Ruangwa
Wilaya ya Ruangwa ni wilaya moja ya Mkoa wa Lindi. Katika sensa ya mwaka 2002, idadi ya wakazi wa wilaya hiyo ilihesabiwa kuwa 124,516 [1].
Sura ya nchi
hariri(Hadi mwaka 2005)
Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa ni miongoni mwa Halmashauri sita (6) ambazo zinaunda Mkoa wa Lindi, zingine ni Kilwa, Lindi mjini, Lindi Vijijini, Liwale na Nachingwea.
Wilaya ipo kusini magharibi mwa Mkoa wa Lindi. Wilaya ipo kusini mwa Ikweta kati ya Latitudo nyuzi 9.5 na 10.3; Longitudo nyuzi 38.5 na 39.5 Mashariki ya Grinwichi.
Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa ina ukubwa wa eneo la kilometa za mraba 2,560, sawa na hekta za mraba 256,036. Kati ya hekta hizo za mraba hekta 104,000 zinatumika kwa kilimo hekta 72,000 sawa na 35% zinatumika kwa kilimo cha mazao ya chakula na hekta 32,000 sawa na 16%kwa kilimo cha mazao ya biashara, sawa na asilimia 51 ya eneo linalofaa kwa kilimo ambalo ni hekta za mraba 204,826 sawa na 80% Hekta 40,612 sawa na 16% ni eneo la misitu ya asili na ya kupandwa. Hekta 10,562 sawa na 4% ni eneo linalofaa kwa matumizi ya makazi ya watu na matumizi mengine.
Hali ya hewa
haririHali ya hewa iko sawa au haitofautiani sana kwa maeneo yote. Hali ya joto ni kati ya nyuzi joto 24 sentigredi wakati wa baridi na 34 sentigredi wakati wa msimu wa joto, kukiwa na wastani wa nyuzi joto 28 sentigredi kwa mwaka.
Wilaya hupata pepo za msimu (Kaskazini Mashariki) kutoka mwezi Juni hadi Oktoba na pepo za kusini Mashiriki kutoka mwezi Novemba hadi Mei kila mwaka. Mvua hunyesha kutoka katikati ya Novemba hadi Mei kila mwaka, maeneo karibu yote hupata mvua kati ya mm 800 hadi mm 1,200 kwa mwaka. Safu za milima ya Rondo hupata mvua nyingi zaidi ya mm 1,000 kwa mwaka na kwa ujumla mvua hupungua kutoka mashariki kuelekea magharibi mwa wilaya.
Wakazi
haririKulingana na Sensa ya mwaka 2002, Halmashauri ina wakazi wapatao 124,516, kati ya hao wanawake ni 64,523 sawa na 52% na wanaume 59,993 sawa na 48%. Wakazi wengi wa Wilaya wanaishi Vijijini.
Uchumi
haririPato la wananchi wa wilaya ya Ruangwa kwa mwaka 2001 lilikuwa shilingi 45,000/=, mwaka 2002 shililingi 65,000/=, mwaka 2003 shilingi 165,000/= na mwaka 2004 shilingi 185,000/= kwa mkazi kwa mwaka. Pato la wananchi kimkoa lilikuwa shilingi 212,472/= mwaka 2004 na pato la Kitaifa lilikuwa Sh.286,472.
Wilaya imejiwekea lengo la kuinua kipato cha wananchi wake angalau kifikie kile cha Kitaifa cha mwaka 2004 ifikapo mwaka 2011 kama ilivyo katika kauli mbiu ya Wilaya.
Aidha pato la wilaya linachangiwa zaidi na sekta ya Kilimo kwa 85%.
Kilimo na mifugo
haririWilaya ya Ruangwa ina jumla ya hekta 204,826 (80%) zinazofaa kwa Kilimo wakazi wa Wilaya hii hawafugi kwa wingi. Kilimo ndiyo Sekta pekee inayotoa ajira kwa zaidi ya asilimia 90 ya Wakazi wenye uwezo wa kufanya kazi.
Mazao makuu ya chakula yanayozalishwa ni mahindi; mtama, mhogo na Jamii ya kunde. Eneo linalolimwa mazao hayo ni Hekta 72,000 (35%) na mazao yanayozalishwa ni tani 42,127 kwa mwaka.
Mazao makuu ya biashara ni korosho na Ufuta. Hekta zinazolimwa ni hekta 20,951 (10%) ipo mikorosho 2,738,340 ambayo hutoa na kuzalisha wastani wa tani 5,305 kwa msimu mzuri wa mavuno. Zao la korosho hufuatiwa na zao la ufuta. Wakulima huvuna ufuta wastani wa tani 2,000 kwa mwaka. Uzalishaji wa mazao ya mifugo ni mdogo kwa vile wakazi wengi wa Ruangwa hawajishughulishi sana na Sekta hiyo. Ili kuondokana na utegemezi wa zao moja au mawili ya biashara, Wilaya inategemea kuzalisha Kilimo cha mazao mengine ya biashara kama vile mlonge, Alizeti na Nyonyo. CHANZO: Mifugo Wilaya 2006
Angalisho: Uzalishaji umepanda/kuongezeka kutokana na kupanuliwa kwa mradi wa HPT kopa Ng’ombe lipa ng’ombe unaoendelea kwa Vijiji vingine ili kukuza uchumi na Lishe Kiwilaya. Pia kuna msisitizo ili:- • Wahisani waendelee kufadhili mradi • Wafugaji binafsi wawe na hamasa ya kufuga ng’ombe wa maziwa
Takwimu za kuku wa kienyeji 2002 – 2005: a) 2001 Kuku - 72,500 b) 2002 Kuku - 105,000 c) 2003 Kuku - 152,431 d) 2004 Kuku - 159,732
Kiasi cha kuku kinapanda kila mwaka Wilaya inatarajia kuchanja kuku kudhibiti kideri kwa kipindi cha miaka 3. Ni matumaini ikifanyika kama ilivyopangwa kuku wa kienyeji wataongezeka.
Maliasili
haririWilaya ina msitu mmoja wa hifadhi wa Serikali Kuu wenye ukubwa wa hekta 4.8 uliopakana na hifadhi ya milima ya Rondo. Pamoja na Wilaya kuwa na eneo kubwa la msitu, Wilaya bado inatilia mkazo upandaji wa miti. Miti 4,071,150 imepandwa kati ya mwaka 1998 na 2005, ikiwemo miti ya vivuli, matunda na mikorosho.
Kuanzishwa kwa mpango shirikishi wa kuhifadhi misitu kwa kuihusisha Jamii (Participatory Forest Management PFM) mwaka 2006 kutaiwezesha Wilaya kuwa na maeneo mengi yaliyohifadhiwa. Mpango huo utahusisha safu ya milima ya Rondo katika Vijiji vine vya Ng’au, Nandenje, Nkowe na Lichwachwa.
Ardhi na madini
haririRuangwa ni mji mpya wa Wilaya (Makao Makuu). Hivyo zipo shuhguli za uandaaji wa Makazi na upimaji wa Viwanja. Lengo ni kila mwaka kupima viwanja 1,000. Hadi kufikia Desemba 2005, jumla ya viwanja 558 tayari vimepimwa na kugawiwa kwa waendelezaji.
Pamoja na lengo la kupima viwanja 1,000 kila mwaka, Idara imekuwa haifikii malengo yake kwa sababu haina vifaa vya kisasa vya Upimaji kama vile, “Total Station”. Kifaa hiki huazimwa kutoka Wilaya jirani ya Masasi Mkoani Mtwara. Ufumbuzi ambao inabidi Wilaya iufanye ni kununua chombo hicho kutoka katika Taasisi zinazouza vyombo vya upimaji na Ramani.
Uchimbaji wa madini upo katika Wilaya ya Ruangwa kwenye maeneo ya Namungo (Mbekenyera) Mandawa, Kitandi na Nambilanje. Madini ya vito vya thamani na dhahabu ndiyo madini yanayochimbwa. Takwimu sahihi za uzalishaji wa madini hayo bado hazijapatikana kwani Wachimbaji wamekuwa hawatoi ushirikiano wa kutosha kwa Serikali za Vijiji katika maeneo husika pamoja na ofisi za Wilaya kwa kudai kuwa wako katika hatua za Utafiti wa madini hayo.
Aina ya madini ya vito vya thamani ni Green tomalin/garnet, Red Garnet, Blue Sapphire, Rhodolites, Emarolds, Pigment materials (External Rendering Rangi ya puchi) Acquamarine na alexandarite.
Barabara
haririWilaya ina jumla ya kilometa 475 za barabara. Kilometa 113 ni za Mkoa kilometa 223 ni za Wilaya na kilometa 139 ni za Vijiji. Kilometa 296 (za Mkoa 113 Wilaya 183) huwa zinapitika kwa shida wakati wa masika na kilometa 179 zinapitika kiangazi. Ili kukidhi mahitaji ya mtandao wa barabara kwa Wilaya inahitajika kilometa 139 (Vijiji) zikarabatiwe, madaraja 4 yajengwe, madrifti 2 yajengwe na Makalvati 22 yajengwe. Fedha za mfuko wa barabara zinazofika Wilayani zina maelekezo ya kufanya matengenezo kwa barabara za Wilaya zilizopo na siyo kuchonga barabara mpya. Hivyo basi, Wilaya inabidi itafute ufadhili kwa Wadau wengine pamoja na kutumia sehemu ya mapato yake katika kukamilisha mtandao wa barabara Wilayani ili kukidhi mahitaji ya jamii.
Huduma za kijamii
haririShule za msingi
haririWilaya ya Ruangwa ina jumla ya Shule 69 na idadi ya wanafunzi 22,793; kati yao wasichana 11,316 na wavulana 11,477. Idadi ya Walimu katia Shule hizo ni 430 wakiwepo walimu wa kike daraja la IIIB/C 52 na IIIA 60 jumla yao 112 na Walimu wa kiume daraja la IIIB/C 162, IIIA 149 na Diploma 7 jumla yao 318. Walimu daraja IIIB/C wa kike na wa kiume ni 214 na daraja la IIIA wa kike na wa kiume ni 299.
Walimu 7 wa Diploma ni wa kiume tu, hakuna wa kike. Kiwango cha Taaluma kwa Wilaya ya Ruangwa bado kiko chini sana kutokana na ukweli kwamba Walimu walio wengi karibu 50% ya walimu wa Shule za Msingi ni wa daraja IIIB/C. Sababu kubwa iliyopelekea hali hii ni kuwa mwaka 1995 wakati Wilaya imeundwa, walimu wote wa daraja la IIIA karibu 75% walibaki katika Wilaya Mama ya Lindi. Kutokana na hali hii Wilaya imefanya juhudi kubwa katika kuwasomesha Walimu wa daraja la IIIB/C kupitia mpango wa masomo ya mbali ili kuinua kiwango cha Taaluma yao pamoja na kutumia Chuo cha Ualimu Nachingwea kuwafundisha nyakati za likizo walimu walio katika mpango huo.
Pamoja na zoezi hilo; Wilaya inapopata vibali vya ajira mpya imeweza kuwaajiri Walimu wa daraja la IIIA. Pia mpango wa kuwaajiri walimu wanafunzi waliotoka Vyuoni, umeongeza kiwango cha kupitikana kwa walimu daraja la IIIA.
Madarasa ya awali
haririIdadi ya madarasa ya awali ni 68, idadi ya wanafunzi ni 3,458 wakiwemo wavulana 1,631 na wasichana 1,827, Walimu wanaofundisha madarasa hayo ni wa Shule za msingi ambao idadi yao ni 68 wakiwemo wa kike 44 na wa kiume 24. Walimu wote wa madarasa ya awali ni wa daraja la IIIB/C. Walimu wanaotakiwa ni wa daraja la IIIA. Walimu waliopo wanajiendeleza chini ya mpango wa mafunzo kwa wanafunzi walio mbali (Distance learning programme) pamoja na kuhudhuria mafunzo nyakati za likizo katika Chuo cha Ualimu cha Nachingwea.
Shule za sekondari
haririWilaya ya Ruangwa ina Shule 2 za Sekondari ambazo ni Mbekenyera na Nkowe. Shule zote ni za Serikali Shule hizi zinachukua wanafunzi wa Kidato cha I hadi IV. Lakini zina upungufu mkubwa wa walimu. Shule nyingine za Sekondari za Kata 13 zinaendelea kujengwa pamoja na Sekondari 1 ya Kijiji cha Liuguru Katika kata ya Narungombe. Ili kutatua tatizo sugu la upungufu wa Walimu Wilaya inafanya kila juhudi kujenga mazingira ya kuvutia pamoja na kutoa motisha kwa Walimu watakaokuja kufundisha katika Shule za Ruangwa.
Vyuo vya ufundi
haririWilaya ina Chuo 1 cha ufundi stadi kinachoitwa “Nkowe Chuo cha Ufundi”, katika Chuo hicho kuna fani nne (4) za Ufundi; fani ya ufundi seremala, uashi, Sayansikimu na bati/chuma. Vile vile Chuo kinakabiliwa na upungufu mkubwa wa wakufunzi. Kwa vile Chuo hiki kimesajiliwa na VETA-MTWARA (VETA MAKAO MAKUU KANDA YA KUSINI), Ufumbuzi wa tatizo la upungufu wa walimu na zana za kufanyia kazi utapatikana muda si mrefu.
Afya
haririWilaya ina jumla ya Zahanati 16, kati ya hizo Zahanati 13 ni za Serikali na 2 ni za Mashirika ya Dini na 1 ni ya Mtu binafsi (MUZDALFA). Ujenzi unaendelea kwenye Zahanati 6 ambazo ni Makanjiro, Mtimbo, Mtakuja, Likwachu, Liuguru, na Mtondo. Ili kukidhi mahitaji ya Zahanati, inatakiwa zijengwe Zahanati 4 zaidi. Zahanati hizo zinatakiwa kuongezwa katika Vijiji vya Chibula, Chinongwe, Luchelegwa na Nandanga. Hospitali ya Wilaya ina jengo 1 la Upasuaji na chumba cha mionzi (X-ray) lakini hakuna mashine ya mionzi na vifaa vya upasuaji. Huduma za Afya hutolewa na Waganga 35, wauguzi 35, wakunga wa jadi 108, Waganga wa jadi 47, Wahudumu wa Afya Vijijini 48 na MCHAs 8 (Wakunga wasaidizi).
Wakazi wa Wilaya hii husumbuliwa na magonjwa 10 ambayo ni Malaria, Kichomi, Magonjwa ya Koo na mapafu, upungufu wa damu, magonjwa ya kuhara, magonjwa ya akina Mama, Ajali, kichocho na UKIMWI.
Sekta hii ya Afya ina mapungufu yafuatayo katika utoaji wa huduma. Katika Hospitali ya Wilaya kuna upungufu wa majengo ambayo ni ;wodi 4 zikiwemo wodi ya uzazi, wodi ya watoto, wodi 2 za upasuaji[ 1 ya wanawake na 1 ya wanaume]. Wodi 1 ya Uzazi inaendelea kujengwa.
Pia kuna upungufu wa Watumishi wa kada mbalimbali ikiwemo Hospitali ya Wilaya Watumishi 150; Vituo vya Afya Watumishi 58 na Zahanati watumishi 348.
Kwa ujumla utoaji wa huduma za Afya ni 85% Wilaya ikifanikiwa kupata baadhi ya vifaa vya upasuaji vinavyokosekana pamoja mashine ya mionzi (X-ray machine) inakusudia kuongeza kiwango cha utoaji wa huduma za Afya kwa 95% ifikapo mwaka 2008.
Maji
haririWilaya ya Ruangwa ina jumla ya miradi ya maji 11 katika Vijiji 25 kati ya miradi hiyo 6 inafanya kazi kwa kutoa huduma katika Vijiji 15. Wilaya pia ina Visima vifupi 257. Kati yake 71 vimekauka 79 vinahitaji Pampu mpya na 107 vinatoa huduma. Idadi ya watu wanaopata huduma ya Maji safi na salama ni 50,803 sawa na 40.8% ya wakazi wote. Hali hii inatokana na Ukame uliokithiri hadi kupelekea visima 21 kukauka.
Ili kutoa huduma ya maji inayokidhi mahitaji ya Jamii, Wilaya inatakiwa kuchimba visima vifupi vyenye pampu 141 ili kuhudumia watu 35,250; Visima virefu vyenye pampu 65 ili kuhudumia watu 16,250; kujenga mitandao mipya 8 ya mabomba (New piped schemes na kukarabati mitandao 6 iliyopo (Existing schemes) ili kuhudumia watu 22,361. Inatarajiwa kuwa jumla ya watu 73,861 sawa na 59% watahudumiwa.
Ushirika na asasi nyingine
haririKuna michepuo ya aina mbili ya Vyama vya ushirika vya msingi ndani ya Wilaya kama ifuatavyo:-
(i) Vyama vya Ushirika vya Msingi vya mazao -vipo 13
(ii) Vyama vya ushirika vya kuweka na kukopa-vipo 3 (Ongezeko la Chama 1 cha kuweka na kukopa cha Mbwemkuru Savings & Credit Society, licha ya viwili (2) vilivyopo yaani RUTESCO na RUWOSCO).
Vyama viwili vya kuweka na kukopa vimekwisha sajiliwa na Mrajis msaidizi. Vyama hivyo ni Chama cha kuweka na kukopa cha Wafanyakazi (RUWOSCO) – Ruangwa Workers Savings and credit Cooperative society na Chama cha kuweka na kukopa cha Walimu (RUTESCO –Ruangwa Teachers savings and credit Cooperative society). Wilaya kwa sasa hivi inatilia mkazo uanzishwaji wa SACCOS nyingi ili kupelekea uanzishwaji wa Benki ya wananchi.
Mashirika yasiyo ya serikali wilayani
haririHalmashauri inashirikiana na mashirika mawili katika shughuli za utoaji huduma kwa jamii kama ifuatavyo:
ROPA (RUANGWA ORGANISATION FOR POVERTY ALLEVIATION) Shirika hili linajishughulisha na kazi za kuhifadhi mazingira, kutoa Elimu ya kujikinga na VVU/UKIMWI na shughuli za kiuchumi (kutoa mikopo kwa vikundi vya akina Mama vya uzalishaji).
Viungo vya Nje
hariri- Takwimu za Wilaya ya Ruangwa Ilihifadhiwa 14 Januari 2005 kwenye Wayback Machine.
- Historia ya kuanzishwa kwa wilaya ya Ruangwa Ilihifadhiwa 6 Januari 2005 kwenye Wayback Machine.
Marejeo
hariri- ↑ "Sensa ya Tanzania ya 2002". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2010-02-10. Iliwekwa mnamo 2010-10-30.
Kata za Wilaya ya Ruangwa - Tanzania | ||
---|---|---|
Chibula | Chienjele | Chinongwe | Chunyu | Likunja | Luchelegwa | Makanjiro | Malolo | Mandarawe | Mandawa | Matambarale | Mbekenyera | Mbwemkuru | Mnacho | Nachingwea | Nambilanje | Namichiga | Nandagala | Nanganga | Narungombe | Nkowe | Ruangwa |
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Lindi bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Ruangwa kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno. |