Uario
Uario (au Uariani) ni msimamo wa teolojia ambao unamuita Yesu "Mwana wa Mungu" lakini kwa kukanusha imani ya Wakristo karibu wote kuhusu Utatu mtakatifu, yaani uwemo wa nafsi tatu za milele katika Mungu pekee: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.
Hivyo unafafanua kwamba Yesu Kristo si sawa na Mungu Baba wala si wa milele, bali ni kiumbe tu, ingawa bora kuliko wote.[1]
Jina linatokana na lile la Ario (250 hivi – 336), padri wa Aleksandria, Misri. Ingawa yeye hakuwa wa kwanza kufafanua hivyo maneno ya Yoh 14:28, mafundisho yake yalivuruga kabisa Kanisa kwa muda mrefu na kuhitaji mitaguso mikuu miwili ili kuyakomesha katika Dola la Roma.[2][3]
Kwa ajili hiyo, katika mitaguso hiyo ya kiekumeni ya kwanza (Mtaguso wa kwanza wa Nisea na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli) ilitungwa ikapanuliwa kanuni ya imani ya Nisea-Konstantinopoli iliyotakiwa kufuatwa na maaskofu wote, hata kwa nguvu ya serikali ya Dola la Roma.
Juhudi hizo hazikuzuia Uario kuendelea nje ya dola hilo, hasa kati ya makabila ya Kijerumani ambayo muda mfupi baadaye wakavamia Dola la Roma na kudhulumu Wakatoliki, hasa Hispania na Afrika Kaskazini.
Mwanzoni mwa karne za kati, Uario uliachwa kabisa, lakini ukatokea tena na tena, hasa nchini Marekani.
Hivyo Uario unafuatwa hata leo na madhehebu kadhaa ya Ukristo, ambayo kwa sababu hiyo yanatazamwa na wengine wote kama si Wakristo ama walau ni Wakristo wa pembeni (kwa Kiingereza "Marginal Christians"). Mfano wake ni Mashahidi wa Yehova, Wamormoni, lakini pia baadhi ya Wapentekoste.
Tanbihi
hariri- ↑ Williams, Rowan (2002). Arius: heresy and tradition. Wm. B. Eerdmans Publishing Co. uk. 98. ISBN 978-0-8028-4969-4.
- ↑ Socrates of Constantinople, Church History, book 1, chapter 33. Anthony F. Beavers, Chronology of the Arian Controversy.
- ↑ "First Council of Constantinople, Canon 1". ccel.org.
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Uario kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |