Bendera ya Kamerun

Bendera ya Kamerun ina milia mitatu ya kusimama yenye rangi za kijani-nyekundu-njano pamoja na nyota njano ya pembetano katika mlia wa katikati.

Bendera ya Kamerun

Muundo wa bendera hufanana na bendera ya Ufaransa (Kamerun ilikuwa koloni yake) lakini inatumia rangi za Umoja wa Afrika.

Kamerun iliingia katika uhuru na bendera tofauti kidogo. Muundo na rangi zilekuwa zilezile lakini mlia wa kwanza (ya rangi kijani) ulionyesha nyota mbili zilizoonyesha Kamerun ilikuwa shirikisho la jamhuri baada ya kuungana sehemu mbili tofauti za Kamerun ya awali. Koloni ya Kijerumani ya Kamerun ilipasuliwa 1918 ikiwa sehemu kubwa ilikuwa chini ya Ufaransa na sehemu ndogo chini ya Uingereza. Kanuni za Umoja wa Mataifa zililazimisha Waingereza kushauriana na wenyeji wenyewe badala ya kuunganisha sehemu zao za Kamerun na Nigeria tu jinsi ilivyowahi kupangwa awali. Matokeo ya kura yalisababisha sehemu zilizotengwa kuunganishwa tena. Hivyo Kamerun ilianzishwa kama shirikisho la jamhuri hali iliyoonyeshwa kwa nyota mbili.

1972 serikali ilibadilisha katiba ya Kamerun ikawa nchi ya umoja, bila shirikisho. Nyota mbili zilifutwa na badala yake nyota moja katika mlia wa katikati ikaonekana kwa jina la "nyota ya umoja".