Akbar
Jalaluddin Muhammad Akbar ((جلال الدین محمد اکبر jalāl ud-dīn mohammad akbar); pia: Akbar Mkuu) alikuwa mtawala wa Uhindi kati ya 1556 hadi 1605. Huhesabiwa kuwa mkubwa kati ya watawala wa nasaba ya Moghuli.
Alizaliwa 15 Oktoba 1542 akawa mfalme mkuu akiwa na umri wa miaka 13 baada ya kifo cha babaye Humayun.
Mafanikio ya kijeshi na kisiasa
haririAkbar alifaulu kuondoa matishio yote ya kijeshi kwa kuwashinda Waafghanistan na pia mfalme wa Kihindu wa Delhi. Kwa njia hii alirudisha utawala wa Kiislamu juu ya kaskazini ya Uhindi. Alipata sifa nyingi kama jenerali aliyeongoza wanajeshi wake mwenyewe katika kila hatari.
Baada ya kushinda alijenga maelewano na raia wengi ambao hawakuwa Waislamu. Alifuta kodi ya jizya kwa wasio Waislamu akaoa mabinti wa wakubwa wa Rajput waliokuwa kundi la Wahindu wa Kaskazini. Aliwapa Wahindu vyeo vya juu katika serikali. Aliweza kuboresha uchumi pamoja na mapato ya serikali kwa kulinganisha kodi za mazao na mapato ya wakulima - zamani walipaswa kulipa kiasi fulani bila kujali hali ya mavuno.
Mtawala mtaalamu na msanii
haririAkbar alikuwa na vipaji vingi. Alijihusisha na usanifu majengo, uchoraji, useremala, ujenzi na ufundi. Aliamuru kukusanya fasihi na habari za historia na utamaduni wa Wamoghul pamoja na Uhindi. Alikusanya pia picha na sanaa kwa ujumla kutoka pande nyingi za dunia.
Siasa ya kidini
haririAliwapa Wahindu uhuru wa kufuata dini yao akatunza mahekalu yao kinyume cha watawala Waislamu waliomtangulia ambao waliwahi kubomoa majengo ya kidini ya Wahindu.
Alianzisha majadiliano ya kidini kati ya wataalamu wa dini mbalimbali yaani Wasilamu, Wahindu, Kalasinga na hata Wakristo kutoka Uhindi Kusini.
Viungo vya Nje
hariri- Akbar Archived 28 Septemba 2007 at the Wayback Machine.
- Utawala wa Akbar
- Wamoghuli: Akbar Archived 11 Septemba 2007 at the Wayback Machine.
- Historia ya Akbar, Mfalme wa Moghuli Archived 30 Juni 2009 at the Wayback Machine.
Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Akbar kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |