Paul von Lettow-Vorbeck

Paul Emil von Lettow-Vorbeck (20 Machi, 18709 Machi, 1964) alikuwa afisa wa jeshi la Dola la Ujerumani na mkuu wa jeshi la Schutztruppe katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.

Lettow-Vorbeck mnamo 1913 akiwa Luteni Kanali

Lettow-Vorbeck alipata umaarufu kama kamanda Mjerumani wa pekee aliyeweza kuongoza jeshi lake dhidi ya idadi kubwa ya vikosi vya Uingereza bila kushindwa kamili hadi mwaka 1918 akifaulu kuvamia koloni za Ureno na Uingereza hadi kusalimisha amri siku kadhaa baada ya mwisho wa vita.

Jitihada zake zilielezwa kuwa "kielelezo kikuu cha vita ya msituni katika historia" [1].

Matendo ya Lettow-Vorbeck yamepokelewa kwa namna tofautitofauti. Kwa upande mmoja uongozi wake katika vita ulitazamiwa kama mafanikio kwa sababu alilazimisha Uingereza kupeleka wanajeshi wengi Afrika ya Mashariki badala ya kuwatumia Ulaya na kuendelea bila kushindwa mpaka mwisho wa vita. Kwa upande mwingine vita yake haikuwa zaidi ya usumbufu kwa Uingereza kulingana na wanajeshi mamilioni waliopigana pale Ulaya halafu ilisababisha vifo vingi kati ya wakazi wazalendo wa Afrika kwa jambo ambalo halikuwa la kwao. Mwanahistoria Iliffe alikadiria idadi ya waliokufa kati ya 100,000 hadi 300,000 hasa askari ya kikosi cha wapagazi na watu raia kutokana na njaa iliyosababishwa na vita.[2]

Familia na kuwa mwanajeshi hariri

Paul von Lettow-Vorbeck alizaliwa kama mtoto wa afisa wa jeshi la Prussia akajiunga mwenyewe na jeshi tangu mwaka 1890. Mwaka 1900 alitumwa China kwa kupingana na harakati ya wanamgambo Mabondia. Mwaka 1904 alitumwa Afrika ya Kusini-Magharibi ya Kijerumani (Namibia) katika vikosi vya kupigana na Waherero alipojeruhiwa na kurudi Ujerumani.

 
Lettow-Vorbeck na gavana von Schnee pamoja na kikosi cha askari wa Schutztruppe kwenye kadi ya posta 1914
 
Tangazo la kuomba michango ya misaada kwa wanajeshi likimwonyesha Lettow Vorbeck na sahihi yake

Mkuu wa Schutztruppe katika Afrika ya Mashariki hariri

1913 alipewa cheo cha luteni kanali na kutumwa Afrika ya Masahriki alipokuwa mkuu wa Schutztruppe. Katika Agosti 1914 alipokea habari za Vita Kuu ya Kwanza huko Ulaya. Gavana Mjerumani von Schnee aliyetaka kuelewana na Waingereza kutokuwa na vita Afrika lakini dhidi ya amri ya gavana Lettow-Vorbeck aliamua kuandaa utetezi wa koloni. Alielewa ya kwamba Afrika haikuwa muhimu kwa vita ya Ulaya. Mpango wake ilikuwa kulazimisha Uingereza kutuma wanajeshi Afrika ambao wasingeweza kupigania Ulaya na hivyo labda kusaidia ushindi wa Ujerumani.

Mwanzoni alikuwa na jeshi dogo tu cha askari Waafrika 2,472 na maafisa na maafande Wajerumani 300. Aliongeza askari wa polisi 2,000 na mamia ya walowezi Wajerumani waliojitolea katika jeshi.

Vita katika Afrika ya Mashariki hariri

 
Uchoraji wa msanii Mwafrika asiyejulikana wa kuonyesha jinsi Lettow-Vorbeck alisalimisha amri 1918 mbele ya Waingereza

Kwenye Novemba 1914 Wajerumani waliweza kuzuia jaribio la Waingereza kuvamia Tanga na kwenye Februari 1915 alirudia kushinda vikosi vya Waingereza huko Yasini kwenye mpaka na Kenya[3]. Lettow aliendelea kushambulia njia ya reli kati ya Mombasa na Nairobi. Katika mapigano haya Lettow-Vorbeck alikamata bunduki na ramia kwa askari wake lakini alitambua pia ya kwamba idadi ndogo ya jeshi lake isingetosha tena kuwa na mapigano makubwa. Hivyo aliamua kuendelea kwa njia ya vita ya msituni kwa shabaha ya kuchosha Waingereza walikokuwa na idadi kubwa zaidi ya wanajeshi kutoka Kenya, Uhindi na Afrika Kusini.

Alitumia mwaka 1915 kuongeza idadi ya askari Waafrika hadi karibu 16,000 akapokea pia wanamaji wa manowari SMS Koenigsberg kutoka Ujerumani iliyozamishwa na Waingereza katika delta ya mto Rufiji. Wakati huohuo Waingereza waliongeza vikosi vingi kutoka Afrika Kusini wakashambulia katika Machi 1916 kutoka upande wa Kenya. Wakati huohuo jeshi la Ubelgiji ilivamia kutoa Kongo ya Kibelgiji.

Hapo Lettow Vorbeck alipaswa kurudi polepole. Baada ya mapigano ya Mahiwa ambako Schutztruppe ilipotea askari zaidi ya 500 lakini Waingereza walipotea 2,400 Lettow Vorbeck alipandishwa cheo kuwa jenerali baada ya habari hizi kufika Ujerumani. Katika Novemba 1917 alipaswa kukimbia zaidi akiwa na uhaba wa ramia. Kwa kuacha nyuma wajeruhiwa wote akavuka mto Ruvuma na kuingia Msumbiji. Katika mapigano mbalimbali alipata tena silaha na ramia pamoja na chakula kutoka kwa Wareno akazunguka katika Msumbiji kusini.

Katika September 1918 Lettow-Vorbeck alivuka tena mto Ruvuma akarudi katika eneo la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani (Tanzania, mkoa wa Songea) akiepukana na mapigano dhidi ya jeshi kubwa la Waingereza akapita hadi kuingia katika Rhodesia ya Kaskazini (Zambia) pasipo na jeshi la Kiingereza. Hapo kwenye siku ya 13 Novemba 1918 Waingereza walituma ujumbe ya kumwarifu kuwa vita ilikwisha tayari huko Ulaya. Walipatana kutopigania tena na tarehe 25 Novemba 1918 Lettow-Vorbeck aliongoza jeshi lake hadi mji wa Abercorn (sasa Mbala, Zambia) aliposalimisha amri na kukabidhi silaha kwa Waingereza. Wakati huu jeshi lake bado lilikuwa na Wajerumani 1155, askari Waafrika 1,168 na wapagazi 3,500.

Kurudi Ujerumani hariri

Baada ya kipindi cha kufungwa huko Dar es Salaam Lettow-Vorbeck alirudi Ujerumani kwenye Machi 1919 ambako alipewa nafasi ya peredi huko Berlin na kusherehewa kama shujaa wa vita.

Alioa akiendelea kwa muda kama mwanajeshi lakini baada ya kushiriki katika jaribio la kupindua serikali ya Jamhuri ya Ujerumania liachishwa. Akafanya kazi katika kampuni ya biashara na kuwa mbunge wa chama cha DNVP kilichotaka kumrudisha mfalme aliyepinduliwa mwaka 1918. Hakupenda Hitler na hakushiriki na siasa yake. 1926 alifaulu kushawishi serikali ya Ujerumani ya kwamba askari Waafrika katika Tanganyika walipata mishahara amabayo hayakulipiwa tangu mwaka 1917 hadi 1918 pamoja na kiasi kidogo cha malipo ya pensheni. 1953 alisafiri tena Tanganyika aliokutana na askari wazee 400.

Kabla ya kifo chake bunge la Ujerumani Bundestag liliamua 1964 kulipa tena pensheni kwa askari wa Schutztruppe walioishi bado.

Kumbukumbu yake ya wasiwasi hariri

Kumbukumbu ya Lettow Vorbeck katika Ujerumani kulibadilika katika ya heshima ya shujaa wa vita na ukosoaji kama mteteaji wa ukoloni na mwajibika kwa vifo vingi vya Waafrika katika vita ya nchi za Ulaya.

Makambi manne ya jeshi la Ujerumani yalipewa jina lake pamoja na barabara katika miji mbylimbali. Leo hii kuna kambi 1 ambayo bado lina jina yake na miji kadhaa yaliamua kubadilisha majina ya mitaa iliyowahi kupewa jina lake.

Marejeo hariri

  1. as the greatest single guerrilla operation in history, and the most successful [zimmerer.typepad.com/Documents/Guerrilla%20Von%20Lettow%20New.pdf Hoyt] Hoyt, Edwin P. (1981), Guerilla: Colonel von Lettow-Vorbeck and Germany's East African Empire (PDF), New York: MacMillan Publishing Co., Inc., ISBN 0-02-555210-4, retrieved October 16, 2016
  2. John Iliffe: A Modern History of Tanganyika. uk.. 249 ff na 269 f.
  3. The battle of Jassin