Bakari (Bootes kwa Kilatini na Kiingereza) [1] [2]. ni jina la kundinyota kwenye angakaskazi ya dunia yetu.

Nyota za kundinyota Bakari (Bootes) katika sehemu yao ya angani

Mahali pake

Bakari ipo kati ya makundinyota ya Mashuke (pia Nadhifa, lat. Virgo) na Dubu Mkubwa (Great Bear). Njia Nyeupe inapita katika sehemu ya Bakari.

Jina

Bakari ilijulikana kwa jina hili kwa miaka mingi kati ya mabaharia Waswahili waliotumia nyota kutafuta njia baharini wakati wa usiku.[3]

Jina Bakari linatokana na ar. بقار baqqaar yaani "mchunga ng'ombe"[4]. Waarabu walipokea jina hili kutoka kwa elimu ya Wagiriki wa Kale kupitia Ptolemaio na kitabu chake cha Almagesti aliyetumia jina la Βοώτης boôtes[5]. Mitholojia ya Kigiriki iliona hapa picha ya Philomelos mwana wa mungu wa kilimo Demeter aliyebuni plau inayovutwa na maksai. Kwa hiyo Bakari ni yule anayeongoza maksai wanaovuta plau.

Lakini kuna mitholojia ya mbadala inayoona hapa mwindaji wa dubu. Kama jina lilikuwa kiasili Βοητης bo-e-tis maana yake ni "kuita kwa sauti kubwa" na inaweza kuunganishwa na hadithi ya mwindaji wa dubu (kundinyota jirani kwenye anga) anayeita mbwa wake.

Bakari-Bootes ni kati ya makundinyota yaliyotajwa tayari na Klaudio Ptolemaio katika karne ya 2 BK. Iko pia katika orodha ya makundinyota 88 ya Umoja wa kimataifa wa astronomia inapotajwa kama "Bootes"[6]

Nyota

Nyota angavu zaidi ni Simaki (α Alfa Bootis au Arcturus) inayojulikana pia kwa jina la kimataifa ya en:Arcturus yenye mwangaza unaoonekana wa −0.05 mag ikiwa umbali wa Dunia wa mwakanuru 36.7 (sawa na 11.26 parsek). Simaki ni nyota angavu zaidi ya nne angani.

Tanbihi

  1. Tahajia ya Bootes kwa Kiingereza mara nyingi ni “Boötes “ kwa kudokeza ya kwamba hapa hakuna “oo” ndefu “kama kwenye neno “ndoo” lakini “o-o” yaani sauti ya “o” mara mbili pekee. )
  2. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Bootes" katika lugha ya Kilatini ni "Bootis" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Bootis, nk.
  3. ling. Knappert 1993
  4. zaidi: anayeongoza ng'ombe; linganisha kamusi ya Lane "بَقَّار An owner, or a possessor, [or an attendant,] of بَقَر or oxen, or bulls, or cows", uk. 238 Digitized Text Version v1.1 ب Book I-1]
  5. Allen uk. 92 anataja maneno mawili ya Kigiriki Βους bus (ng'ombe) na ωθειν othein (kuendesha, kuongoza mwendo)
  6. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017

Marejeo

  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 92 ff (online hapa kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
  • Lane, Edward William: An Arabic - English Lexicon in eight parts part 1872, (Perseus Collection Arabic Materials Digitized Text Version v1.1, of reprint Beirut – Lebanon 1968), online hapa
  Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Bakari (kundinyota) kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.