Daphne Marjorie Sheldrick (4 Juni 1934 – 12 Aprili 2018) alikuwa mwandishi, mhifadhi, na mtaalamu wa ufugaji, hasa ufugaji wa tembo yatima. Sheldrick alikuwa mwanamke wa kwanza kulea tembo wachanga wa Afrika kwa mafanikio na kuwafundisha jinsi ya kuishi katika mazingira ya asili. Alikuwa mwanzilishi wa Sheldrick Wildlife Trust, mojawapo ya programu zilizofanikiwa zaidi katika uokoaji na uhifadhi wa tembo yatima duniani.

Daphne Marjorie Sheldrick
Amezaliwa 4 Juni 1934
Kenya
Amekufa 12 Aprili 2018 (umri 83)
Nairobi, Kenya
Anajulikana kwa ajili ya Sheldrick Wildlife Trust
Ndoa David Sheldrick
Watoto Gillian Woodley (binti), Angela Sheldrick (binti)

Maisha ya Awali

hariri

Daphne Jenkins alizaliwa nchini Kenya mwaka wa 1934 na wazazi Waingereza, wakati ambapo Kenya ilikuwa bado chini ya ukoloni wa Waingereza. Wazazi wake, Bryan Jenkins na Marjorie Webb Jenkins, walikuwa na shamba kubwa na biashara ya mbao huko Gilgil, ambao ni mji katika Kaunti ya Nakuru, Kenya.

Katika Vita ya Pili ya Dunia, babake, mwanasayansi wa asili, alipelekwa kwenye mbuga ya wanyama ambako aliamriwa kuua pundamilia na nyumbu ili kulisha askari wa Uingereza na Kenya. Mwaka 1940, akiwa na umri wa miaka 6, Daphne alienda kuitembelea kambi ya baba yake na kufikiri, "Hivi ndivyo ningependa kuishi, hapa nje kati ya wanyama chini ya anga."

Alisoma katika Shule ya Msingi ya Nakuru na Shule ya Upili ya Kenya High. Alipata nafasi ya kwenda chuo kikuu lakini alichagua kuolewa.

Miaka ya Baadaye

hariri
 
Tembo yatima wa Daphne Sheldrick huko Nairobi, Kenya

Mwaka 1953, aliolewa na Bill Woodley, ambaye alipigania kusitisha ujangili wa wanyamapori katika mbuga za wanyama za Kenya, lakini waliachana. Tarehe 20 Oktoba 1960 Daphne Sheldrick aliolewa na bosi wa Woodley, David Sheldrick.

Kuanzia 1955 hadi 1976, alikuwa msimamizi wa Mbuga ya Kitaifa ya Tsavo pamoja na mume wake. Walianza kutunza kila aina ya wanyama yatima. Lengo lao lilikuwa kuwaunganisha wanyama hawa tena porini. Wanyama wengi walikuwa tembo wachanga na Daphne Sheldrick alianza kuwalisha kwa mkono fomyula ya maziwa, ambao aliitengenza mwenyewe. Alipowapa tembo maziwa ya kawaida, walikufa au walipata utapiamlo. Baada ya kupambana na kansa ya matiti kwa muda, Daphne Sheldrick alikufa na umri wa miaka 83.

 
Mtu anampa mtoto tembo maziwa katika Sheldrick Wildlife Trust

Sheldrick Wildlife Trust

hariri

Sheldrick Wildlife Trust ni shirika la uhifadhi, linalojitolea kwa ulinzi wa wanyamapori na uhifadhi wa makazi yao katika Afrika Mashariki. LIlianzishwa na Daphne Sheldrick mwaka 1977 baada ya kifo cha mumewe. Misheni ya shirika ni kuchunguza hatua zote zinazosaidia uhifadhi na ulinzi wa wanyamapori na makazi. Hatua hizi ni pamoja na kupambana na ujangili, kulinda mazingira ya asili, kuongeza ufahamu wa jamii, kushughulikia matatizo ya ustawi wa wanyama, kutoa huduma ya utabibu wa mifugo, na kuokoa yatima wa tembo na vifaru. Sheldrick Wildlife Trust hufanya kazi pamoja na Huduma ya Wanyamapori ya Kenya, Huduma ya Misitu ya Kenya na jamii zinapakana na Hifadhi za Kitaifa za Kenya. Baada ya kifo cha Daphne Sheldrick mwaka 2018, binti yake, Angela Sheldrick, aliendelea na misheni ya Sheldrick Wildlife Trust.

Mafanikio

hariri

Kwa kazi yake kama mhifadhi, Sheldrick alipatiwa tuzo ya Most Excellent Order of the British Empire na Malkia Elizabeth II mwaka 1989. Na badaaye mwaka 2006, Malkia Elizabeth II alimpandisha Sheldrick cheo na kuwa Dame Commander of the Order of the British Empire, kwa huduma za uhifadhi wa wanyamapori. Alikuwa wa kwanza kupokea tuzo hii nchini Kenya tangu nchi hiyo ilipata Uhuru mwaka 1963.

Marejeo

hariri