Batiya (kwa maana "gudulia" au "kikombe" , kwa Kilatini na Kiingereza Crater) [1] ni jina la kundinyota kwenye angakusi ya Dunia yetu. Batiya lipo jirani na kundinyota la Nadhifa (Virgo), Shuja (en:Hydra) na Ghurabu (en:Corvus).

Nyota za kundinyota Batiya (Crater) katika sehemu yao ya angani

Jina

Batiya lilijulikana kwa jina hili kwa miaka mingi kati ya mabaharia Waswahili waliotumia nyota kutafuta njia baharini wakati wa usiku.[2]

Jina la Batiya limepokelewa kutoka kwa Waarabu wanaosema باطية baaṭiya na hao walitafsiri jina la Wagiriki wa Kale walioona hapa chombo cha kukoroga divai na maji na kukiita Κρατερ krater[3], lililotafsiriwa kwa Kilatini kama "Crater" ambalo sasa ni jina la kimataifa.

Katika mitholojia ya Kigiriki kuna hadithi ya mungu Apollo aliyemtuma ndege aina ya kunguru (Ghurabu) kumchukulia maji kwa gudulia lakini ndege alichelewa kwa sababu alikula matunda njiani. Aliporudi akaeleza kuchelewa kwake kwa uwongo ya kuwa nyoka alimzuia, hivyo akamwonyesha nyoka aliyemshika kwenye miguu yake. Apollo alijua ni uwongo akakasirika na kumrusha kunguru (Ghurabu-Corvus) pamoja na gudulia (Batiya-Crater) na nyoka (Shuja-Hydra) kwenye anga wanapokaa kama nyota. Alimwadhibu ndege mbaya kwa kuweka gudulia la maji (Batiya-Crater) karibu naye lakini ndege huyo hakuweza kunywa.[4]

Batiya ni kati ya makundinyota 48 yaliyotajwa tayari na Klaudio Ptolemaio katika karne ya 2 BK. Lipo pia katika orodha ya makundinyota 88 ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [5] kwa jina la Crater. Kifupi chake rasmi kufuatana na UKIA ni 'Crt'.[6]

Nyota

Kundinyota la Batiya lina nyota chache na dhaifu kiasi. Nyota angavu zaidi ni δ Delta Crateris yenye mwangaza unaoonekana wa mag 3.6. ikiwa umbali wa miakanuru 186 kutoka Dunia.

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Crater" katika lugha ya Kilatini ni " Crateris" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Crateris, nk.
  2. ling. Knappert 1993
  3. neno la Kiarabu ni tafsiri ya Kigiriki krater; hiki kilikuwa chombo cha kuchanganya divai na maji, pamoja na viungo kama asali vilivyokorogwa humo kwa kuongeza utamu katika utamaduni wa Ugiriki wa Kale
  4. Allen, Star-Names and their Meanings uk 180 na Crater Constellation - Myth, tovuti ya Constellation Guide, iliangaliwa Septemba 2017
  5. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  6. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R.