KWC Mtumiaji huyu ni mwanafunzi katika JKUAT.
KWC Mtumiaji huyu ni mshiriki katika Shindano la Wikipedia ya Kiswahili la 2009.   (Submissions)


HAKUNA KAMA MAMA Mama, ama kwa hakika jina mama kwa baadhi ya viumbe halina uzito katu katika maisha yao. Nataka ukae kitako, utafakari, utie ukitoa, uwaze ukiwazua na upime uzito wa jina hili mama. Mwenye macho haambiwi tazama na na asiye na mwana aelekee jiwe. Ni jambo makhsusi na kwa moani yangu, nimeonelea niwapeleke ila simwingine, ni mwendo ule ule wa kobe , maana ulinifikisha mbali japo wengine walitutangulia wakasema chelewa chelewa utapata mwana si wako. Kwa mukhtasari, nitagusia katika vipande vya maisha yangu na kufanya wazi uzito wa jina mama. Yaliyo nisibu na baadhi ya mambo yaliyotendwa na nina kunilea hadi nilipofika bado ningali nayafahamu mithili ya sehemu ya juu ya kiganja cha mkono.

Tafakari kwa makini tukipiga mfano, mwanamke mja mzito, mwendo wake hauna tofauti na ule wa kobe hasa zikikaribia siku zake zakukuleta katika mazingira ya ajabu. Akila huchagua, anapokaa na kusimama huwa mwangalifu ili asikuumize mgeni mashuhuri na huku mikono kwa uchache, mara tano kwa siku humuomba Maulana akustiri wewe unayeenda mbio leo hii ungali matumboni. Yote aliyafanya mwanake kukuhifadhi usipatikaniwe na janga lolote lile ambalo litakukosesha wewe kukosa kuja katika mazingira ya kilimwengu. Maumivu yakimkumba kidoleni, huwa dukuduku la moyo lisha mvaa, kwa wakati huu, huwa hasiki la muadhini wala la mteka maji msikitini. “Mwanangu yu matatani!” ndivyo anavyo tamka. Yuwapelekwa hospitalini ama mganga aletwe nyumbani ikiwa yuwacheleya akitembea atakuumiza. Mganga ahakikishe kuwa ulikua wageuka ndio sababu akaumwa lakini uko salama usalimini ukitarajiwa siku yoyote ile.

Yote haya wafanyiwa wewe, uwe mke au mume, haja yake utoke na siha nzuri, mzima kama kigogo ndivyo furaha ya mvuvi. Kwa miezi tisa au zaidi, ogopa ndio ngao yake huku akitia maanani kwa mwoga huenda kicheko na shujaa huenda kilio. Mgeni aje, mwenyeji apone, ama kwa hakika, dalili ya mvua ni mawingu na siku njema hutambulika tangu alfajiri ya jogoo la kwanza. Raha ikizidi siraha bali ni karaha, maumivu huanza kama mzaha.Chambilecho wahenga mzaha mzaha hutumbua usaha. Mama huhisi kama mgongo unamuuma huku akipitisha fikira kuwa unageuka ndani ya kifuko kilicho jaa maji ndi. Mungu si athumani, vile vilivyo sitirika Ajue ni Yeye Rabi Mutsa na lau tutayapitisha katika nyoyoni mwetu, hakuna hata moja litatueleya abadan. Maumivu yazidi kukithiri nukta baada ya nyingine. Kijasho chembamba mama cha mtiririka njia mbili ukidhani ni kisima cha ginigi. Hana hanani, akiulizwa haungami. Imekuwa dhahiri shahiri ya kwamba siku iliyokuwa ikingojewa kwa hamu na ghamu, yabisha mlango. Mzazi mjaa mzito yuwalia kwa uchungu. Kila mtu wa karibu, awe baba na wengine huingiwa na taharuki isiyo mithilika.Mama yuwajifunga kibwebwe na kujikaza kisabuni japo povu linamtoka akijizuilia usikaribishwe njiani. Hospitalini amefikishwa huku mganga ampokea kwa mikono miwili na kwa utaratibu wote wakikuhofia wewe usije ukadhurika. Wakati uliokua ukisubiriwa ndio umefika. Jamaa na majirani wanahamu wakisubiri mganga atoke ili awape habari nzuri. Mama yuko na mganga na wengineo wakimsaidia kukuleta ulimwenguni. Mama moyo wamuenda mbio maradufu mfano wa saa ukutani huku pumzi zikimuishia akijaribu kukusaidia utoke. Kelele anazopiga utadhani ni mwehu kwa uchungu anaohisi mwilini. Damu zamtiririka tiriri mithili ya maji yanayo fuata mkondo chini ya mlima, lakini mama hajali, potelea pote kufa gari kufa dereva, liwalo na liwa, yeye haja yake ni wewe na mimi tutoke buheri wa afya. Alafu kuzaa si kazi kulea ndio kazi.

Nijambo la kusikitisha leo hii, umekuwa barobaro wamtukana na kumdharau kama kitambara cha kufutia maji machafu. Ama kwa hakika hatujui tutokako na twendako pia halikadhalika. Sasa ulimwenguni umekaribishwa na vigelegele, vifijo na nderemo. Sherehe za kukata na shoka zikafanywa mgeni mashuhuri amewasili. Kila mtu katika jamii wana fawaisha mpwito pwito belele kufurika mithili ya kibogoyo aliyeota meno yaumu ya shamramra za dhifa ya kula nyama. Hawaukosea walobugia chumvi, ukitaka kumjua pweza alipo muulize mvuvi na uchungu wa mwana muulize mzazi. Litilie maanani leo hii, toka tangu za mababu zetu, watoto kwa hakika walikuwa wakizaliwa na sijambo geni lakini ushawahi kaa kitako ukatafakari tabu waliyopitia wazazi wako? Ni nadra sana kumpata kiumbe ametoa shukrani kwa wazazi wake wawili. Usinielewe vibaya katika kipande hiki, huwezi katu, abadan, nime kataa na walikataa kata kata, mzazi huwezi kumlipa hata chembe. Ijapokuwa ni umgeni mashuhuri huwezi kuwa sawa na viumbe walo kutangulia. Umnyonge, mdhaifu, hauna nguvu, kila kitu wafanyiwa; kulishwa, kuogeshwa, kuenda haja ndogo au kubwa pia huwa tatizo kubwa. Ni mfano wa kizee kikongwe asiye na mbele wala nyuma abebeshwe ulimwengu mzima mabegani. Hujijui hujitambui, huna hunani, ukiulizwa huungami, lakini kuna mtu mmoja shujaa. Nguvu zake hazina tofauti na jitu la miraba mine. Akufanyia yote unayohitaji,akulinde na majanga yote yanayoweza kukupata.Na kwa uhakika, ni heri limpate yeye baya kabla halijakufikia wewe. Huba lake lote ni lako, baba kwa wakati huu kigawanyo chake cha mapenzi amepokonywa ukapewa wewe mpendwa wa dhati. Hakuna mwengine ila ni mama.

Nikigusia kipande katika vipande vya maisha yangu, nilipopata fahamu kuwaona na kuwatambua wazazi wangu ni wakati nilipokua shule ya mwanzoni. Alinipenda mithili ya kito. Asubuhi kabla ya kutoka kwenda shule, atahakikisa niko na kila kitu nilichohitaji shuleni na nifikapo mlangoni mwa nyumba yetu hunibusu kwenye bapa la uso langu huu akiniambia, “Mungu atakulinda mpaka urejee salama jioni.” Pindi ninapokumbuka maneno haya ni machozi hunitirika tiriri njia mbili kama ngamia najiuliza nilini Mungu atanipa nafasi niwaangalie na kuwafurahisha wazazi wangu?

Namshukuru Mola muumba hadi wa leo maana hapa nilipofikea ni Yeye aliyewakubalia dua za wazazi wangu na sikuwa nina akili mzuri na ujanja, la, ni sababu yao ndio mola amenifikisha nilipo. Nilipokuwa shule ya msingi, mambo yalienda mrama kidogo na aliniambia maneno yake bado yangali akilini ni kama ananiambia sasa hivi huku nikinukuu maneno haya. Nilitia pamba masikio, sikusikia la muadhini wala la mteka maji msikitini nikajifanya hodari wa maisha. Namsadikisha aliyesema jungu kuu halikosi ukoko. Mtihani wa mwisho wa darasa la nane ulinivamia na ukapita, lakini haukupita na mimi, bali uliniacha nyuma. Wenzangu walinitangulia nikashindwa la kusema, kweli majuto ni mjukuu huja baada ya kitendo na yakimwaika hayazoleki. Ikiwa Mola huwasamehe waja wake waliomkosea sembuse binadamu kwa binadamu mwenzake? Mama siku zote humsamehe mwanawe na ndio siku nilirejea nyuma na kuomba msamaha na kuahidi sitorudia makosa niliofaya. Nilirudia darasa la saba na kuweka ahadi kwa nguvu zake Mola nitafaulu pindi nifanyapo mtihani wangu wa mwisho wa darasa la nane. Maisha yetu yalikuwa ya wastani na nilimsaidia mamangu katika kila biashara aliyofanya ili tupate kujiendeleza kihali na mali. Nilihakikisha kuwa tabasamu lake ndio kioo changu na ndivyo mambo yalivyo endelea hadi mtihani ulipokaribia wa darasa la nane. Shukrani ningali natoa na nazidi kutoa kwa Mola muurmba kwa kuwapa nguvu wazazi wangu kuwa na mimi wakati wote. Mtihani niliupita na ndivyo alikuwa akiniambia,”mwanangu usihofie lolote, ushapita tangu uanze kufanya mtihani mwenyewe.” Nilijawa na furaha bashasha zilizokithiri kiwango. Majibu yalipotoka, nimefaulu na kupata nafasiya shule ya upili.

Kila ninapomuhitaji huwa yuko nami, si wakati wa furaha pia wakati wa shida. Nilimaliza shule ya upili na kubahatikiwa nafasi katika chuo kikuu cha Jomo Kenyatta. Haya yote yamefananyika si kwamba nina akili kushinda wengine, la, ni kwa ajili ya kuwafurahisha wazazi wawili. Ajabu ya wengine, mtu humtukana mamake au babake wa jambo lisilo la maana na hata pia likiwa la maana haifai katika dini yoyote mtu kumkemea mzazi ijapokuwa wenye makosa ni wao. Maisha ya mwanadamu hutegemea na kuwatendea wema wazazi wawili ndipo mtu hupata usahali wakila jambo pindi wazazi wake wameridhika naye. Kaa uyapime maneno haya, maana kuteleza si kuanguka. Kukosea ni umbo tuliloumbiwa na Rabbi Musta. Ikiwa uhusiano wako na wazazi wako ni mzuri, usikinai, zidi kuukithirisha na ikiwa si mzuri nakusihi mwendani urejee nyuma. Nikiwakumbusha tena twendako hatukujui. Fanya hima na usichelewe utapata mwana si wako.Kweli hakuna kama mama.

images [1] [2] [3]