Lugha

utaratibu wa mawasiliano kati ya viumbe

Lugha (kutoka neno la Kiarabu: لغة) ni utaratibu wa kuwasiliana kati ya binadamu (wengine wanadai hata kati ya viumbe wenye akili).

Mawasiliano kwa lugha ya ishara ya Kimarekani

Somo la lugha linaitwa maarifa ya lugha au isimu.

Mwaka wa 2008 ulikuwa Mwaka wa Lugha wa Kimataifa.

Maana ya neno "lugha"

Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu zenye maana na zilizokubaliwa na jamii ya watu fulani ili zitumike katika kuleta mawasiliano.

Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu kwa sababu zilitokea kama bahati tu kwa binadamu. Wanyama hawatumii lugha kama chombo cha mawasiliano, kwa kuwa lugha ni sauti zenye maana na kukubaliwa na jamii.

Hakuna lugha bora zaidi duniani, kwa kuwa lugha zote zina ubora, mradi zikidhi matakwa ya jamii husika.

Mbali na maana ya kawaida kuna pia lugha ya ishara inayotumiwa na watu bubu. Katika fani ya programu za kompyuta ni kawaida kuongea juu ya " lugha ya kompyuta".

Umuhimu wa lugha

  • Lugha ni kitambulisho cha jamii
  • Lugha hutolea elimu
  • Lugha huleta mawasiliano katika jamii
  • Lugha hukuza utamaduni
  • lugha huburudisha

Tabia za lugha

Lugha huwa na tabia zifuatazo:

  • Lugha huzaliwa: ni kutokana na lugha nyingine moja au zaidi zilizotangulia kuwepo.
  • Lugha hukua: lugha hukua (kuongezeka kwa maneno, kuongezeka kwa idadi ya wazungumzaji, kuwa na mawanda mapana, kusanifiwa) kadiri inavyoendelea kutumiwa na jamii.
  • Lugha hutohoa: lugha ina tabia ya kuchukua au kukopa maneno kutoka lugha nyingine.
  • Lugha hufundishika: mtu yeyote anaweza kujifunza walau kiasi lugha yoyote hata kwa njia ya ufundishaji.
  • Lugha huathiriana: lugha yoyote inaweza kuathiriwa na lugha nyingine.
  • Lugha lazima ijitosheleze: kila lugha inajitosheleza kulingana na mahitaji ya jamii inayotumia lugha yenyewe.
  • Lugha zina ubora: lugha zote ni bora hakuna lugha bora kuliko nyingine zote.
  • Lugha hurithiwa: jamii hurithi lugha kutoka kizazi hadi kizazi.
  • Lugha hufa: inapozidi mno kubadilika mwisho si yenyewe tena, lakini pia inapoachwa isitumike tena kwa kuwa wahusika wanapendelea lugha nyingine.

Sifa za lugha

  • Lugha lazima iwe inahusu binadamu
  • Sauti-sauti hufanywa na mwanadamu
  • Lugha hufuata misingi ya fonimu, yaani, a, b, ch, d, f, h, z n.k.
  • Lugha huwa na mpangilio maalumu wenye kubeba maana. Mpangilio huo huanza na fonimu ---> Silabi ---> Neno
  • Lugha hujitambulisha ili kuzalisha maneno mengi.

Dhima za lugha

  1. Lugha hutumika kama chombo cha mawasiliano kwa kupashiana habari.
  2. Lugha hutumika kujenga umoja, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wanajamii.
  3. Lugha hutumika kutunza, kukuza, na kuendeleza utamaduni wa jamii.
  4. Lugha hutumika katika kutetea maarifa mbalimbali (ni nyenzo ya kufundishia).
  5. Lugha hutumika kama alama ya utambulisho wa kabila/jamii au taifa fulani.
  6. lugha hutumika kutoa burudani.

Aina za lugha kwa kigezo cha uwasilishaji

Kimsingi lugha ni moja. Uwasilishwaji wake ndio huigawa katika tanzu/aina kuu mbili:

  1. Lugha ya mazungumzo
  2. Lugha ya maandishi

Lugha ya mazungumzo

Hii ni lugha ambayo huwasilishwa na watu kwa njia ya mazungumzo ya mdomo - na hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mazungumzo. Lugha ya mazungumzo ni kongwe, hai na halisi zaidi ya mzungumzaji na ina maana nyingi, kwani mzungumzaji na msikilizaji huwa ana kwa ana katika mazingira mamoja.

Stadi za lugha ya mazungumzo ni kuzungumza na kusikiliza.

Na. Chanzo Kikomo
1 Kuzungumza Kusikiliza
2 Mzungumzaji Msikilizaji

Lugha ya maandishi

Hii ni lugha ambayo huwasilishwa kwa njia ya maandishi. Hii ni kiwakilishi cha lugha ya mazungumzo katika mfumo wa maandishi. Lugha ya maandishi ni changa kwani imeanza milenia za hivi karibuni baada ya kuvumbuliwa kwa maandishi.

Stadi za lugha ya maandishi ni kuandika na kusoma:

Na. Chanzo Kikomo
1 Kuandika/Maandishi Kusoma
2 Mwandishi Msomaji

Kwa kawaida, lugha ni sehemu ya utamaduni wa umma fulani. Lugha ya aina hii inaitwa lugha asilia. Lakini pia kuna lugha za kuundwa.

Nyanja za lugha

Lugha ina nyanja kuu mbili, nazo ni:

  • Sarufi - hushughulikia kanuni za lugha
  • Fasihi - hushughulikia sanaa zitokanazo na lugha husika ili kuumba kazi mbalimbali za kifasihi.

Kukua na kufa kwa lugha

Tangu siku za kwanza za binadamu, lugha zimekuwa zikichipuka, kukua, kutangaa na kufa kama kiumbe yeyote mwingine. Kwa hivyo, lugha zilizopo leo ulimwenguni, huenda baada ya karne nyingi kupita zikatoweka na kuzuka nyinginezo.

Leo ulimwenguni mathalan, kuna lugha karibu 6,700, zikiwa 1,000 katika bara la kaskazini na la kusini la Amerika, 2,000 zikiwa kwenye bara la Afrika, 230 katika bara la Ulaya, 2,200 katika bara la Asia, na 1,300 katika bara la Oshania (Australia na nchi jirani nayo).

Kurasa zinazohusiana

Tazama pia

Viungo vya nje

 
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu: