Senati ya Muungano wa Madola ya Amerika (kutoka Kilatini "senatus" - baraza la wazee) ni sehemu ya bunge la Marekani pamoja na Nyumba ya Wawakilishi. Wabunge wake huitwa "maseneta".

Jengo la Capitol mjini Washington DC ni makao ya senati.

Kila jimbo kwenye shirikisho la Muungano wa Madola ya Amerika linachagua maseneta wawili kwa kipindi cha miaka sita bila kubagua kati ya majimbo. Maana yake jimbo kama Wyoming lenye wakazi nusu milioni lina maseneta wawili sawa na jimbo la Kalifornia lenye wakazi milioni 37.

Idadi ya majimbo ya Marekani ni 50 hivyo kuna maseneta 100. Uchaguzi si wakati mmoja kwa wote lakini theluthi moja inachaguliwa kila baada ya miaka miwili.

Pamoja na sehemu nyingine ya bunge, yaani Nyumba ya Wawakilishi, Senati inaamua juu ya sheria zinazopaswa kupita pande zote mbili.

Senati ina jukumu la kuamua juu ya vita na amani. Rais wa nchi anapaswa kupata kibali cha senati kabla ya kuita maafisa muhimu kama mawaziri na mahakimu wa mahakama kuu ya kitaifa.

Seneta anapaswa kuwa na umri wa angalau miaka 30 na kuwa raia wa Marekani tangu miaka 9 au zaidi.