Biafra
Biafra ilikuwa jamhuri iliyojitenga na Nigeria kati ya 1967 hadi 1970 iliyotambuliwa na nchi chache tu na kurudishwa Nigeria baada ya vita kali. Eneo la Biafra ilikuwa katika kusini-mashariki ya Nigeria inayokaliwa na Waigbo hasa wakati ule lilitwa "Mkoa wa Mashariki" lililokuwa moja kati ya mikoa mitatu ya Nigeria baada ya uhuru.
Sababu za farakano
haririUasi wa kijeshi
haririKatika Januari 1966 ilitokea ghasia katika Nigeria. Sehemu za jeshi zilipindua serikali wakamwua waziri mkuu Abubakar Tafawa Balewa aliyekuwa wa asili ya kaskazini. Kiongozi wa serikali mpya alikuwa jenerali mkuu wa jeshi la Nigeria Johnson Aguiyi-Ironsi aliyekuwa Igbo ambaye mwenyewe hakushiriki katika uasi. Lakini katika miji ya kaskazini ya Nigeria raia Waigbo walitafutwa na kuuawa ovyo. Waigbo maelfu walikimbia katika miji ya kaskazini na kukimbilia kwao nyumbani walipoleta habari za mauaji.
Uasi wa pili ulifuata haraka tarehe 29 Julai 1966 na safari hii kikundi cha maafisa kutoka kaskazini walimwua Ironsi na kuchukua serikali mkononi mwao chini ya uongozi wa jenerali Yakubu Gowon. Mwaka uliofuata 1967 serikali mpya ilianza kubadilisha muundo wa utawala; mikoa mitatu ya Nigeria iligawiwa kuwa majimbo 12. Waigbo walisikitika ya kwamba mipaka ilichorwa kwa kusidi la kuacha maeneo ya Delta penye mafuta ya petroli nje ya majimbo penye Waigbo wengi. Ili ilitazamiwa kama jaribio la kuwatenga Waigbo na malighafi hizi.
Azimio la farakano
haririMwaka huohuo wa 1967 mauaji mapya ya Waigbo yalitokea katika kaskazini. Katika hali hii afisa kiongozi wa jeshi katika mkoa wa mashariki kanali Emeka Ojukwu tar. 30 Mei 1967 alitangaza uhuru wa mkoa wa mashariki ulioitwa sasa "Jamhuri ya Biafra". Nchi chache tu zilitambua nchi mpya zilikuwa Gabon, Haiti, Côte d'Ivoire, Tanzania na Zambia.
Vita ya wenyewe kwa wenyewe
haririVita ya miaka mitatu ilianza 6 Julai 1967 jeshi ka serikali ya Nigeria iliposhambulia. Serikali ya Lagos ilipata msaada kutoka Urusi na Uingereza. Ufaransa, Ureno na Afrika Kusini zilisaidia upande wa Biafra lakini bila kutambulia nchi rasmi. Usaidizi hasa wa Urusi uliotoa ndege za kijeshi za aina Ilyushin IL-28 na mabomu ya Napalm uliwapa Wanigeria nguvu zaidi. Jeshi la anga la Biafra ilikuwa na ndege ndogo tu za kiraia zilizobadilishwa kubeba silaha.
Vita ilisababisha njaa kali na wakazi milioni 2 - 3 wa Biafra walikufa kutokana na njaa na magonjwa. Tarehe 13 Januari 1970 mabaki ya jeshi la Biafra yalijisalimisha mjini Amichi. Rais Ojukwu alikimbia kwenda Côte d'Ivoire.
Upatanisho
haririBaada ya mwisho wa vita hofu ilikuwa kubwa ya kulipizwa kisasi lakini serikali ya Lagos ilijitahidi kujenga upatanisho na amani upya. Ojukwu alirudi Nigeria mwaka 1980.