Tazama Tanzania
“Tazama Tanzania” ni jina la wimbo maarufu ulioimbwa na kutungwa na kundi la wanandugu Varda Arts kutoka nchini Tanzania. Wimbo umetayarishwa na Varda Arts wenyewe na kutolewa mapema mwaka wa 1985. Huu ni wimbo ambao huhesabiwa kama alama kamili ya kundi la Vard Arts. Sauti zinazosikika katika wimbo ni pamoja na Aziz Varda, Iqbal Varda, Rafiq Farook, Yunus Senior na Yunus Junior.
"Tazama Tanzania" | ||
---|---|---|
Picha ya kiwambo cha Tazama | ||
Wimbo wa Varda Arts | ||
Umetolewa | 1985 | |
Umerekodiwa | 1985 | |
Lugha | Kiswahili | |
Urefu | 6:20 | |
Mtunzi | Aziz Varda | |
Mtayarishaji | Varda Arts |
Wimbo unahusu mazingira mazuri ya Tanzania na kuitambua nchi kama pepo ya duniani. Sifa ya uzuri utu na ubinadamu walionao Watanzania.
Kuhusu wimbo kwa ujumla
haririKupitia wimbo huu, Varda Arts walialikwa kushiriki katika mashindano ya “Kumi Bora” ya kwanza kutokea nchini Tanzania mnamo mwaka wa 1988. Katika mashindano hayo, Varda Arts walitengeneza historia nchini Tanzania katika nyanja ya muziki hususani bendi yenye asili ya Kiasia kushiriki katika mashindano na kupata ushindi dhidi ya mabendi mengine maarufu na yenye muda mrefu na vyombo vya kisasa Afrika.[1]
Wimbo hasa unaitaja Tanzania kama pepo ya duniani kwa kusifia neema za Mungu kwa uzuri wa asili, mandahri mazuri ya bahari, Mlima Kilimanjaro, hifadhi za taifa, maliasili na watu wake walio-wacheshi walioungana chini ya mwavuli mmoja bila kubaguana rangi, kabila wala dini. Zawadi hiyo ilitolewa na Baraza la Sanaa Tanzania’ (BASATA) katika uwanja wa taifa uliofurika watu huko jijini Dar-es-Salaam.[2][3]
BASATA ni tawi la Wizara ya Elimu na Utamaduni ikiwa kama sehemu yake kuboresha sanaa kwa kutambua juhudi zinazofanywa na wasanii nchini Tanzania. Katika makala iliyochapishwa mnamo tarehe 8 Machi, 1992 na mwandishi na mpiga picha nguli Muhidin Issa Michuzi ambaye anafahamika sana kwa kuwa mwanzilishi wa mwanzo kabisa wa mablogu Tanzania kwa kuanzisha ‘Michuzi Blog’—alitoa maelezo yake kuhusu mashindano ya ‘Onesho la Kumi Bora’ la mwaka wa 1988:
Kitu pekee kikubwa na cha kushangaza wakati wa mashindano ya Onesho la Kumi Bora ni kwamba Varda Arts ilikuwa bendi pekee iliyokuwa haina vyomvo vyake wenyewe. Lakini waliweza kukodisha vyombo na kuja kufanya kazi na hilo ni mafanikio tosha. Kujituma kote na kujijenga wenyewe kama wasanii bila kulilia misaada kutoka katika jumuia za Kiasia, serikali wala wafadhili hiyo ni fahari tosha ambayo inatakiwa iwe mfano wa kuigwa na wasanii wengine.”
—Muhidini Issa Michuzi
Michuzi aliongezea zaidi kwa kusema, kulikuwa na bendi nyengine zilizotakiwa kushiriki katika mashindano lakini walikataa kushiriki kwa kisingizio cha kwamba hawana vyombo vizuri vya kushiriki katika shindano hilo. Jambo ambalo hutakiwi kusahau ni kwamba nyakati hizo ilikuwa tabu hata kupata gitaa la uzi nchini.
Wakati wa kujiandaa ili kushiriki katika shindano hili, siku mbili kabla ya onesho, mpigaji kinanda mkubwa wa bendi ya Varda Arts, Rafiq Farook akaumwa ghaflal. Badala ya kujiondoa katika shindano, Varda Arts wakaamua kumfundisha Yunus Mkubwa namna ya kupiga kinanda licha ya kwamba hajawahipo kupiga kinanda hapo awali. Ili kufanikisha zoezi, Aziz Varda alilazimika kumpatia mazoezi ya masaa nane kwa siku ili kufidia onesho la siku mbili zijazo.
Katika kufanikisha hili, aliweza kukizoea kinanda vyema kabisa na siku ya onesho alifanya kwa kadiri alivyoweza licha ya magumu yote waliyopitia na kushinda wasanii wengine waliokuwa na uzoefu na vifaa vya kuaminika. Mwaka wa 1989, yaani, mwaka uliofuatia, wimbo wa Varda Arts ‘Watoto;’ nao ulizawadiwa tuzo, hivyo ‘Tazama Tanzania’ na ‘Watoto’ zikawa zinaendelea kupigwa katika maredio kwa zaidi ya miaka thelathini sasa ambayo kwa bendi yenye asili ya Asia hayo kwao ni mafanikio makubwa sana.
Mashairi
haririWimbo unaanza na maneno ya; "Ukiuliza habari, salama Tanzania, Funga safari ya Tanzania, Tanzania, Tanzaniaaa! Tazama Tanzania!" Wanaimba katika sauti ya huzuni sana. Halafu kwa Kiswahili chenye lafudhi ya Kihindi. Kwa wakati huo ilikuwa ajabu sana kusikia Wahindi wakiimba Kiswahili. Hayo maneno ya juu wanaimba mara mbili kwa sababu ni kiitikio chake. Kiitikio kipo katika muundo wa salamu ya kutaka kujua habari za Tanzania. Jinsi kulivyo salama na utazame Tanzania. Wakimaliza kuimba, wanaacha vinanda vitupu vya huzuni vinapiga hali ambayo ilileta ladha nzuri kwa muziki wa asili ya Asia kwa matamshi ya Kiswahili.
- Mstari wa kwanza
"Wageni karibuni kwa shangwe na ngoma.
Twaingia kwa lugha tamu ya hekima,
Kiswahili lugha yetu ya zote awamu,
Twaelewana wote bila hasama!"
Wamepokezana humu waimbaji.
Halafu wanatumia maneno ambayo watalii wengi wanayatumia kwa miaka ile ya 1980.
"Jambo, habari gani nzuri!
Salama Tanzania, Tanzania!"
- Mstari wa pili
"Bahari yetu ya Dar es Salaama!
Inakuja kwa wavuvi mapemaaa!
Najua lachomoza la tumaini,
Huzama na kuacha aamani!
Anarudia tena:
"Ukiuliza habari, salama Tanzania,
Funga safari ya Tanzania, Tanzania, Tanzaniaaa!
Tazama Tanzania!"
Video ya muziki
haririVideo yake imetawaliwa na maeneo mbalimbali ya kuvutia ya Tanzania. Ndani yake anaonesha ustaarabu wa Waswahili, maeneo ya pwani na bara. Mlima Kilimanjaro, bungeni ndani, Waswahili, Wamaasai na watu wengine wanaishi nchini Tanzania. Sehemu kubwa ya video imeonesha mazingira ya milima na mabonde, bahari na mito.[4] Video hii ilikuwa maarufu sana miaka ya 1990 kwa sababu ilikuwa ikioneshwa mno katika televisheni ya CTN ambapo Aziz Varda aliwahi kuwa mtayarishaji mkuu wa vipindi pale.
Marejeo
hariri- ↑ Varda Arts (2016-01-25), Varda Arts - Tazama Tanzania (Karibu Hotel), iliwekwa mnamo 2019-03-11
- ↑ Varda Arts (2016-02-08), Varda Arts - Tazama Tanzania (Top-Ten Competition), iliwekwa mnamo 2019-03-11
- ↑ Varda Arts (2015-10-27), Vard Arts - Tazama Tanzania (National Stadium), iliwekwa mnamo 2019-03-11
- ↑ Varda Arts (2018-12-01), Varda Arts - Tazama Tanzania, iliwekwa mnamo 2019-03-11