Kundinyota (kwa Kiingereza: star constellation) ni idadi ya nyota zinazoonekana angani kuwa kama kundi moja.

Nyota za kundinyota Jabari (Orion) angani
Baada kuunganisha nyota za Jabari (Orion) kwa kuwaza mistari kunajitokeza picha ya mvindaji
Jabari (Orion) kama mvindaji alivyowazwa na Johann Bayer wakati wa karne ya 17 - alibadilisha kushoto na kulia maana alichora "kwa mtazamo kutoka juu"
Ramani ya anga inayoonyesha kundinyota kwa picha (uchoraji wa karne ya 17, Uholanzi)

Kusudi la kupanga nyota katika kundinyota

Tangu zamani watu walitazama nyota kama nukta na nyota za jirani kama kundi. Waliwaza kundinyota kuwa picha wakichora mistari kati yake, hivyo kuona picha za watu, wanyama au miungu yao. Kundinyota zinazojulikana sana ni kama vile Jabari (en:Orion), Nge (pia Akarabu, en:Skorpio), Mara (en:Andromeda) au Salibu (en:Southern Cross).

Kupanga nyota hivi kwa makundi kulikuwa msaada kwa watu kukumbuka na kutambua nyota.

Hali halisi nyota hizi hazina uhusiano kati yake, zinaonekana tu kama kundi kwa mtazamaji aliye duniani lakini haziko mahali pamoja katika anga-nje. Zinaweza kuwa mbali sana kutoka nyota nyingine inayoonekana iko ndani ya kundinyota lilelile.

Hivyo kundinyota ni tofauti na fungunyota (en:star cluster) ambalo ni idadi kubwa ya nyota zilizopo kweli karibu eneo moja angani. Ila tu kwa jicho tupu fungunyota linaonekana kama nyota moja tu au halionekani kutokana na umbali, zimetambuliwa kwa darubini tu. Kilimia (Pleiades) ni fungunyota la pekee linaloweza kutambuliwa bila msaada wa mitambo na hivyo ni maarufu kama kundinyota pia.

Inasaidia kutofautisha maeneo kwenye anga ya usiku kama nyota zinaweza kutajwa kuwepo katika eneo la kundinyota fulani linalokumbukwa kwa rahisi kutokana na ruwaza ya nyota.

Elimu hii ilikuwa msaada hasa kwa watu waliosafiri wakati wa usiku kama mabaharia na pia wafugaji katika mazingira ya jangwani. Walizoea kutumia nyota kama maelekezo ya njia zao.

Mfano wa Jabari (Orion)

Picha za kundinyota la Jabari (Orion) katika makala hii zinaonyesha njia kuanzia kutazama nyota angani hadi kufikia wazo la kundinyota ambalo ni picha ya mtu.

1. Jabari inaonekana vizuri kwa sababu, kwanza kuna nyota tatu zinazokaa kama mstari. Juu yake upande wa kushoto kidogo ni nyota mbili zinazong'aa sana. Chini ya mstari wa nyota tatu kuna nyota mbili au tatu (inategemea ubora wa macho) za karibu sana. Halafu chini yake tena kuna nyota mbili za mbali kidogo zinazong'aa na kufanana na zile mbili za juu. Kama giza linaongezeka, nyota zaidi zinazoonekana.

2. Watu waliunganisha nyota kwa kuwaza mistari wakaanza kumwona mtu. Nyota tatu za katikati(δ, ε, ζ) ziliitwa ukanda, nyota mbili za kung'aa za juu (α, γ) zikawa mabega ya mtu na nyota mbili za chini (β,κ) miguu yake. Nyota mbili au tatu chini ya "ukanda" (ι, θ) zikatajwa kama upanga unaofungwa kwenye ukanda. Nyota nyingine hafifu zaidi zikaunganishwa katika picha hii: nyota za "π" 1,2,3 zikawa kama ngao; λ kama kichwa.

3. Wasanii walichora picha kama ile ya juu upande wa kushoto (nyota kadhaa zilitiwa rangi katika makala hii kwa kuonekana vizuri zaidi si picha yenyewe). Hivyo katika mawazo ya watu katika tamaduni mbalimbali anga lilijaa miungu pamoja na mashujaa wa kale.

Historia ya kundinyota

Tamaduni nyingi zilipanga nyota kwa makundi. Kuna mapokeo tofautitofauti hadi leo kati ya mapokeo ya Kimagharibi (yaani Ulaya pamoja na nchi za Kislamu), ya Kihindi na ya Kichina.

Mpangilio unaotumiwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia (UKIA) uliamuliwa mwaka 1922 kwenye msingi wa elimu ya nyota ya Ugiriki ya Kale jinsi iliyoelezwa wakati wa karne ya 2 BK katika kitabu cha Almagesti cha Klaudio Ptolemaio wa Misri alimotaja makundinyota 48. Ptolemaio aliandika hitimisho ya elimu ya siku zake iliyoandaliwa na wanaastronomia waliomtangulia kama Hipparchos wa Nikaia na Eratosthenes. Wagiriki wenyewe waliendeleza elimu ya wataalamu wa Babeli waliowahi kuorodhesha nyota nyingi na kuzipanga kwa makundi.

Kitabu cha Ptolemaio kilifasiriwa kwa Kiarabu katika karne ya 9 wakati Waislamu walitawala sehemu kubwa za nchi zenye utamaduni wa Kigiriki. Almagesti iliyotafsiriwa ilikuwa msingi kwa maendeleo ya astronomia katika ustaarabu wa Kiislamu. Kwa jumla Waislamu walipokea mpangilio wa nyota kutoka kwa Wagiriki na kufasiri majina ya makundinyota. Kuanzia karne ya 12 vitabu vya Kiarabu vilifasiriwa kwa Kilatini na hivyo kupatikana kwa mataifa ya Ulaya ambako vitabu vya Wagiriki wenyewe vilipotea. Hapo majina mengi ya Kiarabu kwa nyota mbalimbali yalipokelewa katika lugha za Ulaya.

Baada ya uenezaji wa mataifa ya Ulaya duniani kupitia wapelelezi kama Kristoforo Kolumbus, Vasco da Gama, Ferdinand Magellan na Pieter Dirkszoon Keyser wanaastronomia wa Ulaya walipokea taarifa kuhusu nyota ambazo hazikujulikana kwao bado. Walianza kuchora ramani za nyota za angakusi ya dunia na kupanga makundinyota mapya kwa ajili ya nyota za kusini. Hapo alikuwa hasa Mholanzi Petrus Plancius aliyetunga makundinyota mapya 12 kwenye globu ya nyota yake.

Mnamo mwaka 1603 Mjerumani Johann Bayer alibuni mfumo wa kutaja nyota ambao kimsingi unaendelea kutumiwa hadi leo[1]. Alipanga nyota zinazoonekana kufuatana na kundinyota; hapa aliipa kila nyota herufi tofauti kufuatana mwangaza katika kundi lake. Kwa hiyo nyota angavu zaidi katika kundinyota lilipewa herufi ya Kigiriki Alfa (α), iliyofuata kwa mwangaza Beta (β) na kadhalika. Mfumo huu unajulikana kama majina ya Bayer (ing. Bayer designations)

Bayer hakupanga ufuatano kikamilifu jinsi sisi tunavyoona mwangaza leo hii. Wakati mwingine alipanga nyota zenye mwangaza wa kufanana pamoja na kuzipa herufi kuanzia kushoto kwenda kulia au kutoka juu kwenda chini.

Kama kundinyota lilikuwa na idadi kubwa ya nyota kushinda idadi ya herufi za alfabeti ya Kigiriki aliendelea kutumia herufi za Kilatini kama a-b-c.

Mfumo wa Bayer ulionekana kuwa na kasoro hasa tangu kuboreka kwa darubini kwa sababu idadi ya nyota zilizoweza kutambuliwa iliongezeka mara kwa mara. Hapo kulikuwa na mifumo mbadala iliyofuata kwa mfano ule wa namba za Flamsteed. Pamoja na maendeleo ya darubini idadi za nyota zilizoweza kutofautishwa imezidi kuongezeka. Leo hii nyota nyingi hutajwa kufuatana na orodha mbalimbali zenye nyota mamilioni lakini hata hivyo majina ya Bayer hutumiwa hadi leo kwa nyota angavu zaidi.

Matumizi ya kundinyota katika astronomia

 
Mpangilio wa anga lote kwa makundinyota kufuatana na Delporte na Ukia

.

Astronomia imeshatambua kwamba kundinyota halipo hali halisi, ni namna ya kupanga nyota tu tukitazama kutoka kwetu duniani. Hali halisi hazipatikani mahali pamoja au pa karibu katika anga-nje. Hata hivyo ni msaada wa kutaja eneo fulani kwenye anga tunayoona. Kwa sababu hiyo Umoja wa Kimataifa wa Astronomia umetambua kundinyota 88 zinazokubaliwa kama msaada wa kutaja nyota. Sayansi ya astronomia inatumia kundinyota kama mbinu ya kupata ramani ya anga juu yetu. Majina ya nyota zinazoonekana hutajwa kufuatana na eneo la kundinyota zinapoonekana halafu kwa kuongeza herufi za kigiriki.

Mfano mashuhuri ni nyota iliyo karibu na Jua letu katika anga ya ulimwengu ambayo ni Rijili Kantori. Hutajwa kama "Alpha Centauri" maana ni nyota iliyohesabiwa kama nyota ya kwanza kwa mwangaza katika eneo la kundinyota "Centaurus" (swa. Kantarusi).

Wanaastronomia wanatumia zaidi mfumo wa digrii zinazolingana na utaratibu wa latitudo na longitudo hapa duniani wakitaka kutaja mahali kamili pa nyota. Lakini hadi leo kundinyota ni msaada wa kujua eti nyota fulani au nyotamkia inapatikana katika eneo gani kwenye anga ya usiku. Hii ni sawa na kusema "mji fulani uko kaskazini-magharibi ya Afrika" kabla ya kutaja kikamilifu mahali pake kwa longitudo na latitudo.

Kundinyota katika astronomia ya kisasa

Tazama pia makala: Makundinyota 88 ya UKIA

Mwanzo wa karne ya 20 mpangilio wa kundinyota haukuridhisha kwa sababu sehemu za mipaka kati ya kundinyota hazikueleweka vema. Hivyo mkutano mkuu wa kwanza wa Umoja wa Kimataifa wa Astronomia (IAU) mwaka 1922 ulifafanua idadi ya kundinyota kuwa 88[2]. Mwanaastronomia Eugène Delporte kutoka Ubelgiji alipewa kazi ya kupanga eneo lote la anga kwa makundi na kuchora mipaka kati ya kundinyota. Tokeo la kazi yake lilikubaliwa kwenye mkutano mkuu wa mwaka 1928.

Kundinyota na utabiri katika Unajimu

Makundinyota yamekuwa muhimu kwa ajili ya unajimu. Ni hasa makundinyota 12 ya Zodiaki yanayotazamiwa kuwa muhimu na kutawala tabia za watu kwenye horoskopi. Waswahili wa kale walirithi makundinyota haya kutoka elimu ya Waarabu na kuyaita buruji za falaki[3]

Majina asilia ya buruji za falaki ni:

Katika unajimu wa siku hizi majina mengi ya kimapokeo yamesahauliwa katika unajimu Afrika ya Mashariki na badala yake wapiga falaki wanatumia orodha ya majina ambayo mara nyingi ni tafsiri ya majina ya Kiingereza tu au pia namna ya kutaja alama ya kundinyota kwa neno la Kiswahili. Kwa Mizani na Mashuke bado ni majina asilia. Majina katika unajimu wa kisasa jinsi yalivyo kawaida ni yafuatayo:

  1. Kondoo (Aries): Machi 21 – Aprili 19
  2. Ng’ombe (Taurus): Aprili 20 – Mei 21
  3. Mapacha (Gemini ): Mei 22 – Juni 20
  4. Kaa(Cancer): Juni 21 – Julai 22
  5. Simba (Leo): Julai 23 – Agosti 22
  6. Mashuke (Virgo):Agosti 23 – Sept 22
  7. Mizani (Libra): Sept 23 – Okt 22
  8. Nge (Scorpio): Okt 24- Nov 21
  9. Mshale (Sagittarius): Nov 22- Des 21
  10. Mbuzi (Capricorn):Des 22 – Jan 19
  11. Ndoo (Aquarius):Jan 20 – Feb 18
  12. Samaki (Pisces):Feb 19 – Machi 20

Tazama pia

Makundinyota 88 ya UKIA

Marejeo

  1. Johann Bayer’s southern star chart
  2. "The IAU list of the 88 constellations and their abbreviations" ya mwaka 1922, iliangaliwa Mei 2017
  3. J Knappert, fungu "In East Africa", makala AL-NUDJUM katika THE ENCYCLOPAEDIA OF ISLAM, LEIDEN BRILL 1997, VOLUME VIII NED — SAM, uk 105