Hekaya za Abunuwasi

(Elekezwa kutoka Riwaya za Abunuwasi)

Hekaya za Abunuwasi ni mkusanyo wa hadithi fupi zinazosimulia habari za Abunuwas. Hadithi hizi hazina uhusiano halisi na Abu Nuwas, mshairi Mwarabu aliyeishi Baghdad mnamo mwaka 800 BK.

Jalada la Nasreddin katika lugha ya Kiazeri; hadithi zake zinafanana zile za Abunuwasi

Abunuwasi wa hekaya ni mjanja anayeshindana mara kwa mara na tabia mbaya za watu wenzake kama vile walafi, matajiri wasio na huruma, akiwadanganya kwa kutumia mbinu zao wenyewe. Mara nyingi hadithi zilezile zinasimuliwa pia katika nchi nyingine za Waislamu kwa majina kama hekaya za Nasreddin, Guha au "hekaya za Mullah".[1]

Mchoraji Mtanzania Godfrey Mwampembwa (anayejulikana kwa jina la Gado) alitunga kitabu cha vibonzo kwa jina la Abunuwasi kinachosimulia tatu za hekaya zake.[2] Kitabu hiki kilitolewa na Sasa Sema Publications mwaka 1996.[3] Kuna matoleo kadhaa ya hekaya ya miaka ya nyuma.

Mfano 1

Kuna wakati, Abunuwasi aliamua kuwa mfuga mbuzi. Alinunua mbuzi wa kufuga huku akiwa na lengo la kujiongezea kipato chake pindi mbuzi huyo atapoanza kuzaa, ili awafuge ndama wawe wengi na kumuwezesha kuwa tajiri kuliko wote waliokuwepo katika mji ule..

Siku moja Abunuwasi akipokuwa anampeleka mbuzi wake malishoni, alikuta kiatu kimoja kizuri sana katikati ya njia. Alisimama na kukiangalia. Kiatu kilipendeza machoni mwake ila akasema "kiatu hiki ni kizuri lakini mbona kipo kimoja tu?" Alitafuta kiatu cha pili pembezoni mwa njia ila hakukiona. Alipoona hawezi kuvaa kiatu kimoja, aliamua kukiacha palepale. .

Abunuasi akachukuwa mbuzi wake na mbele kidogo akaona kile kiatu cha mguu wa pili. Abunuwas alishangaa na akaona bora angelikichukua kile cha mwanzo kwa sababu cha pili kimepatikana.

Aliporudi pale mwanzo kukitafuta alichokiacha awali lakini hakukikuta tena, alijaribu kukitafuta lakini hakukiona. Basi akadhani kuna mtu amekiokota. Akarudi haraka alipomfunga mbuzi wake nako pia hakumkuta mbuzi wala kile kiatu kimoja. Mwisho akawa amemkosa mbuzi na viatu, Ndoto zote za Abunuwasi kupata utajiri zikaruka na akabaki na umasikini wake kwa sababu ya tamaa yake.

Marejeo

  1. linganisha makala ya Kiingereza en:Nasreddin
  2. Pilcher, Tim and Brad Brooks. (Foreword: Dave Gibbons). The Essential Guide to World Comics. Collins and Brown. 2005. 297.
  3. Gado (Author). "Abunuwasi (Swahili Edition) (9789966960900): Gado: Books". Amazon.com. Iliwekwa mnamo 2014-06-20. {{cite web}}: |author= has generic name (help)
  Makala hii kuhusu kitabu fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Hekaya za Abunuwasi kama Mwandishi wake, hadithi au matoleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.