tu kama mwanakijiji. Shughuli zake zilikuwa za kilimo ingawa hakuwa na mtaji wa kutosha na mara nyingi alitumia jembe la mkono. Ingawa alikuwa kijijini, lakini muziki kwa vile uko kwenye damu yake hawezi kuuacha, ndiyo sababu kila siku ya Ijumaa hadi Jumapili jioni alikuwa akionekana katika baa mbalimbali huko Kibaha-Maili Moja, akiwatumbuiza watu kwa kutumia gitaa lake la galatone alilolinunua miaka ya 1970.

Mara nyingi alikutikana akiimba nyimbo nyingi zilizopata kutamba miaka ya 1960 hadi 1970, hususan nyimbo kama Mtoto si Nguo na Ndugu sikilizeni navunja vunja vikombe zilizoimbwa na Heorge Mukabi wa Kenya, na Wanawake wa Tanzania na Maneno madogo madogo kwa mabibi na mabwana zilizoimbwa na marehemu Salum Abdallah kule Cuban Marimba.

Wakati wa enzi zake alitunga nyimbo nyingi sana, lakini alisema kwamba, katika miaka 47 akiwa kwenye jukwaa la muziki hakunufaika na chochote zaidi ya kuishia kutumbuiza vilabuni!

Hata hivyo, aliitaka serikali kuweka utaratibu mzuri wa kuwajali wasanii wa zamani kwa kuwaenzi na ikibidi iwekwe siku maalum ya kuwakumbuka wakongwe wa zamani na kazi zao.

Aidha, alisema kwa kuwa Sheria ya Haki Miliki imekwisha pitishwa na serikali, basi ni vyema hata wasanii wa zamani wafikiriwe kupewe chochote na Radio Tanzania kutokana na kazi zao zilizohifadhiwa huko, ambazo sasa RTD (TBC Taifa) imekuwa ikiziuza.

Kifo cha Kungubaya

hariri

Mzee Omari Kungubaya alifariki 20 Oktoba 2016 nyumbani kwake Njeteni, Mbezi ya Kimara na kuzikwa hukohuko, baada ya afya yake kuwa si nzuri kwa muda mrefu. Msiba ulifanyika hukohuko kwake Njeteni, Mbezi ya Kimara.

Urithi

hariri
  • Wakati umewadiwa
  • Wa salamu za wagonjwa
  • Hospitalini
  • Leo tunawapa pole x2
  • Ajuaye Bwana Mungu
  • Kwa mzima kuwa mfu
  • Mgonjwa kuwa salama
  • Leo tunawapa pole x2
  • Kipindi chenu kinawapa pole
  • Wote tunawapa pole
  • Mungu awajalieni pole x2
  • Tunawapa pole x2.

Hayo yalikuwa mashairi ambayo yalikuwa yakifungua na kufunga kipindi cha saa nzima cha Ugua Pole, kilichobeba jina la wimbo huo, kinachosikika Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kila siku ya Jumapili kuanzia saa 4.02 asubuhi hadi saa 5.00.

Lakini pamoja na kufahamika kwa mashairi hayo hata kwa vijana wa kizazi cha leo, ni dhahiri kwamba si wengi wanaomfahamu mtunzi wa wimbo huo unaoendelea kutamba redioni mpaka leo. Pamoja na kutamba na wimbo huo wa kipindi cha redio, hata hivyo, kama walivyo wengi wao, hakunufaika na lolote katika muziki.

Tazama pia

hariri

Marejeo

hariri

Viungo vya Nje

hariri
  Makala hii kuhusu mwanamuziki/wanamuziki fulani wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Omari Kungubaya kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.