Azimio la kazi (kwa Kiingereza: scheme of work) ni mpango kazi (mwongozo) unaoandaliwa na mwalimu ambao unaonesha mpangilio wa kufundisha mada mbalimbali kwa kipindi maalumu katika muhtasari wa somo husika. Huo ni mpango wa ufundishaji kwa kipindi fulani ambao kila mwalimu anauandaa ili kukidhi lengo la ufundishaji.

Mwalimu anaweza kuandaa azimio la kazi katika kipindi cha wiki, mwezi, nusu muhula au muhula mzima. Kitendo hiki cha uandaaji, kinaweza kumsaidia mwalimu kulipanga darasa lake vizuri na hata kujua vifaa atakavyovitumia wakati wa ufundishaji wake.

Umuhimu wa Azimio la kazi

hariri

- Kumsaidia mwalimu kwenda na mpangilio mzuri wa mada.

- Humsaidia mwalimu wapi alipofikia na kumfanya mwalimu anayempokea somo lake kujua wapi alipoishia.

- Kujua muda wa kumaliza mada yake/zake.

- Kumwezesha mwalimu kujua zana atakazozitumia katika ufundishaji wake.

Vipengele muhimu vilivyomo katika Azimio la kazi

hariri

i) Muhula: Sehemu hii huandikwa namba ya muhula ambapo Azimio la kazi litatumika.

ii) Mwezi: Sehemu hii huandikwa jina la mwezi ambao mada fulani zitafundishwa.

iii) Ujuzi: Haya ni maarifa,stadi ambayo mwanafunzi hupata baada ya kufundishwa.

iv) Wiki: Sehemu hii huandikwa idadi ya wiki katika mwezi ambapo somo hilo litafundishwa.

v) Idadi ya vipindi: Hapa huandikwa idadi ya vipindi katika juma au majuma yaliyooneshwa.

vi) Mada kuu: Sehemu hii huandikwa mada kuu itakayofundishwa katika kipindi hicho.

vii) Mada ndogo: Sehemu hii huandikwa mada ndogo itakayofundishwa.

viii) Vitendo vya ufundishaji: Sehemu hii hujazwa na mwalimu kounesha harakati zake za kuwapa somo husika wanafunzi.

ix) Vitendo vya ujifunzaji: sehemu hii huandikwa harakati za wanafunzi wakati wa kupokea somo.

x) Vifaa/zana: Katika sehemu hii, mwalimu huandika vifaa au zana atakazozitumia wakati wa ufundishaji wake.

xi) Rejea: Sehemu hii mwalimu ataandika vitabu alivyovitumia katika ufundishaji wake.

xii) Maoni: Katika sehemu hii mwalimu atatoa maoni yake kuhusu mafanikio, changamoto alizozipata katika ufundishaji wake na njia atakazozitumia katika kuboresha zaidi ufundishaji wake.

  Makala hii kuhusu mambo ya elimu bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Azimio la kazi kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.