Makosa si jambo la ajabu. Kila mwanawikipedia amefanya makosa - tupo hapa kusaidiana ili kamusi elezo yetu ikue na kustawi!

Makosa yafuatayo yanayotokea mara nyingi:

1 Sentensi ya kwanza

Sentensi ya kwanza ya makala ina kawaida yake; neno la kwanza (au: kati ya maneno ya kwanza) ni jina la makala kwa herufi koza (bila kichwa cha pekee!). Jina hili halitokei baadaye tena kwa herufi koza.

2 Kumwaga Kiswahili kibovu kutoka programu ya kutafsiri (google translate n.k.)

Programu za kusaidia tafsiri ni msaada mkubwa kwa mfano translate.google.com. LAKINI hadi sasa programu hizi hazileti tafsiri kamili. Hasa kwenye lugha kama Kiswahili bado zinajaa makosa. Mara nyingi sentensi hazieleweki maana hutafsiri neno-kwa-neno na muundo wa sentensi kwa Kiswahili na lugha za Ulaya ni tofauti mno. Maneno mengi ya Kiingereza yanabaki kwa sababu programu haina uhakika ya Kiswahili chake. Wakati mwingine chaguo la neno si sahihi.

  • Kwa hiyo ni kosa nzito kunakili tu yale yanayotokea kwenye dirisha la "translate" na kuyahifadhi kama makala ya wikipedia.
  • Haitoshi kusahihisha kidogo tu - itachukua muda na kusoma yote mara kadhaa!
  • Bila muda wa kutosha ni afadhali kuandika makala fupi kwa maneno yako mwenyewe

3 Kuongeza kichwa mwanzoni

Wikipedia inaweka kichwa juu ya makala ambayo ni sawa na jina la makala inayoonekana katika mstari wa anwani Mfano: http://sw.wikipedia.org/wiki/Wikipedia:Makosa

Kwa hiyo tusiongeze kichwa juu ya mstari wa kwanza. Vichwa tunaweka ndani ya makala pekee.

4 Kuweka alama ya sahihi au jina lako kwenye makala

Wikipedia ni kazi ya watu wengi. Alama ya sahihi ~~~~ ina mahali pake kwenye kurasa za majadiliano pekee! Menginevyo historia ya ukurasa inakumbuka ni nani aliyeweka aandishi gani.

Wengine wanataka kuonyesha ni nani aliyeandika matini fulani wanaingiza jina ndani ya makala. Hii ni marufuku, itafutwa. Kwa kawaida makala ina michango ya watu mbalimbali. Hii ni sababu hatutaki kuona majina ya watungaji hapa.

5 Kutoandika kwenye nafasi ya kwanza ya mstari

Watu wengine hukosea kutoanzisha mstari mpya kwenye nafasi ya kwanza. Inatokea ukianza mstari kwa "empty space". Tokeo lake ni hivi:

Watu wengine hukosea kuanzisha mstari mpya kwenye nafasi ya kwanza. Inatokea ukianza mstari kwa "empty space".

Kwa maandishi ya kawaida ni kosa. Inaweza kusababisha maandishi marefu kutosomeka. Hutumiwa tu kwa kusudi maalumu kwa mfano kwa kuonyesha mfano fulani hasa ikiwa na maandishi kidogo.

6 Kusahau Jamii

  • Jambo muhimu ni Jamii (category) inayopanga makala katika kundi la makala zinazogusa mada za karibu. Tafuta jamii inayolingana. Anza kwenye jamii kuu kwenye ukurasa wa Mwanzo na kuchungulia ndani zao kwa msaada wa Maalum:SafuyaJamii. Au chungulia hapa Maalum:Jamii.

7 Kutafsiri majina maalumu

Usitafsiri majina maalumu kwa ajili ya watu, makundi ya muziki au vitabu. Klabu ya mpira "Arsenal" itajwe kama "Arsenal" si tafsiri yake kama "Ghala ya Silaha". Bwana Miller anaitwa hata kwa Kiswahili "Miller" si "msagaji". Kitabu cha "Harry Potter" kibaki vile si "Henry Mfinyanzi" isipokuwa kama kuna toleo la Kiswahili kwa jina tofauti na ni toleo hili linalotajwa.

Jambo ni tofauti kama umbo maalumu la jina lipo kwa Kiswahili. Mwanzilishaji wa Ukristo aliitwa katika lugha yake "Yehoshua", kwa Kigiriki "Iesous", kwa Kiingereza huitwa "Jesus" na kwa Kiswahili anajulikana kama "Yesu".

8 Kuvuruga viungo kwa nukta na koma

Viungo vya ndani ya wikipedia ni maneno yaliyowekwa katika mabano mraba ambayo ni sawa na jina la makala nyingine mfano Afrika yakiungana makala. Kama kwa bahati mbaya alama kama nukta au koma inaingizwa ndani ya mabano mfano Afrika, au .Afrika kiungo kimeharibika. Dawa Yake ni kutazama vizuri mabano hasa yakionekana mekundu.

Njia nyingine ni kutojali umbo la majina. Africa ya Mashariki na Afrika ya MAshariki yote hayafai hata kama yamekosa herufi 1 tu, sahihi ni Afrika ya Mashariki.

Kwa umbo sahihi inafaa kutumia dirisha la "tafuta", kuingiza jina na kubofya "tafuta" chini ya dirisha. Sasa inajitokeza orodha inayosaidia.

9 Kuchanganya maana

Makala za maana zina kazi ya kumwelekeza msomaji mahali anapotafuta kama Neno moja linaweza kuwa na maana mbalimbali. Hizi zisichaganywe katika makala moja. Tunaunda makala yenye umbo tofauti la jina kwa mfano mwezi (gimba la angani) na mwezi (wakati).

Maana hizi tunakusanya katika "makala ya maana" (tazama: Msaada:Maana. Haitakiwi kuwa na maandishi marefu bali maelezo mafupi tu mfano: .

  1. mwezi (gimba la angani) - msindikizaji wa sayari
  2. mwezi (wakati) - mojawapo wa vipindi kumi na mbili vya mwaka

Yote mengine yafuate katika makala yenyewe.

Kuingiza maelezo marefu katika makala ya "maana" si vizuri.

Pia kuchanganya maana 2 katika makala moja haitakiwi. Hapa inatokea kirahisi ya kwamba mtumiaji mwingine inaanzisha makala mpya juu ya jambo linalotajwa tayari katika makala ya mchanganyiko.

10 Kutojali makala zilizopo tayari na umbo la majina

Wakati wa kuandika makala tunaweza kutafsiri neno kutoka lugha nyingine; tunatafuta namna ya kutaja jambo kwa Kiswahili. Kumbe jambo hili limeshaelezwa katika wikipedia hii. Kwa hiyo ni vema kuchungulia kama kitu kimetajwa tayari kwa sababu hii inatuwezesha kuweka viungo kwenda makala nyingine ambavyo ni thamani kubwa katika kamusi yetu. Makosa yale hutokea hapa lakini wengine hawajali na kutojaribu hata kidogo. Kutaja jambo tofauti na makala mengine huleta matata kwa wasomaji na kunazuia nafasi ya kuweka viungo. Tunatakiwa kuepukana na tatizo hilo.

Tazama pia