Msaada:Tafsiri ya kompyuta

Tafsiri ya kompyuta ni njia ya kuunda makala ambayo inaweza kusaidia kukuza Wikipedia hii haraka lakini mpaka sasa imeonekana zaidi ni hatari kwa ubora na hadhi ya Wikipedia ya Kiswahili. Matokeo yake mara nyingi ni makala ambazo hazieleweki au zina makosa mazito ya lugha au maudhui.

Programu ya kutafsiri ni chanzo cha makosa

hariri

Watumiaji wengi, hasa wageni, hutumia tafsiri ya kompyuta bila kuhakikisha usahihi wa matini inayopendekezwa na programu. Hadi sasa hakuna programu ya kutafsiri inayoweza kutafsiri bila makosa.

Chanzo cha makosa ni hasa:

  • Muundo wa sentensi, hasa sentensi ndefu
  • Chaguo la maneno, hasa kama neno moja lina maana tofautitofauti, ambalo ni jambo la kawaida.

Tufanye nini?

hariri
  1. Kama makala ina lugha isiyoeleweka au ya ajabuajabu ni vema kuangalia makala yake ya Kiingereza, maana mara nyingi ni tafsiri ya kompyuta ya sehemu ya makala katika enwiki.
  2. Tupime kama ni tafsiri ya kompyuta kwa kutumia translate.google.com. Tumwage sehemu ya makala ya Kiingereza upande wa dirisha la kwanza (tunapochagua "English") na kuangalia tafsiri yake.
  3. Tulinganishe matokeo na matini ya makala ya swwiki tunayochunguza. (Njia rahisi ni: anzisha jedwali katika word, mwaga tafsiri upande mmoja na makala ya swwiki upande mwingine)
  4. Tukihakikisha makala ya swwiki ni matini imepokewa neno kwa neno kutoka google, na Kiswahili kina kasoro, makosa au hakieleweki, tunaamua kama tunaweza kuisahihisha (au kama tunapenda kutumia muda wetu kwa jambo hilo) halafu ama tunasahihisha au tunabandika kigezo cha {{futa}} na kuandikisha makala katika orodha ya Wikipedia:Makala kwa ufutaji (kwa kubofya link yake), ambapo mwingine ataiangalia na kuamua.
  5. Wakabidhi kati yetu wataamua kumzuia mwandishi wa makala kwa kutumia kigezo {{zuia tafsiri}} kinachoonyeshwa hapa chini; kwa njia hiyo mwandishi anapata nafasi ya kuwasiliana na kupokea ushauri lakini hawezi kuendelea bila mawasiliano.
  6. Watumiaji wageni husahau mara kwa mara kuonyesha interwiki kwa hiyo hatujui walitafsiri nini kutoka enwiki. Mara nyingi tunaweza kutambua makala husika ya enwiki kwa kutumia google translate (maana huko walichukua jina). Tubadilishe google translate iwe SW > EN na kumwaga jina la Kiswahili katika dirisha la kwanza. Halafu tutafute tafsiri katika enwiki. Kama hatufiki kwa njia hiyo, tunaweza bado kuangalia kama matini ya enwiki ina jina la mtu n.k. na kuiweka katika dirisha la "Search Wikipdia" tukibofya chini "Search for pages containing ..." na uwezekano ni mkubwa kwamba tutakuta makala tunayotafuta.
Taarifa ya kukuzuia!

Ndugu, imenibidi kukuzuia kwa sababu zinazotajwa chini. Wakati unapokuwa umezuiwa huwezi kuhariri isipokuwa penye huu ukurasa wako wa majadiliano. Unaweza kunijibu kwa kutumia “Email this user”.

Sababu ni kuwa umeingiza matini iliyopatikana kwa njia ya tafsiri ya kompyuta ikiwa na kasoro nzito ya lugha. Umearifiwa kwamba ni marufuku kumwaga matokeo ya google translate katika makala zetu. Wachangiaji wanaopuuza utaratibu huu wanasababisha hasara kubwa kwa Wikipedia yetu na kuwapa wengine kazi kubwa mno ya kusafisha makosa yao.

Bila shaka una nia nzuri kuchangia katika Wikipedia. Tutafurahi kushirikiana nawe lakini ni lazima ufuate utaratibu. Kazi yetu kama wakabidhi ni kulinda mradi huu.

Ukiwa tayari kufuata utaratibu pamoja na kupitia upya matini ulizozileta tayari, naomba uwasiliane nami kwa kufungua ukurasa wangu (bofya jina langu chini) na kuniandikia baruapepe kwa kubofya “Email this user” upande wa kushoto. Hapo nitaweza kukuruhusu tena. Hapo lazima uwezeshe njia kwa kufuata maelezo katika Wikipedia:Email.

Nifanye nini ili nitumie vema programu ya kutafsiri?

hariri

Soma hapa: Msaada:Tafsiri#Programu_za_kutafsiri