Urafiki Jazz Band
Urafiki Jazz Band ilikuwa bendi ya muziki wa dansi kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Bendi hiyo ilianzishwa mwaka 1970 ikiwa inamilikiwa na kiwanda cha nguo cha Urafiki kilichokuwa Ubungo.
Urafiki Jazz Band | |
---|---|
Urafiki Jazz Band katika miaka ya 1970
| |
Maelezo ya awali | |
Asili yake | Dar es Salaam, Tanzania |
Aina ya muziki | Muziki wa dansi |
Miaka ya kazi | Miaka ya 1970 - |
Historia na mtindo wa uimbaji
haririKatika zama hizi ukisikia neno ‘kuchakachua’ maana yake huwa kufanya jambo ambalo si halali au sahihi. Lakini neno ‘Chakachua’ katika miaka ya 70 na 80 lilikuwa na maana ya mtindo wa bendi maarufu wakati huo, na neno hilo lilitokana na mtindo wa bendi hiyo iliyokuwa inapiga mtindo iliyouita Mchakamchaka, neno lililofupishwa na wanamuziki wa bendi hii na kuitwa ‘Chaka Chuwa’. Huo ndio mtindo maarufu uliokuwa ukitumiwa na bendi ya Urafiki Jazz Band.
Bendi hii ilianzishwa mwaka 1970 ikiwa inamilikiwa na kiwanda cha nguo cha Urafiki kilichokuwa Ubungo. Jina rasmi la kiwanda hicho lilikuwa ni Friendship Textile Mill. Kiwanda kilijengwa kwa msaada wa Jamhuri ya Watu wa China na kwa urafiki huo kilipewa jina la Friendship Textile. Bendi ilianzishwa ili kutangaza bidhaa hasa Khanga na Vitenge za kiwanda hiko kwani wakati huo kulikuwa na viwanda vingine kadhaa vya nguo nchini kama vile Mwatex, Mutex, Kiltex, na kadhalika.
Meneja Mkuu wa kiwanda cha Urafiki Bw. Joseph Rwegasira aliubariki mpango huo wa kuanzishwa bendi ya dansi ya kiwanda na hivyo aliidhinisha malipo ya hundi ya Shs. 50,000/= kununulia seti ya vyombo vya muziki kutoka katika duka la Dar Es Salaam Music House ambalo mpaka leo lipo katika mtaa wa Samora Avenue Dar Es Salaam.
Uongozi wa kiwanda ulimuajiri muimbaji Juma Mrisho Feruzi aliyekuwa maarufu kwa jina la Ngulimba wa Ngulimba na kumpa jukumu la kutafuta wanamuziki kwa ajili ya bendi hii. Ngulimba alichukua wapigaji watano kutoka Orchestre African Qillado, bendi ambayo aliipigia kabla ya kujiunga na Urafiki. Wanamuziki aliowachukua walikuwa ni Michael Vincent Semgumi mpiga gitaa la Solo, Ayoub Iddi Dhahabu mpiga gitaa zito la Bass, Abassi Saidi Nyanga mpulizaji wa Tenor Saxophone na Fida Saidi mpulizaji wa Alto Saxophone.
Wanamuziki wengine walikuwa tayari waajiriwa wa kiwanda cha Urafiki kama vile Juma Ramadhani Lidenge mpiga gitaa la Second Solo, Mohamed Bakari Churchil aliyepiga gitaa la rhythm, Ezekiel Mazanda pia alipiga rhythm, Abassi Lulela kwenye Besi, Hamisi Nguru Muimbaji, Mussa Kitumbo Muimbaji, Cleaver Ulanda Muimbaji, Maarifa Ramadhani kwenye Tumba, Juma Saidi mpiga maraccass na Hamisi Mashala mpiga ngoma. Hilo ndilo lilikuwa kundi la kwanza la Urafiki Jazz Band. Mtindo walioanza nao Urafiki ulijulikana ‘Mchaka Mchaka’ na baadaye ukabadilika na kuwa ‘Chaka Chua’ na hatimaye wakati bendi inaelekea ukingoni mwa uhai wake walipiga mtindo wa ‘Pasua’ na ‘Patashika’.
Katika uhai wake bendi ya Urafiki ilipitiwa na wanamuziki wengi waliokuwa maarufu wakati huo na wengine kuja kuwa maarufu baadaye, wakiwemo Gideon Banda mpuliza saxophone kutoka Morogoro Jazz, Thobias Cosmas Chidumule na Frank Mahulu ambao walikuwa waimbaji waliotokea Western Jazz Band waliingia mwaka 1973 na kuongeza nguvu katika safu ya uimbaji.
Baadaye wapiga trampeti Mkali na Hidaya kutoka Morogoro walijiunga wakifuatana na Ali Saidi alietokea Cuban Marimba akipiga gitaa la kati (rhythm) na baadaye mwaka 1975, Mganga Hemedi kutoka Tanga, akitokea Atomic Jazz, nae alijiunga na kuwa upande wa solo na rhythm.
Urafiki Jazz Band ilirekodi nyimbo zaidi ya mia tatu zilizoelezea siasa, mapenzi, nasaha na mafundisho na pia kukosoa. Baadhi ya nyimbo zake za siasa zilizopata umaarufu ni kama zile Mwenyekiti Nyerere, Mauaji ya Soweto, Jembe na Panga na kadhalika. Mwaka 1975 Bendi ilishiriki katika mashindano ya bendi za muziki wa dansi yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar Es Salaam na kushika nafasi ya tatu, hili lilimuwezesha Juma Mrisho Ngulimba wa Ngulimba, kama Kiongozi wa Urafiki kupata nafasi ya kusindikizana na bendi ya Afro 70 kwenda Nigeria kwenye maonyesho ya mtu mweusi yaliyofanyika huko. Urafiki Jazz band haipo tena lakini hakika nyimbo zake bado zinapendwa na kuna vikundi vya vijana vimeanza kurudia nyimbo hizo kwa staili mpya, na hata tungo zake nyingine zikisikika katika mtindo wa taarab.
Ajali ya gari na kufa kwa bendi
haririBendi ya Urafiki ikiwa katika hali yake ya uchanga mwaka 1970 ilipata ajali ya gari, wakati kundi zima likitoka katika onyesho huko Chang’ombe, gari lao aina ya Volkswagon Kombi liligonga mti maeneo kona ya Kigogo na Msimbazi Mission. Baadhi ya wanamuziki waliumia sana na gari lao, likawa halifai kabisa. Wapigaji walioumia walikuwa ni Hamisi Mashala – Drummer Boy - alivunjika mguu, Mohamed Bakari Churchil aliumia kichwani na kushonwa nyuzi kadhaa, na pia Ayoub Iddi Dhahabu na Maarifa Ramadhani walipata maumivu makali kwa ndani mwilini.
Bendi ilisimamisha maonyesho yake kwa muda hadi wanamuziki wake walipopata nafuu na kuanza maonyesho tena. Hali ya ajali ile ilileta fikra mbaya kwa wanamuziki hao na wapenzi wao na ilionekana kana kwamba kulikuwa na mkono wa mtu katika ajali ile. Juma Mrisho ‘Ngulimba’ alitunga wimbo ‘Nimekosa Nini Jama’, wimbo ulioelezea kadhia hiyo. Katika kipindi hiki dhana ya ushirikina ilitawala sana katika bendi mbalimbali. Vifo vya wanamuziki mara nyingi vilihusishwa na upinzani katika bendi. Kufikia miaka ya ‘80’ kati bendi ya Urafiki ikawa inasua sua kutokana na uchakavu wa vyombo na Menejimenti iliyokuwepo wakati huo haikuwa tayari kutoa pesa kununulia vyombo vipya. Bendi ya Urafiki ilifikia tamati katika miaka ya ‘80’ kati kati na bendi hiyo ikatoweka katika anga za muziki na kubaki historia.
Tazama pia
haririMarejeo
haririMakala hii kuhusu mambo ya muziki bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Urafiki Jazz Band kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |