Satelaiti
Satelaiti (pia setelaiti, setilaiti, kutoka Kilatini satelles, "msindikizaji", kupitia Kiingereza satellite) ni kitu kinachofuatana na kitu kingine. Neno linatumiwa kwa maana mbili ambayo ni:
- magimba asilia katika anga-nje kama mwezi, na
- vifaa au vyombo vilivyotengenezwa na kurushwa na binadamu ili kuzunguka dunia kwa kazi mbalimbali, au kwa lugha nyingine vyombo vya angani. Satelaiti havibebi watu.
Kwa kufuata maana hii ya 2, Satelaiti au Setilaiti ni kifaa cha kuundwa na binadamu ambacho huundwa kwa kusudi la kukiweka kwenye obiti kwaajili ya shughuli maalumu kama vile utafiti wa kisayansi. Mara nyingine vifaa hivi huitwa satelaiti za kutengenezwa ili kuzitofautisha na satelaiti asilia kama vile mwezi wa Dunia.
Satelaiti asilia
haririKatika astronomia satelaiti ni gimba dogo linalozunguka gimba kubwa zaidi kwa njia ya obiti (en:orbit). Satelaiti ni hasa gimba linalozunguka sayari; kwa maana hii ni sawa na "mwezi" lakini inatumiwa pia kwa galaksi ndogo inayozunguka galaksi kubwa zaidi. Kuna pia asteroidi zenye satelaiti zao.
Kila satelaiti inashikwa na graviti ya gimba kubwa zaidi, kama ni sayari au asteroidi au galaksi.
Satelaiti kama chombo kilichotengenezwa
haririDunia inazungukwa na maelfu ya satelaiti ambazo ni vifaa au vyombo vilivyorushwa katika anga-nje kwa njia ya roketi na kuzunguka Dunia kwa obiti mbalimbali. Satelaiti hizi zinatekeleza kazi za kisayansi, za kibiashara na za kijeshi.
Satelaiti ya kwanza iliyorushwa angani ilikuwa Sputnik 1. Ilitumwa na Umoja wa Kisovyeti tarehe 4 Oktoba 1957.
Satelaiti zilizopo
haririSiku hizi kuna nchi zaidi ya 50 zilizopeleka satelaiti katika anga-nje. Idadi za nchi zenye uwezo wa kuzirusha ni ndogo zaidi.
Tangu Sputnik 1 takriban satelaiti 6,600 zimepelekwa angani. Mwaka 2013 ilikadiriwa ya kwamba 3,600 bado zilifuata obiti zake. [1] Takriban 1,000 zilifanya kazi;[2] lakini nyingine hazikufanya kazi tena, zilikuwa takataka ya angani.
Takriban satelaiti 500 ziko kwenye obiti za dunia (chini ya kilomita 2,000 juu ya uso wa Dunia), 50 ziko kwenye obiti ya wastani (mnamo 20,000 km) ambazo hasa zile za uongozaji na nyingine ziko kwenye obiti ya juu ambako zinaweza kukaa muda wote juu ya eneo lilelile la Dunia (mnamo 36,000 km).[3]
Vyomboanga vya utafiti vilipelekwa hadi obiti za kuzunguka sayari mbalimbali na sasa zimekuwa satelaiti za sayari hizo kama vile Utaridi, Zuhura, Mirihi, Mshtarii, Zohali, asteroidi kadhaa[4] na pia Jua.
Shughuli za satelaiti
haririSatelaiti hutekeleza shughuli mbalimbali:
- Utafiti wa kisayansi, kama kupima uga sumaku ya dunia na kukusanya data za kila aina
- Uangalizi wa Dunia pamoja na utabiri wa hali ya hewa, kuangalia mwendo wa tufani kubwa na kupima machafuko ya angahewa.
- Mawasiliano pamoja na kusambaza programu za runinga na mawasiliano ya simu
- Uongozaji wa usafiri pamoja na mfumo wa Global Positioning System (GPS)
- Kijeshi pamoja na upelelezi, kupiga picha za nchi mbalimbali, kupokea data za nchi nyingine na mawasiliano ya kijeshi.
Makala bado ni mbegu. Unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuongezea habari. |
- ↑ Rising, David. "Satellite hits Atlantic — but what about next one?", 11 November 2013. Archived from the original on 2013-11-12.
- ↑ "Global Experts Agree Action Needed on Space Debris". European Space Agency. 25 Aprili 2013.
{{cite web}}
: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ Cain, Fraser (24 Oktoba 2013). "How Many Satellites are in Space?". Universe Today.
{{cite web}}
: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ "NASA Spacecraft Becomes First to Orbit a Dwarf Planet". NASA.