Mkoa wa Rufiji (DOA)
Mkoa wa Rufiji ulikuwa mkoa mmoja kati ya mikoa 21 ya koloni ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani (DOA, Deutsch Ostafrika) iliyokuwa mtangulizi wa nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi wa leo.
Mkoa huu ulikuwa na eneo la kilomita za mraba 12,000 kwa pande zote mbili za mto Rufiji kutoka mdomo hadi takriban kilomita 180 kwenda juu, karibu na mdomo wa mto Ruaha Mkuu katika Rufiji. Makao makuu (jer. Bezirksamt) yalikuwepo mwanzoni pale Mohoro lakini yalipelekwa Utete kwenye mwaka 1913.
Mkoa huu ulipakana na
- Mkoa wa Dar es Salaam (V kwenye ramani) upande wa kaskazini
- Mkoa ya Morogoro (VII) upande wa kaskazini-mashariki,
- Mkoa wa Kilwa (VIII) upande wa kusini
Mwaka 1913 kulikuwa na wakazi 89,000, kati hao Wajerumani walihesabu 269 "watu wa rangi wasio wazalendo" (hivyo waliita kwa kawaida Wahindi au Waarabu) na Wzungu 61. Mifugo ilikadiriwa kuwa ng'ombe 520 wa wenyeji na 258 wa Wazungu, na kwa jumla takriban mifugo wadogo kama mbuzi 4500.
Kabla ya 1914 yalikuwepo makampuni 3 ya kizungu na walowezi 5 walioanzisha mashamba ya kibiashara ya pamba na miti ya mpira. Maduka 60 yaliendeshwa na Wahindi. Huko Mpaganya kulikuwa na shule ya mafunzo ya kilimo cha pamba.
Wakati wa Wajerumani hapakuwa na barabara nzuri kwa hiyo usafiri ulitegemea hasa njia ya maji kwenye mto Rufiji. Wakati wa mvua merikebu ndogo ya moshi iliweza kusafirisha mizigo ya takriban tani 30 hadi kilomita 200 juu ya mdomo wa mto, wakati wowote hadi kilomita 160.
Marejeo
hariri- [http://web.archive.org/20200928193610/http://www.ub.bildarchiv-dkg.uni-frankfurt.de/Bildprojekt/Lexikon/php/suche_db.php?suchname=Kilwa Ilihifadhiwa 28 Septemba 2020 kwenye Wayback Machine. "Rufiji, 2. Bezirk", makala katika Kamusi ya Koloni za Kijerumani]