Sputnik 1 (Kirusi Спутник kwa maana msindikizaji) ilikuwa satelaiti ya kwanza iliyotengenezwa na binadamu na kuzunguka Dunia katika anga-nje. Ilitengenezwa katika Umoja wa Kisovieti na kurushwa angani tarehe 4 Oktoba 1957 kutoka kituo cha Baikonur (leo nchini Kazakhstan).

Sputnik 1 ilikuwa na umbo la tufe lenye kipenyo cha sentimita 58 na masi ya kilogramu 83.6. Ilikuwa na antena mbili zenye urefu wa mita 2.4 na 2.9. Ilibeba vifaa vya kupima jotoridi ndani yake pamoja na shinikizo la gesi iliyo mwilini mwake transmita ya redio iliyorusha vipimo hivi kupitia antena.

Sputnik 1 ilizungukua Dunia mara 1,440 katika muda wa miezi 3 hadi kushuka na kuungua katika angahewa ya Dunia tarehe 4 January 1958.

Kurushwa kwa Sputnik 1 kulitokea wakati wa mashindano makali baina ya Umoja wa Kisovieti na Marekani. Marekani ilishtuka kabisa kwa sababu waliwahi kuamini ya kwamba walikuwa mbele. Mshtuko wa Sputnik ulisababisha mabadiliko katika siasa ya Marekani iliyoongeza juhudi zake katika teknolojia na elimu. [1] Hapo yalianza mashindano ya anga (en:Space Race baina ya Marekani na Umoja wa Kisovieti ambapo pande zote ziliendelea kupeleka satelaiti nyingi kwenye anga zilizofuatwa na vyomboanga vya kubeba watu hadi Marekani ilifaulu kufikisha watu mwezini mwaka 1969 kwa mradi wa Apollo 11.


References

  1. Calmes, Jackie (2010-12-06). "Obama Calls for New 'Sputnik Moment'". The New York Times. Iliwekwa mnamo 2011-12-24.