Joseph Narcis Mloka

Joseph Narcis Mloka (19302004) alikuwa mshairi kutoka Tanzania.

Mloka alizaliwa katika kijiji cha Utunu, Matombo, wilaya ya Morogoro Vijijini, mwaka 1930, akiwa mtoto wa kwanza katika familia ya watoto wanne: Sabina Narcis, (Balozi) Daniel Narcis Mloka (1938 – 1994), na Andrew Narcis Mloka (1942 – 2010).

Baba yao, Narcis Bambalawe, aliyefariki mwaka 1976, aliajiriwa na Serikali ya Kikoloni wakati wa utawala wa Mwingereza, nchini Tanganyika, akiwa mhudumu katika soko la kuu la Mtamba, Matombo mkoani Morogoro.

Mama yao, Anna Segumba, aliyefariki mwaka 1994, alikuwa mkulima.

Narcis Bambalawe, ni mtoto wa mwisho wa Bambalawe Mwanamene (Bambalawe wa XII), aliyeitawala Matombo kabla na baada ya ukoloni, mtawala ambaye alikuwa na karama mbalimbali kama vile kujigeuza kama nyenyele shimoni alipotafutwa na wakoloni, kuigeuza Matombo kuwa msitu wakati wakoloni walipotaka kutawala, kuhamisha kidonda kutoka kwenye sehemu ya siri na kukiuguzia sehemu ya kawaida, n.k.

Joseph Narcis Mloka, alizaliwa katika kizazi kilichokuwa na karama ya uandishi.

Nduguye, Daniel alichapisha vitabu kadhaa katika maisha yake kikiwemo, Baharia Bila Meli , The Cock Tail , Operesheni Pata Potea na vinginevyo.

Aidha, Andrew, alikuwa mwandishi wa hadithi fupi kadhaa za Kiingereza zilizokuwa zikichapishwa katika magazeti ya Daily News na Sunday News katika miaka ya themanini na tisini.

Joseph alipata elimu yake ya msingi, darasa la kwanza hadi la nane, kati ya mwaka 1942 hadi 1949, katika Shule ya Kati ya Kigurunyembe, mjini Morogoro.

Alipohitimu mafunzo yake ya elimu ya msingi, alisomea ualimu.

Alihitimu kozi ya ualimu na kuanza kazi ya ualimu na kuendelea nayo katika mbalimbali za kati (Middle Schools), mnamo mwezi Novemba, 1950.

Aidha, mwaka 1953 alifundisha katika Shule ya Kati ya Matombo (Matombo Middle School).

Mwaka huo huo wa 1953 alichukua mafunzo ya kilimo huko Hehile, Lushoto mkoani Tanga na kurejea tena Matombo kuwa Mwalimu Mkuu.

Tarehe 8/10/1953 alifunga ndoa na Theresia Wilbert Mpangalala katika Kanisa Katoliki la Mt.Paulo Matombo, Morogoro.

Kati ya mwaka 1956-57, Marehemu Joseph, alichukua mafunzo ya mwaka mmoja ya chuo cha kilimo Tengeru Arusha.

Baada ya kuhitimu mafunzo hayo aliteuliwa kuwa mwalimu wa kilimo katika Shule ya Kati ya Lugoba, Chalinze mkoa wa Pwani, 1958-1961 akiwa na Mwl.Joseph Kunambi.

Miongoni mwa wanafunzi wake waliokuwa katika shule hiyo, ni Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete

Kati ya mwaka 1962-1964 alikuwa mwalimu wa kilimo katika Shule ya Kati ya Kidodi, Wilaya ya Kilombero.

Kufuatia kuanzishwa kwa shule za msingi, alihamishiwa shule ya msingi Mtombozi akiendelea kuwa mwalimu wa kilimo, tangu 1964-1970.

Mwaka 1970 alihamishiwa shule ya msingi Mkulazi, tarafa ya Ngerengere ambako alifundisha kwa miezi sita. Mwaka huo huo (1970) alihamishiwa shule ya msingi Tununguo, Tarafa ya Ngerengere.

Mwanzoni mwa miaka ya themanini alihamishiwa shule ya Msingi Matombo.

Aidha, miaka hiyo hiyo alifundisha katika shule ya msingi Kifindike, Matombo.

Alistaafu kazi ya ualimu mwaka 1985 na kati ya mwaka 1987-1988 alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kijiji cha Kiswira, Matombo.

Ni katika kipindi chake hicho cha uenyekiti ndipo alipopata nafasi ya kuishawishi serikali kuanzisha Shule ya Sekondari ya Matombo.

Mbali ya kazi yake ya ualimu, alikuwa mtunzi na mghani mahiri wa nyimbo na mashairi.

Aliianza sanaa hii akiwa katika Shule ya Kati ya Kidodi.

Alitunga shairi lake la kwanza mwaka 1962 lililoitwa “PONGEZI KUPATA UHURU.”

Mashairi yake mengine ni: Azimio la Arusha, Heko twakupa pongezi Julius Kambarage na Maganga ale dona, yaliyochapishwa katika gazeti la Kiongozi kwa nyakati mbalimbali.

Lakini pia alikuwa mwanafasihi simulizi aliyependa sana kuwasimulia watoto wake hadithi fupi mbalimbali zikiwemo hadithi ya Chaukaange, Chang’amwatsi Udodo Ung’ali (Katembea uchi akiwa bado mdogo) na nyingine nyingi.

Watoto wake ni Antonia Joseph Mloka (1954 – 1999), Charles Joseph Mloka, Blandina Joseph Mloka (1960 – 2000), Peter Joseph Mloka, Daniel Joseph Mloka, Michael Joseph Mloka na Gerald Joseph Mloka.

Aidha, alishiriki kutunga na kuimba wimbo maarufu wa Kiluguru uliotamba katika sherehe za kitaifa, Matombo, ulioitwa, “BABA MWENDA AGAMAFUTA GAMKOMILE!” Wimbo huu ulikuwa ulikuwa ukimzunguzia na kumlaani mkoloni (Baba Mwenda) jinsi alivyolazimika kukabidhi uhuru kwa Watanganyika baada ya kusalimu amri kutokana na tamaa yake iliyokithiri ya kutamani mali zetu (agamafuta gamkomile – mafuta au mali zetu ndizo zilizomponza).

Kutokana na kujishughulisha sana na sanaa hii alikuwa mmoja kati ya walimu mahiri wa Kiswahili na jitahada zake zimemfanya ateuliwe kwenye kamati mbalimbali za Kiswahili za wilaya ya Morogoro kwa wakati huo.

  Makala hii kuhusu mwandishi fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Joseph Narcis Mloka kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.