Rhapta ni jina la soko na mji wa kale katika pwani ya Afrika ya Mashariki. Habari zake zilipatikana tangu karne ya kwanza katika mwongozo wa kigiriki kwa ajili ya mabaharia. Jina la Rhapta lilitajwa tena katika vitabu vingine hadi karne ya 6 BK lakini baadaye lilipotea au kubadilishwa.

Wataalamu walio wengi hukubaliana ilikuwepo ufukoni wa Tanzania lakini hakuna uhakika kuhusu mahali pake kamili. Kuna kisio la kuwa Rhapta ni jina la kale la Pangani lakini hiyo ni kisio tu kutokana na bandari nzuri ya kiasili inayopatikana pale Pangani. Wengine wanaona Tanga au mdomo wa mto Rufiji ilikuwa mahali pa Rhapta.

Kitabu cha Periplus ya Bahari ya Eritrea kilichoandikwa mnamo mwaka 70 BK kinataja Rhapta kuwa soko kuu la Azania barani pia kituo cha mwisho kati ya miji na vituo vilivyofanya biashara na dunia ya Kiroma. Mnamo mwaka 200 mwandishi Mmisri Claudius Ptolemaius anataja Rhapta kuwa mji mkuu wa Barbaria (Afrika ya Mashariki barani). Rhapta ilikuwa mdomoni mwa mto wenye jina la Rhapta ambao pia uliaminika kuwa na asili yake katika "Milima ya Mwezi". Mdomo wa mto ulikuwa karibu na kisiwa cha Menouthis. Hakuna uhakika kama kisiwa hiki ni Pemba au Mafia.

Sarafu za kiroma za karne za kwanza BK zimepatikana sehemu mbalimbali za pwani; zinathibitisha kuwepo kwa biashara kati ya dunia ya Kiroma na Azania wakati ule.

Kufuatana na Periplus biashara ilikuwa ya pembe za ndovu na magamba ya kobe.