Visiwa vya Aleuti (kwa Kiingereza: Aleutian Islands, kwa lugha ya wazawa: Tanam Unangaa) ni safu ya visiwa 150 hivi vyenye asili ya kivolkeno kaskazini mwa Bahari Pasifiki.

Ramani ya upinde wa Visiwa vya Aleuti kati ya Alaska na Siberia

Vinaenea kwa kilomita za mraba 17,666 na safu hiyo ina urefu wa kilomita 1900 kutoka Rasi ya Alaska (Marekani) hadi Rasi ya Kamchatka katika Siberia (Urusi). Upinde wa visiwa hivyo unatenganisha Bahari ya Bering na sehemu nyingine ya Bahari Pasifiki.

Mara nyingi hugawiwa katika makundi kama vile (kuanzia Rasi ya Alaska) Fox Islands, Islands of Four Mountains, Andreanof Islands, Rat Islands, Near Islands upande wa Marekani, halafu Visiwa vya Komandorski upande wa Urusi.

Kila kisiwa ni mlima wa volkeno unaoenea juu ya uso wa bahari. Safu hii imetokea kama sehemu ya pete ya moto ya Pasifiki; hapa bamba la Pasifiki linasukumwa chini ya bamba la Amerika Kaskazini na hivi kusababisha nafasi kwenye koti la dunia inayowezesha joto na magma kupanda juu.

Upande wa Alaska kuna wakazi wasiozidi 8,200 wanaoishi kwenye visiwa 7. Sehemu ya Kirusi huitwa Visiwa vya Kamanda (au Komandorski) yenye wakazi 800 hivi kwenye Kisiwa cha Bering.

Viungo vya Nje hariri

 
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu: