Uhindi
Uhindi (pia India) rasmi kama Jamhuri ya Uhindi, ni nchi katika Asia ya Kusini, na ni nchi ya saba kwa ukubwa duniani kwa eneo. Inapakana na Pakistan magharibi, China, Nepal, na Bhutan kaskazini, Bangladesh na Myanmar mashariki, na imezungukwa na Bahari ya Hindi kusini. Ina idadi ya watu takriban bilioni 1.428, ikiwa ya kwanza duniani. Jiji lake kubwa zaidi ni Mumbai, huku mji mkuu ukiwa New Delhi. India imegawanyika katika majimbo 28 na maeneo 8 ya muungano. Inajulikana kwa historia yake tajiri ya ustaarabu wa kale kama Indus Valley pamoja na urithi wake wa kihistoria kama Taj Mahal na mfumo wa kidemokrasia mkubwa zaidi duniani.Uhindi ina eneo la kilomita za mraba 3,287,263 na kuwa nchi ya saba duniani kubwa.
Jamhuri ya Uhindi भारत गणराज्य (Bhārat Gaṇarājya) | |
---|---|
Kaulimbiu: "सत्यमेव जयते" (Satyameva Jayate) – "Ukweli huushinda daima" | |
Wimbo wa taifa: "Jana Gana Mana" | |
Mji mkuu | New Delhi |
Mji mkubwa | Mumbai |
Serikali | Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho |
• Rais | Droupadi Murmu |
• Waziri Mkuu | Narendra Modi |
Uhuru kutoka Uingereza | |
• Uhuru | 15 Agosti 1947 |
• Jamhuri | 26 Januari 1950 |
Eneo | |
• Jumla | km2 3,287,263 km² (ya 7) |
• Maji (asilimia) | 9.6% |
Idadi ya watu | |
• Kadirio la 2023 | 1,428,627,663 |
• Msongamano | 429/km²/km2 |
PLT (PPP) | Kadirio la 2025 |
• Jumla | ▲ $17.36 trilioni (ya 3) |
• Kwa kila mtu | ▲ $11,940(ya ) |
PLT (Kawaida) | Kadirio la 2025 |
• Jumla | ▲ $4.27 trilioni |
• Kwa kila mtu | ▲ $2,940 |
HDI (2022) | ▲ 0.644 – kati |
Gini (2021) | ![]() |
Sarafu | Rupia ya Uhindi (₹) (INR) |
Majira ya saa | UTC+5:30 IST |
Upande wa magari | Kushoto |
Msimbo wa simu | ++91 |
Jina la kikoa | .in |

Historia
Historia ya awali
Binadamu walifika India kutoka Afrika kabla ya miaka 55,000 iliyopita. Uwepo wao wa muda mrefu, kwanza kama wawindaji-wakusanyaji waliozagaa barani, umefanya watu wa eneo hilo wawe na tofauti kubwa kati yao upande wa urithi wa kibiolojia, ambayo inapitwa na Waafrika tu.
Makazi ya kudumu yalianza magharibi, katika beseni la mto Indus, miaka 9,000 iliyopita, hata kuzaa ustaarabu maalumu (Indus Valley Civilisation) katika milenia ya 3 KK.
Kabla ya ukoloni
Kufikia mwaka 1200 KK, Kisanskrit cha Kale, mojawapo kati ya lugha za Kihindi-Kiulaya, kilikuwa kimeenea India kutoka Kaskazini-Magharibi, kikawa lugha ya Rigveda, mwanzoni mwa dini ya Uhindu. Hivyo lugha za Kidravidi zikakoma kaskazini.
Kufikia mwaka 400 KK, matabaka ya kudumu katika jamii yalikuwa yamejitokeza katika Uhindu. Hapo dini za Ubuddha na Ujaini zilitokea, zikipinga taratibu hizo za kibaguzi. Katika bonde la mto Gange yalianza madola ya Maurya na Gupta. Ndani yake hadhi ya wanawake ilirudi nyuma, na mtazamo wa kwamba baadhi ya watu hawatakiwi hata kuguswa ukaimarika. Huko India Kusini, Falme za Kati zilieneza maandishi na tamaduni vya lugha za Kidravidi kwa falme za Asia Kusini Mashariki.
Kati karne za kwanza baada ya Kristo, dini za Ukristo, Uislamu, Uyahudi na Uzoroastro pia zilitia mizizi katika pwani za Kusini.
Majeshi kutoka Asia ya Kati yalivamia kwa kwikwi mabonde ya India, hata kuunda usultani wa Delhi na kuingiza India Kaskazini katika umma wa Kiislamu.
Katika karne ya 15 BK, Dola la Vijayanagara liliunda utamaduni wa kudumu wa Kihindu kusini mwa India. Katika Punjab, Usikh ulianzishwa, ukipinga dini rasmi.
Dola la Mughal, mwaka 1526, liliwezesha karne mbili za amani na kuacha urithi wa usanifu majengo bora.
Wakati wa ukoloni
Uhindi wa Kiingereza ni kipindi cha historia ambapo nchi za Bara Hindi ama zilitawaliwa na Uingereza moja kwa moja ama zilikuwa chini ya usimamizi wa Uingereza kama nchi lindwa.
Utawala huo ulienea juu ya Uhindi wa leo pamoja na Pakistan, Bangladesh, Nepal na kwa muda pia juu ya Burma (Myanmar).
Utawala wa Kiingereza ulikuwa na vipindi viwili vifuatavyo:
Utawala wa Kampuni ya Kiingereza kwa Uhindi wa Mashariki (British East India Company)
Tarehe 31 Desemba 1600 malkia Elizabeth I alitoa hati ya ulinzi wa kifalme kwa biashara kati ya Uingereza na "Uhindi wa Mashariki".
Kampuni iliyopokea hati hii ilikuwa kundi la wafanyabiashara na matajiri wa London waliovutwa na utajiri wa nchi za mashariki na hasa na faida kubwa mikononi mwa wafanyabiashara Wareno na Waholanzi waliotangulia katika biashara kati ya Ulaya na nchi za Asia ya Kusini.
Kampuni ilishindana kibiashara na kivita na wafanyabiashara wa Ureno, wa Uholanzi na wa Ufaransa. Iliweza kununua au kuvamia vituo vya biashara na kujenga maboma yake kuanzia mwaka 1644 huko Bombay, Madras na penginepo.
Mwaka 1717 kampuni ilipata kibali cha mtawala wa Moghul cha kusamehewa kodi kwa biashara katika Ubengali.
Tangu mwaka 1680 kampuni ilianzisha jeshi lake la maaskari Wahindi na kuwa mshiriki katika siasa ya Uhindi.
Kati ya miaka 1756 na 1763 Uingereza pamoja na mataifa mengine ya Ulaya ilishiriki katika Vita vya miaka saba viliyokuwa vita vya kwanza vya kimabara. Waingereza walipigana pamoja na Prussia dhidi ya Austria, Ufaransa, Urusi na Uswidi. Jeshi la kampuni liliendesha vita hivyo dhidi ya maeneo ya Ufaransa katika Uhindi. Wafaransa walishindwa wakabaki na vituo vidogo tu katika miji kama Pondicherry na Mahe lakini kampuni iliongeza maeneo yake katika Uhindi.
Baada ya mwaka 1757 Kampuni ya Kiingereza ilikuwa enzi muhimu, iliweza kushindana hata na nguvu ya Moghul. Ilianza kutawala sehemu kubwa za Uhindi wa Kusini pamoja na Ubengali.
Kampuni ilitumia mbinu mbili:
- mikataba na madola ya watawala wa Kihindi waliokubali kupokea mabalozi wa kampuni kwao waliokuwa kama washauri wakuu wa Maharaja au Nawab wa eneo; siasa ya nje na mambo ya jeshi ziliwekwa chini ya kampuni
- uvamizi na utawala wa moja kwa moja, maeneo yale yalikuwa mali ya kampuni.
Mafaniko makubwa ya kampuni yalisababisha mgogoro huko Uingereza na sheria mbalimbali za bunge la Uingereza zililenga kuongeza athira ya serikali ya Uingereza juu ya shughuli za kampuni.
Katika karne ya 19 kampuni ikawa mtawala wa sehemu kubwa za Uhindi, ama kwa njia ya mikataba na watawala wa kienyeji au kwa utawala wa moja kwa moja. Kampuni ilianza kubadilisha uso wa India kujenga reli na kuanzisha mawasiliano wa kisiasa kwa huduma ya posta na pia simu za telegrafi.
Mwaka 1857 ilitokea uasi wa wanajeshi Wahindi wa jeshi la kampuni uliosababisha na mkasi wa mabadiliko na dharau ya viongozi Waingereza kwa utamaduni wa wenyeji. Utawala wa kampuni ulianza kuporomoka; uliokolewa tu kwa kupeleka Uhindi wanajeshi kutoka Uingereza. Uasi ulikomeshwa kwa mabavu.
Lakini kuingilia kati kwa serikali ya Uingereza kulikuwa mwisho wa utawala wa kampuni. Mwaka 1858 serikali ya London ilichukua madaraka yote ya kampuni ikafanya Uhindi kuwa koloni la taji la Uingereza.
Kuanzia mwaka 1858 Uhindi ulitawaliwa kama koloni la Uingereza. Kaisari wa mwisho wa Moghul Bahadur Shah Zafar II aliondolewa nchini. Malkia Viktoria wa Uingereza alichukua cheo chake akaitwa "Kaisari wa Uhindi" (kwa Kiingereza: "Empress of India"; kwa Kihindi: "Padishah-e-Hind") akamuachia utawala gavana wake aliyepewa cheo cha "makamu wa mfalme" (Vice-Roy).
Muundo wa utawala uliendelea: maeneo ya kampuni yalikuwa makoloni ya Uingereza. Maeneo ya watawala Wahindi yalibaki yalivyo lakini kila Maharaja au Nawab alipaswa kula kiapo cha utii kwa malkia kama Kaisari au malkia mkuu wa Uhindi na kumkubali mshauri Mwingereza katika jumba lake kama mwakilishi wa Uingereza.
Mwisho wa karne ya 19 harakati za kutafuta uhuru zilianza upya. Mwaka 1885 chama cha INC (Indian National Congress) kiliundwa na Wahindu na Waislamu pamoja waliodai uhuru. Mwaka 1906 viongozi Waislamu walitoka katika INC na kuunda "Shirikisho la Waislamu".
Mwaka 1917 Uingereza ulitamka ya kwamba ulitaka kuelekea polepole hali ya kujitawala kwa Wahindi. Viongozi wa wenyeji hawakuridhika na mkasi wa mabadiliko. Chini ya uongozi wa Mahatma Ghandi mwendo wa kupigania uhuru bila mabavu ulipata nguvu. Ghandi alipigania hasa umoja wa Wahindu na Waislamu lakini alipingwa na viongozi wenye itikadi kali wa pande zote mbili.
Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia Waingereza walikubali kujiondoa katika Uhindi. Swali kubwa lilikuwa kama nchi itabaki kama nchi moja au kama maeneo ya Waislamu yatajitenga.
Baada ya uhuru
Tarehe 14/15 Agosti 1947 utawala wa Uingereza ulikwisha. Bara Hindi iligawanywa katika nchi mbili za Uhindi na Pakistan. Mgawanyo ulikuja na vita na kumwaga kwa damu nyingi.
Tarehe 30 Januari 1948 Ghandi mwenyewe aliuawa na Hindu mkali aliyemchukia kwa sababu alitaka usawa wa Waislamu na Wahindu.
Mgawanyiko wa kiutawala
Hii ni orodha ya majimbo ya Uhindi:
Majimbo
Maeneo ya Muungano:
Demografia
Uhindi, ikiwa na idadi ya watu inayokadiriwa kuwa 1,428,627,663 mnamo 2023, ndiyo nchi yenye watu wengi zaidi duniani. Sensa ya 2011 ilirekodi watu 1,210,193,422, ikionyesha ongezeko la 17.64% kutoka 2001, ambalo lilikuwa chini ya ongezeko la 21.54% kati ya 1991 na 2001. Uwiano wa kijinsia kulingana na sensa ya 2011 ulikuwa wanawake 940 kwa kila wanaume 1,000. Kufikia 2020, umri wa wastani ulikuwa miaka 28.7. Sensa ya kwanza baada ya uhuru mwaka 1951 ilihesabu watu milioni 361. Ukuaji wa idadi ya watu umechochewa na maendeleo ya kitabibu na ongezeko la uzalishaji wa kilimo, hasa baada ya Mapinduzi ya Kijani. Matarajio ya maisha kwa sasa ni miaka 70—wanawake wakiwa na wastani wa miaka 71.5 na wanaume miaka 68.7. Uhindi ina madaktari 93 kwa kila watu 100,000. Ukuaji wa miji pia umeathiri mabadiliko ya idadi ya watu, huku ongezeko la wakazi wa mijini likifikia 31.2% kati ya 1991 na 2001. Sensa ya 2011 ilionyesha kuwa 31.16% ya Wahindi waliishi mijini, kutoka 27.81% mwaka 2001, na miji kama Mumbai, Delhi, Kolkata, Chennai, Bengaluru, Hyderabad, na Ahmedabad ikiwa mikubwa zaidi. Kiwango cha usomaji na uandishi kilikuwa 74.04% mwaka 2011, huku wanawake wakiwa na 65.46% na wanaume 82.14%. Tofauti ya usomaji kati ya maeneo ya vijijini na mijini ilipungua, ikiashiria maendeleo makubwa ya elimu vijijini, ambapo Kerala ilikuwa na kiwango cha juu zaidi cha usomaji (93.91%) na Bihar cha chini zaidi (63.82%).
Uhindi ni moja ya mataifa yenye utofauti mkubwa wa lugha duniani. Takriban 74% ya watu huzungumza lugha za Kihindi-Arya, ambazo ni sehemu ya familia ya lugha za Kihindi-Kiulaya, huku 24% wakizungumza lugha za Kidravidia, ambazo zilikuwepo kabla ya athari za Kihindi-Arya katika eneo hilo. Asilimia 2% iliyobaki huzungumza lugha za Kiaustroasia au Kisinotibeti. Kihindi ndicho lugha rasmi ya serikali kuu, huku Kiingereza kikihudumu kama lugha rasmi msaidizi inayotumika sana katika utawala, biashara, na elimu ya juu. Katiba ya Uhindi inatambua lugha 22 kama lugha rasmi za kikatiba, na kila jimbo au eneo la muungano lina lugha zake rasmi. Uhindi pia ina utofauti mkubwa wa kidini, ambapo Uhindu ndio dini kubwa (79.80% ya watu), ikifuatiwa na Uislamu (14.23%), Ukristo (2.30%), Usikh (1.72%), Ubuddha (0.70%), Ujain (0.36%), na dini zingine (0.9%). Taifa hili lina idadi ya tatu kwa ukubwa ya Waislamu duniani, ikiwa na idadi kubwa zaidi miongoni mwa nchi zisizo na Waislamu wengi.
Tazama pia
Viungo vya nje
- (Kiingereza) (Kihindi) Tovuti rasmi
- (Kiingereza) India Travel
- India entry at The World Factbook
- Uhindi katika Curlie (ex-Open Directory Project)
- India profile from the BBC News
- India Encyclopædia Britannica entry
- Indiaat the UCB Government Information Library (archived from originalIlihifadhiwa 17 Machi 2015 kwenye Wayback Machine.)
Nchi na maeneo ya Asia |
Afghanistan | Armenia2 | Azerbaijan | Bahrain | Bangladesh | Bhutan | Brunei | China | Falme za Kiarabu | Georgia2 | Hong Kong3 | Indonesia | Iraq | Israel | Jamhuri ya China (Taiwan) | Japani | Kamboja | Kazakhstan | Kirgizia | Korea Kaskazini | Korea Kusini | Kupro2 | Kuwait | Laos | Lebanoni | Macau3 | Malaysia | Maldivi | Mongolia | Myanmar | Nepal | Omani | Pakistan | Palestina | Qatar | Saudia | Singapuri | Sri Lanka | Syria | Tajikistan | Timor ya Mashariki | Turkmenistan | Uajemi | Ufilipino | Uhindi | Urusi1 | Uthai | Uturuki1 | Uzbekistan | Vietnam | Yemen | Yordani |
1. Nchi ina maeneo katika Asia na Ulaya. 2. Nchi iko Asia lakini inahesabiwa pia kati ya nchi za Ulaya kwa sababu za historia au utamaduni. 3. Eneo la pekee la China. |
Makala hii kuhusu maeneo ya Uhindi bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Uhindi kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |