Qur'ani na Wanafikra Ulimwenguni

Na Salum Bendera Kitabu kitakatifu cha Qur’ani ni muujiza mkubwa wa Mwenyezi Mungu na hati ya milele ya Uislamu. Kitabu hiki cha Mwenyezi Mungu licha ya kuweko hujuma na njama mbalimbali za kukipotosha lakini kimesalimika na njama zote hizo na licha ya kupita miaka na miaka lakini hadi leo kingali kinakwenda na wakati na kinawaongoza wanadamu katika njia nyoofu na kila mwenye kukifuata na kutekeleza kikamalifu mafundisho yake ataondoka katika kiza totoro la upotovu na kupata nuru ing'arayo ya uongofu. Sifa kuu na bora ya Qur’ani Tukufu ni kudhamini hidaya, uongofu na kumuongoza mwanadamu.. Kila mwenye kuifuata Qur’ani na mafundisho yake ataongoka na kuepukana na upotovu. Mwenyezi Mungu anasema katika katika Qur'ani kwamba:

‘’Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapokuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu huingia kati ya mtu na moyo wake, na kwamba hakika kwake Yeye tu mtakusanywa.’’ (Anfaal 8:24)

Endapo mtu atairejea na kuitalii historia iliyojaa fakhari ya Uislamu, atapata athari nyingi zisizo na mithili na zenye mshangao za Qur’ani katika kuiongoza jamii ya mwanadamu. Wanahitoria wamefikia natija hii kwamba, kabla ya kuja Uislamu, ulimwengu ulikuwa umezorota kielimu na kimaadili na watu walikuwa katika giza. Utumiaji mabavu, udikteta na dhulma ni baadhi tu ya mambo yaliyokuwa yametawala na kuenea katika mataifa mengi hasa baina ya Waarabu katika zama za ujahilia. Uporaji na unyang’anyi ulikuwa umeenea mno huku watu wakiwa wameshikamana na mila potofu na kufuata pamoja na kuabudu vitu ambavyo havikuwa na faida wala madhara kwao. Mwanamke alikuwa hathaminiwi hasa katika zama za ujahilia baina ya Waarabu. Wakati nuru ya Uislamu ilipoangaza, na Qur’ani ikaja katika medani na watu wakawa chini ya mafundisho aali na adhimu ya kitabu hicho kitakatifu na chenye kuleta uhai cha Mwenyezi Mungu, kulitokea mabadiliko makubwa katika jamii ya mwanadamu. Kwa muktadha huo, Qur’ani ikawa imeleta maisha mapya na kuwatoa wanadamu katika ujahili wa kupindukia na kuwaleta katika maisha ya saada, izzah na utukufu. Ni hapo ndipo thamani ya mwanadamu ilipotambuliwa vyema na kuthaminiwa na hivyo kupelekea kuheshimiwa misingi ya akhlaqi na maadili na vile vile wanadamu kujishughulisha na kutafuta elimu yenye manufaa. Licha ya kuwa leo hii wale wenye mitazamo finyu wanajaribu kupuuza nafasi muhimu ya Qur’ani Tukufu katika kuyabadilisha maisha ya mwanadamu, lakini dhamiri zenye mwamko, insafu na uadilifu ulimwenguni zimekiri kuhusiana na nafasi hiyo adhimu ya Qur’ani. Kwa hakika Qur’ani ni kitabu ambacho kimebainisha na kuleta mambo ambayo ni mahitaji ya lazima ya mwanadamu. Mwanadamu peke yake hawezi kujiwekea sheria kuhusiana na mambo yote yanayohusu maisha yake, sheria ambazo daima ziwe hai na zisizo na mapungufu ndani yake na wala si zenye kubadilikabadika. Mara nyingi tumeshuhudia mtu akialifu kitabu na kubainisha mitazamo na nadharia zake kuhusiana na jambo au elimu fulani, lakini haupiti muda mrefu, nadharia za mualifu na mtunzi wa kitabu hicho hupitwa na wakati, au hata mualifu mwenyewe kukiri kwamba, alikosea kutoa nadharia yake hiyo kuhusiana na jambo fulani. Amma kuhusiana na kitabu cha Qur’ani mambo ni kinyume kabisa. Licha ya kupita karne nyingi tangu kuteremshwa kwake na maendeleo makubwa yaliyopatikana katika uwanja wa elimu, si tu kwamba, Qur’ani haijapitwa na wakati na kuonekana kuwa ni kitabu cha kale, bali kimeonekana kuwa kinakwenda na wakati na hata katika baadhi ya mambo ambayo yanagunduliwa leo, ukirejea Qur’ani unapata kuwa jambo hili lilikwishazungumziwa zamani na kitabu hicho kisichojiwa na batili mbele wala nyuma yake. Kitabu kitkatifu cha Qur’ani kikiwa na mipango maalumu na ratiba yenye malengo maalumu kimezungumzia maudhui mbalimbali. Qur’ani imezungumzia kuhusu kumtambua Mwenyezi Mungu, viumbe, mbingu, ardhi na vilivyomo, historia ya waliotangulia, Manabii, akhlaqi (madili) haki za familia, muongozo wa kutawala na kuendesha serikali, mfumo wa kijamii, muamala, biashara na masuala ya kiuchumi na mambo mengine kadha wa kadha. Albert Einstein msomi na mwanafizikia wa Kijerumani anasema kuwa,

‘’Qurani sio kitabu cha aljebra na jiometri au hesabati, bali ni mjumuiko na mkusanyiko wa sheria ambazo humpeleka mwanadamu katika jiha na upande wa uongofu, njia ambayo, wanafalsafa wakubwa ulimwenguni wameshindwa kuianisha.’’

Mtambuzi na mtaalamu mmoja wa masuala ya Mashariki ya Kati wa Kijerumani anasema kwamba: ‘’ Qur’ani kwa mafundisho yake, ilikuwa na nafasi muhimu ya kuinua fikra za Waislamu na ikawafanya Waislamu watutangulie katika kufikiri, utafiti, kubuni mambo na uvumbuzi katika masuala mbalimbali ya kielimu.’’ Wataalmu wa masuala ya kidini kwa upande wao wanaamini kwamba, Qur’ani imepita miujiza mingine yote. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana nyoyo zenye maandalizi huathirika haraka na maneno ya kitabu hicho adhimu. Gute Zeiten malenga na mwandishi wa Kijerumani anasema, Qur'ani ina taathira ya kustaajabisha, ambapo awali ibara zake zinaoneka kuwa ni nyepesi, lakini msomaji huathiriwa na kuvutwa haraka bila ya hiari yake na kuwa na uzuri usio na mwisho. Kwa miaka mingi makasisi wetu wametufanya tuwe mbali na uhakika wa Qur’ani tukufu pamoja na adhama yake.’’ Wanafikra wa Kiislamu nao kwa upande wao kila mmoja amezungumzia kwa namna yake muujiza wa Qur’ani. Allama Muhammad Hussein Tabatabai mwanafalsafa na mfasiri mkubwa wa Qur’ani katika zama hizi anasema:

‘’Qur’ani ni muujiza mkubwa katika balagha, ufasaha na hekima. Ni hazina na dafina yenye muujiza kwa wasomi na ni sheria ya kijamii kabisa kwa ajili ya watunga sheria. Kitabu hiki ni ubainisho wa siasa mpya na ambazo hazijawahi kushuhudiwa na wanasiasa.’’
Amma Jalaluddin al-Suyut msomi na alimu wa Kiislamu  anasema kuwa, muujiza umegawanyika katika sehemu mbili.  Muujiza wa kuhisika na wenye kuoneka na sehemu ya pili ni muujiza wa kiakili. Miujiza ya kuhisika na yenye kuonekana inawahusu Mitume waliotangulia. Amma Mtume Muhammad SAW akiwa Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu, muujiza wake ni wa kiakili yaani wa hoja za kiakili na wa milele na wala hauhusiani na jambo au tukio fulani.