Mzee Kipala

TANGAZO LA KIFO cha
Ingo Koll au Kipala kilichotokea tarehe 10, Julai, 2023 nchini Ujerumani. Kipala alikuwa mchangiaji mashuhuri wa Wikipedia kuanzia Disemba 2005 hadi Juni 28, 2023. Siku kumi na mbili mbele tangu kuhariri Wikipedia yetu kwa mara ya mwisho, Mola Jalali Muumba wa mbingu na ardhi, alitwaa kiumbe chake. Kipala atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa wa kuhariri Wikipedia hii. Kwanza akiwa kama msimamizi (admin) baadaye mrasimu (bureaucrat) ambaye ametoa haki za usimamizi kwa wakabidhi ama wasimamizi wengine kama Muddyb, Antoni na wengine wengi tu. Miaka kumi na nane ya kusimamia na kutunga makala mbalimbali itakumbukwa hadi mwisho wa dunia ya Wikipedia. Kipala amechangia makala za aina mbalimbali ikiwemo, muziki, filamu, tiba, elimu ya nyota, dini, siasa, demografia, jiografia, sayansi, na mengine mengi. Amepata kuwa msaada mkubwa kwa wachangiaji wapya kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Alianzisha Jenga Wikipedia ya Kiswahili kwa lengo la kuboresha makala mbalimbali na kutoa mafunzo kwa watu wapya. Pengo lake halitazibika. Sisi wanajumuia ya Wikipedia ya Kiswahili tunasikitika kutangaza kifo chake!