Mkoa wa Lindi
Lindi ni jina la mji, wilaya na mkoa ulioko Kusini-Mashariki mwa Tanzania.
Mkoa wa Lindi ni kati ya mikoa 31 iliyopo nchini Tanzania yenye postikodi namba 65000.
Umepakana na mikoa ya Pwani, Mtwara, Ruvuma na Morogoro. Upande wa mashariki hupakana na Bahari Hindi.
Eneo la mkoa
haririMkoa huo umeanzishwa mwaka 1971 na una eneo la km² 67,000. Karibu robo ya eneo lake au km² 18,000 ni sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya Nyerere.
Mkoa una wilaya sita za: Lindi Mjini, Mtama (hadi 2019 Lindi Vijijini), Kilwa, Nachingwea, Liwale na Ruangwa.
Mito mikubwa ndiyo Lukuledi, Matandu na Mavuji, yote yaelekea Bahari Hindi.
Mwinuko huanza mwambaoni ukipanda hadi mita 500, hakuna milima mirefu.
Hali ya hewa
haririHali ya hewa ya Lindi ni ya joto mwaka wote ikiwa na wastani kati ya sentigredi 24,5 na 27.
Mkoa hupokea kati ya mm 980 na 1200 za mvua kwa mwaka, hasa kati ya miezi ya Novemba na Mei.
Wakazi
haririKatika sensa ya mwaka 2022 wakazi walihesabiwa 1,194,028. Wakazi kwa wilaya ni (idadi katika mabano): Kilwa (297,676), Lindi Mjini (174,126), Mtama (166,493), Liwale (136,505), Nachingwea (233,655), Ruangwa (185,573)[1].
Karibu asilimia 90 kati hao ni wakulima.
Makabila makubwa zaidi ni Wamwera, ambao wanapatikana hasa wilaya ya Nachingwea na Lindi vijijini katika kata za Rondo, halafu Wamachinga, Wamalaba ambao wako zaidi Lindi mjini, Wamatumbi na Wangindo huko Kilwa.
Miundombinu ya mawasiliano
haririKuna barabara chache katika hali nzuri. Ndizo km 155 za barabara ya lami na km 3567 za barabara ya mavumbi, mara nyingi katika hali mbaya. Wakati wa mvua mara kwa mara njia ya kwenda Daressalaam imefungwa.
Kuna matumaini ya kuboreka kwa mawasiliano na jiji la Daresalaam tangu kumalizika kwa daraja la Rufiji.
Kwa sasa barabara ya kutoka Mingoyo mpaka Dar es Salaam imekamilika kwa kiwango cha lami, kimebaki kipande cha kilometa 60 tu kuanzia Muhoro, wilaya ya Kilwa, mpaka kukaribia daraja la Mkapa juu ya mto Rufiji ambacho kinamaliziwa kwa kiwango cha lami.
Kuna kiwanja cha ndege Lindi, Nachingwea na Kilwa Masoko. Lindi na Kilwa Masoko kuna pia bandari. Huduma za simu zimepata maendeleo kiasi tangu kuanzishwa kwa simu za mkononi.
Utalii haujafikia umuhimu sana kutokana na matatizo ya mawasiliano magumu, ingawa Lindi ina sehemu mbalimbali zenye uwezo wa kuwavuta watalii: Kilwa Kisiwani ndio mji wa kihistoria wa pwani ya Afrika ya Mashariki pamoja na magofu ya miji mingine ya Waswahili, Selous ni hifadhi kubwa kabisa katika Afrika, ufuko wa mchanga ni wa kuvutia sana, nafasi za zamia majini ni tele.
Gesi iliyopatikana baharini karibu na kisiwa cha Songosongo imeleta matumaini ya maendeleo.
Kilimo na biashara
haririMkoa wa Lindi wakazi wake wengi ni wakulima, hasa maeneo ya vijijini wengi wanalima mazao mchanganyiko, yaani ya biashara na chakula. Mazao ya biashara hasa ni korosho, ambazo zinapatikana kwa wingi katika wilaya ya Ruangwa, Lindi Vijijini, na Nachingwea, pia kuna zao la ufuta na ndizi kama zao la biashara na chakula pia.
Mazao ya chakula kuna mahindi, mpunga, muhogo, nyanya, vitunguu: hizi pia hulimwa sana wakati wa masika kutegemea na mvua za vuli.
Biashara wakazi wengi wa mkoa wa Lindi wanafanya biashara, hasa biashara ndogondogo zijulikanazo kama "machinga trade": wanauza mazao wakati wa mavuno na huchukua bidhaa nyingi kutoka Dar es salaam na kupeleka vijijini hasa kwenye kata.
Elimu
haririMkoa wa Lindi huko nyuma kielimu kwani shule za sekondari mpaka sasa si nyingi sana na shule hizo hazina walimu wa kutosha kutokana na miundombinu ya barabara na shule zenye kidato cha tano na cha sita mpaka sasa ni Lindi sekondari - Lindi, Mahiwa na Namupa seminari - Lindi vijijini. Pia kuna chuo cha ualimu Nachingwea katika wilaya ya Nachingwea.
Majimbo ya bunge
haririWakati wa uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2015 mkoa huu ulikuwa na majimbo ya uchaguzi yafuatayo:
- Kilwa Kusini : mbunge ni Selemani Ally Bungara (CUF)
- Kilwa Kaskazini : mbunge ni Ngombare Edgar (CUF)
- Lindi Mjini : mbunge ni Hassan Suleiman Kaunje (CCM)
- Liwale : mbunge ni Zuberi Kuchauka (CCM)
- Mtama : mbunge ni Nape Nnauye (CCM)
- Mchinga : mbunge ni Hassan Bobali (CUF)
- Nachingwea : mbunge ni Hassan Elias Masala (CCM)
- Ruangwa : mbunge ni Kassim Majaliwa (CCM)
Tazama pia
haririTanbihi
hariri
Arusha | Dar es Salaam | Dodoma | Geita | Iringa | Kagera | Katavi | Kigoma | Kilimanjaro | Lindi | Manyara | Mara | Mbeya | Morogoro | Mtwara | Mwanza | Njombe | Pemba Kaskazini | Pemba Kusini | Pwani | Rukwa | Ruvuma | Shinyanga | Simiyu | Singida | Songwe | Tabora | Tanga | Unguja Kaskazini | Unguja Kusini | Unguja Mjini Magharibi |
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Lindi bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Mkoa wa Lindi kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno. |