Jina la Kuzaliwa Lovy Longomba
Tarehe ya Kuzaliwa Septemba 25, 1953
Tarehe ya Kufa Mwaka 1996
Kazi Yake Msanii wa muziki
Mwenza Mado Zaina
Watoto Ellie Longomba (Ke), Christian Longomba (Me) and Longomba Elias (Me)
Ndugu Awilo Longomba (mdogo wake)
Utaifa DRC (zamani Zaire)
Sababu ya Kifo Ajali ya gari
Mahali Alipofia Mombo, wilayani Korogwe, Tanga, Tz.
Majina Mengine ya mamman

Lovy Longomba (Septemba 25, 1953 - 1996) alikuwa msanii wa muziki wa rumba mwenye asili ya nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (zamani ilijulikana kama Zaire au Congo - Kinshasa)[1].

Alikuwa mtoto wa mwanamuziki maarufu wa Congo Kinshasa, Vicky Longomba (jina halisi ni Victor Longomba Basange Lokuli), ambaye ni mmoja wa waasisi wa kundi maarufu la T.P. O.K. JAZZ. Lovy alikuwa kaka wa Awilo Longomba.

Mwanzo wa safari yake ya kimuziki

hariri

Lovy alianza kujihusisha na muziki mnamo mwaka 1976 alipojiunga na kundi la Orchestre Macchi la mjini Kinshasa. Katika bendi hiyo, alikuwa pia na mwanamuziki Dindo Yogo. Hakudumu sana kwenye kundi hilo kwani miezi si mingi baadae, alishirikiana na wanamuziki wengine na kuunda kundi jipya lililojulikana kama Orchestre Etumba na Ngwaka.

Mnamo mwaka 1978 Lovy aliondoka Kinshasa na kwenda Nairobi, Kenya. Huko alijiunga na kundi lililojulikana kama Orchestre Les Kinois. Kutokana na kipaji chake, bendi nyingine iliyokuwa na ushawishi zaidi, ilimchukua ikiwa ni miezi 3 tu tangu ajiunge na Les Kinois. Kundi hilo la pili lilijulikana kama Bana Liwanza.

Hata hivyo, Bana Liwanza nao hawakubahatika kupata huduma za kijana mwenye kipaji na sauti tamu, nyororo; Kwa muda mrefu kwani baada ya nusu mwaka tu kupita, Lovy alijiunga na Orchestre Super Mazembe. Wakati huo kiongozi wa Mazembe alikuwa Mutonkole Longwa Didos.

Mafanikio kimuziki

hariri

Lovy alipata kufahamika zaidi katika nchi za Afrika ya Mashariki ya wakati ule (Tanzania, Kenya na Uganda) zaidi ya alivyofahamika nchini mwake. Hiyo ni kutokana na kufanya kazi yake ya muziki kwa miaka mingi akiwa ndani ya Afrika Mashariki.

Umaarufu wa Lovy ulishamiri nchini Kenya alipojiunga na kundi la Orchestre Super Mazembe la jijini Nairobi. Maarufu kama 'Super Mazembe', ni kundi lililoanzishwa nchini Congo Kinshasa ya wakati huo Kwa jina la Super Vox (mwaka 1967) na baadae kuhamia nchini Kenya, mwaka 1974. Lovy hakuwa mmoja wa waasisi wa kundi hilo lakini alijiunga nao baadae (mwishoni mwa 1978/1979 mwanzoni).

Ni katika Super Mazembe ambapo ulimwengu ulimtambua vema Lovy. Sauti yake nyembamba, ya juu na nyororo, ilimfanya apewe jina la utani la ya mamman. Sauti yake ilikuwa na ladha iliyozidi sauti za kike. Si uzuri wa sauti tu bali Lovy alikuwa mtunzi hodari pia.

Miongoni mwa vibao alivyotunga na kuimba ama kushiriki kuimba akiwa Kenya, na viliwika ni pamoja na Pitie, Mado Zaina, Tika Nalela, Annie, Ouma, Elee, Lovy,

Kuondoka Super Mazembe

hariri

Lovy aliondoka Super Mazembe mnamo mwaka 1985 wakati kundi hilo lilivunjika. Akaenda kuanzisha bendi yake ya Super Lovy na baadae Bana Likasi. Makundi hayo hayakudumu sana.

Baadae Longomba alikwenda nchini Tanzania kujiunga na kundi la Orchestra Maquis Original (zamani Orchestre Maquis du Zaire). Maquis ilikuwa bendi iliyomilikiwa na Wakongo wa Kitanzania. Sifa zao zilikuwa sawa na Lovy yaani kuishi na kufanya kazi nje ya Kongo kwa miaka mingi.

Lakini baada ya kufika Dar Es Salaam na kuwasiliana na wana Maquis, Plan A ilishindikana kwani Maquis walijibu kuwa uimbaji wa Lovy ulikuwa hauswihi ndani ya bendi hiyo. Ndipo mwenyeji wake mkuu Bw. Skassy Kasambula alipomuunganisha na Bw. Juma Mwendapole, kama Plan B ambaye wakati huo alikuwa katika harakati za kuisuka bendi yake ya Afriso.

Alivyoipagawisha Tanzania

hariri

Mnamo mwaka 1986 , Lovy alihamia Tanzania na kulianzisha, pia kuliongoza kundi la muziki lililojulikana kama The African Sound Orchestra, maarufu zaidi kwa finyanzo la jina hilo, yaani AFRISO [Ngoma][2]. Ukubwa wake kimuziki pamoja na umahiri wake vilimfanya awe mbuyu wa bendi. Watu wengi walijua kuwa yeye ndiye aliyekuwa mmiliki wa bendi. Baadae sana (miaka ya 2010) ndipo watu wakajulishwa kuwa mmiliki wa bendi alikuwa mzee Juma Mwendapole wa Msasani, Dar Es Salaam.

Akiwa na Afriso Ngoma, Dar ilitikisika. Safu ya mwanzo ya bendi hiyo iliwajumuisha yeye mwenyewe Lovy, Kinguti System, Anania Ngoliga, Kassim Mponda, Maneno Uvuruge, Kasile, Mawazo, Kalamazoo, na wengine[1]. Miongoni mwa vibao vilivyowapa sifa nyingi ni pamoja na Salima, Kaibego, Kigeugeu, Ellie, nk. Kibao Ellie kilichukua jina la binti yake Ellie Longomba.

Lovy na familia

hariri

Lovi Longomba alikuwa na mke aliyeitwa Mado Zaina. Tungo kadha za mwanamuziki huyu zinaakisi mapenzi yake kwa mkewe. Mado alitajwa naye katika nyimbo kwenye tungo alizofanya akiwa Kenya, hali kadhalika akiwa Tanzania na Afriso Ngoma. Wawili hao walijaliwa kupata watoto watatu: Elly Longomba, Christian Longomba na Lovy Longomba Junior. Christian na Lovy Jr. walikuwa mapacha.

Watoto hao wote walibarikiwa vipaji vya muziki na walifanya vizuri katika tasnia ya muziki. Kwa sasa, familia hiyo mashuhuri iliyokuwa ya watu watano, amebakia Lovy Longomba Junior tu, ambaye ameacha shughuli za muziki wa kidunia na anafanya shughuli za kiuchungaji (dini) nchini Marekani[3].

Mado Zaina alifariki mwaka 2017 na kuzikwa katika makaburi ya Lang'ata (Nairobi) nchini Kenya. Hiyo ilikuwa ni baada ya kupitia katika kipindi cha changamoto kubwa (alihukumiwa kifungo cha maisha nchini Pakistani)[4]. Elly Longomba alifariki nyuma zaidi, na Christian alifariki Machi 13, 2021[5].

Kufariki

hariri

Lovy Longomba alipata ajali mbaya ya gari akiwa safarini kutoka Kenya kuelekea Dar es Salaam. Ilivyoelezwa, Lovy alipanga safari ya kuelekea nchini Tanzania kutokea Kenya. Lakini, hakuwa amefanya booking, hivyo hakuwa na kiti. Kwa kuwa alikuwa anafahamika, mhudumu wa basi (Coastal) alimpa kigoda akalie, eneo la mbele karibu na dereva. Ajali ilipotokea katika eneo la Mombo ambalo liko karibu na Same mkoani Kilimanjaro, Tanzania, Lovy aliathirika sana. Hiyo ilikuwa mwaka 1996. Majeraha makubwa aliyopata yalichangia kifo chake.

Ni jambo la kiungwana kumalizia makala hii kwa kuwataja mabwana Masoud Masoud, Adam Zuberi, Zomboko Rajab, Moshy Kiyungi, gazeti la Uelekeo kadhalika tovuti za wadau wa rumba wa Kenya kwa juhudi zao za kuhifadhi habari za wanamuziki na marejeo mengine.

Marejeo

hariri
  1. 1.0 1.1 https://www.discogs.com/artist/1336990-Lovy-Longomba
  2. france (2015-12-19). "'Kinguti System' nyota inayongaa nchini Thailand". Mtanzania (kwa American English). Iliwekwa mnamo 2024-05-31.
  3. https://www.vanguardngr.com/2020/11/the-artiste-formerly-known-as-lovy-longomba-jnr/
  4. "'My mum was framed, arrested and jailed in Pakistan,' Lovy Longomba reveals". Mpasho (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2024-06-01.
  5. "Longombas member Christian dies aged 36". Music In Africa (kwa Kiingereza). 2021-03-15. Iliwekwa mnamo 2024-05-31.
  Makala hii kuhusu mwanamuziki fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Lovy Longomba kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.