Wakara
Wakara ni kabila la watu wa Tanzania wanaoishi hasa katika Mkoa wa Mwanza, wilaya ya Ukerewe, hususan katika kisiwa cha Ukara.
Kutokana na uhaba wa ardhi uliosababishwa na ongezeko la kasi la idadi ya watu, Wakara wengine wamelazimika kuhama kisiwa hicho. Kwa sasa wanapatikana kwa wingi katika kisiwa cha Ukerewe na wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, na Chato Mkoa wa Geita[1]
Hadi kufikia mwaka 1987 idadi ya Wakara walikuwa kwa makadirio ya jumla ya 86,000.
Lugha
haririLugha yao ni Kikara. Lugha hiyo inafanana sana na Kijita na Kikwaya, lugha ambazo huzungumzwa na Wajita na Wakwaya; makabila ambayo hupatikana katika mkoa wa Mara. Haya makabila yana mila ambazo vilevile zinafanana sana. Hata majina yao hufanana.
Hata hivyo ipo tofauti ndogondogo sana katika matamshi ya lugha hizo. Kwa mfano, badala ya maneno yenye "g" kutamkwa na Wakara, wao hutamka "k" tofauti na wenzao Wajita na Wakwaya. Pia kuna maneno yenye herufi "j". Wakati Wajita na Wakwaya hutamka maneno yenye "j" kama yalivyo, Wakara hutamka maneno hayo kama "ch".
Mifano halisi ni kama ifuatavyo:
- Wajita Wakara
- Chigende (twende) Chikende
- Jaji (babu) Chachi
- Magesa (Jina la mtu) Makesa
Historia
haririInasemekana kuwa asili ya Wakara ni kutoka Sudan Kusini. Inaaminika Wakara walikimbia vita vya biashara ya watumwa, wakipitia Uganda na hatimaye kujikuta katika kisiwa cha Ukara ambapo waliamua kuweka maskani. Kundi hili hupatikana zaidi katika sehemu ya magharibi ya kisiwa hiki. Hata hivyo kuna jamii ya watu wachache ambao walitokea sehemu ya mashariki, katika mkoa wa Mara.
Kazi
haririKwa asili Wakara wanajulikana kwa kuwa watu wenye bidii ya kazi, wavumilivu, waaminifu na wakweli, wenye msimamo katika masuala ya msingi, wakarimu na wakaribishaji wa wageni. Kazi zao za asili ni pamoja na kilimo, ufugaji na uvuvi.
Mtu hawezi kuongelea maendeleo ya wilaya ya Ukerewe na mkoa wa Mwanza kwa ujumla bila kuwataja Wakara. Kutokana na tabia yao ya kufanya kazi kwa bidii wamejikuta wakiwa wachangiaji wakubwa wa maendeleo ya kiuchumi kwa maeneo haya kutokana na kushiriki kwao kuzalisha mazao mbalimbali ya chakula na biashara ambayo husafirishwa na kuuzwa katika sehemu kubwa ya mkoa wa Mwanza na maeneo mengine jirani. Kwa miaka mingi jamii hii imekuwa wazalishaji wakubwa wa mazao ya mihogo, viazi vitamu na mpunga, na samaki.
Tanbihi
hariri- ↑ "Wanawake wanaotakaswa baada ya kuzaa pacha Tanzania", BBC News Swahili, iliwekwa mnamo 2024-01-13
Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Wakara kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |