Uzushi wa kidini (Kiing. heresy) ni mafundisho ambayo ni tofauti na yale yanayokubaliwa katika jumuiya fulani ya kidini kuwa imani sahihi.

Katika dini mbalimbali kama vile Ukristo, Uislamu na Uyahudi dhana ya uzushi hutumiwa kutofautisha yale yanayotazamiwa kuwa imani halali au imani potovu. Katika nchi ambako dini fulani inaunganishwa na mamlaka ya serikali, watu wanaotazamiwa kuwa wazushi wanaweza kuteswa.

Mateso ya aina hiyo yalitokea mara nyingi katika historia ya Ukristo na pia katika historia ya Uislamu. Kwa hiyo mateso kutokana na mashataka ya uzushi ni aina ya pekee ya mateso ya kidini.

Uyahudi

hariri

Ndani ya Uyahudi, makundi yalikuwepo kandokando miaka 2000 iliyopita kabla ya kubomolewa kwa hekalu ya pili; Mafarisayo walifundisha ufufuo wa wafu lakini Masadukayo waliukataa[1]; hata hivyo hawakutumia dhana ya uzushi wakati ule.

Wakristo wote wa kwanza walikuwa Wayahudi waliotazamiwa kumfuata Masiya asiye kweli; Masadukayo waliwatesa [2] lakini Mafarisayao waliwavumilia mwanzoni [3]

Mafundisho kuhusu uzushi yalianza katika enzi ya marabi walioendelea kuongoza Wayahudi baadaye. Katika vitabu vya Talmudi kuna fafanuzi zifuatazo kuhusu wazushi[4]:

Pamoja na hayo, imani zifuatazo zinatajwa kama uzushi: wanaokataa kuwepo kwa Mungu, wanaosema Mungu hakuumba ulimwengu peke yake, wanaosema nyota fulani zinasaidia mawasiliano na Mungu, wanaokataa unabii wa Musa, wanaodai eti Mungu haangalii matendo ya watu, wanaodai Torati haitoki na Mungu moja kwa moja, wanaopinga mapokeo ya jumuiya kuhusu Torati.

Ukristo

hariri

Katika makanisa mengi mafundisho yaliyokataliwa na mitaguso ya kiekumene iliyokutana katika karne za kwanza baada ya Kristo hutazamiwa kama uzushi.

Nyaraka katika Agano Jipya zinaonyesha tayari maonyo dhidi "manabii wa uongo na waalimu wa uongo"[5] au "wazushi" (Titus 3:10 αἱρετικὸν ἄνθρωπον airetikon anthropon), ila maneno hayo yalitaja mafundisho ya kinyume ya msimamo wa mwandishi.

Karne za kwanza

hariri

Baadaye yalitokea mikondo mbalimbali ndani ya kanisa changa iliyokataliwa katika mchakato wa miaka mingi na idadi kubwa ya maaskofu, wataalamu na sharika za kikristo. Mafundisho hayo yaliyokataliwa yalihusu hasa jinsi ya kuelewa uungu wa Yesu na utatu wa Mungu.

Mafundisho yaliyopatikana kati ya Wakristo wa karne za kwanza na kukataliwa yalikuwa pamoja na:

  • Unostiki (gnosticism) uliofundisha funuo maalumu kutoka Mungu aliyekuwa tofauti na muumbaji wa dunia inayoonekana
  • Markion, aliyeathiriwa na unostiki akifundisha kwamba Mungu wa Yesu alikuwa tofauti na mungu wa Agano la Kale
  • Umontano uliofundisha ufunuo wa pekee uliopokelewa na Montano kuwa mwisho wa Dunia uko karibu na Wakristo walitakiwa kuupokea kwa kufunga, kuondoka katika ndoa na matendo ya kuzaa na kuwa tayari kufa kama mashahidi wa imani
  • Paulo wa Samosata aliyefundisha Yesu ni tofauti na Mungu maana binadamu Yesu aliasiliwa na Mungu wakati wa ubatizo wake.

Baada ya Mtaguso wa Nikea

hariri

Baada ya mwisho wa mateso ya Wakristo chini ya serikali ya kipagani ya Roma, maaskofu kutoka sehemu zote za Dola la Roma walikutana mara ya kwanza mwaka 325 wakishauriana kuhusu imani na hasa mafundisho ya Uario.

Marejeo

hariri
  1. linganisha Marko 12:18
  2. linganisha Mdo. 26:12: Saulo - Paulo alitafuta Wakristo akitumia mamlaka ya makuhani wa Yerusalemu waliokubaliwa kama wahusika juu ya jumuiya za Kiyahudi ndani ya Dola la Roma, pamoja na malaka ya kuadhibu
  3. linganisha Mdo 5:17-35; Masadukayo pamoja na Kuhani Mkuu walitaka kuchukua hatua kali dhidi ya mitume lakini Gamalieli kama msemaji wa Mafarisayo alishauri kuwavumilia akikumbusha mifano mingine ya harakati za kimasiha kati ya Wayahudi
  4. Mishneh Torah, Hilchot Teshuvah 3:6-8
  5. 2 Petro 2:1