Manikongo (pia: Mwene Kongo au "mwenye Kongo" yaani "Bwana wa Kongo") ilikuwa cheom cha mtawala wa Ufalme wa Kongo kati ya karne za 14 hadi 18 katika maeneo ambayo leo ni sehemu za Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mchoro wa Manikongo.

Mji mkuu wa Manikongo ulikuwa M'banza-Kongo (iliitwa baadaye Sao Salvador kati ya 1570-1975) ambayo leo ni makao makuu ya jimbo la Zaire la Angola.

Hakuna uhakika umbo la neno lilitokea namna gani labda lilikuwa tu njia ya Wareno ya kuandika "Mwene Kongo". Lakini umbo hilo lilitumika katika maandiko na nyaraka zilizotumwa kati ya Manikongo na Wafalme wa Ureno zilizohifadhiwa hadi leo.

Mwene Kongo alichaguliwa na akina "bambuta" au wazee wa ufalme. Vyeo mbalimbali chini yake viligawiwa kufuatana na mapokeo kati ya wawakilishi wa koo muhimu.

Manikongo wa kwanza alikuwa Lukena lua Nimi (1380 - 1420) aliyeanzisha ufalme.

Nzinga Nkuwu (1482-1505) alikuwa mwene Kongo wa sita aliyeanza kuwasiliana na Ureno. Akawa Mkristo mwaka 1491 na kutumia jina la Kireno João I (Yohane I).

Mfalme wa mwisho wa Kongo huru alikuwa Pedro V (1859-1891) aliyepaswa kukubali ubwana wa mfalme wa Ureno.

Uwezo wa Manikongo ulipungua kadiri jinsi uwindaji wa watumwa uliharibu utaratibu wa ndani na kuwapa wakubwa moyo kupinga mamlaka ya mfalme.

Baada ya mwisho wa ufalme cheo kimeendelea kwa maana ya kiutamaduni hata wakati wa ukoloni na uhuru.

Viungo vya Nje hariri