Chumo (filamu)
Chumo ni filamu iliyotoka mwaka 2011 nchini Tanzania. Ndani yake anakuja Hussein Mkiety (Juma), Jokate Mwegelo (Amina), Jafari Makati (Ali), Yusuph Mlela (Yustus). Filamu imetayarishwa na Tanzania na kufadhiliwa na JHU-CCP kupitia Mfuko wa Rais wa kutokomeza Malaria na USAID. Chumo inawasilisha ujumbe wa malaria wakati wa ujauzito kupitia hadithi ya kusisimua ya wapenzi wenye bahati mbaya. [1] Wawili wanapendana lakini vikwazo vya kifamilia vinapelekea mapenzi yao kuwa magumu. Filamu imeongozwa na Jordan Riber ambaye ni mtoto wa John Riber ambaye ndiye aliyetayarisha filamu ya Neria (1993) na kuongoza Yellow Card (2000). Filamu ilipata kuchaguliwa katika kinyang'aro cha tuzo za ZIFF huko Zanzibar mwaka 2011. Vilevile filamu imeshinda tuzo ya "Golden Hamster" huko nchini Marekani katika tamasha la filamu la Northwest Projections, mjini Washington. Filamu ilipata kuteuliwa katika matuzo kemkem kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu kutolewa.[2] Filamu ilizinduliwa rasmi tarehe 4 Juni, 2011 katika viwanja vya BIAFRA ambapo kulikuwa hakuna kiingilio.
Chumo | |
---|---|
Posta ya Chumo | |
Imeongozwa na | Jordan Riber |
Imetayarishwa na | John na, Louise Riber |
Nyota | Hussein Mkiety |
Muziki na | Julian Gordon Hastings |
Sinematografi | Owen Prum |
Imehaririwa na | Jordan Riber Louise Riber |
Imetolewa tar. | 4 Juni, 2011 |
Ina muda wa dk. | 45 |
Nchi | Tanzania |
Lugha | Kiswahili |
Hadithi
haririJuma ni kijana mvuvi maskini anayependa kuhadithia hekaya mbalimbali. Huku Amina akiwa msichana mdogo anayependa kuhadithiwa hekaya na hadithi mbalimbali. Katika kuhadithiana kwao hekaya mbalimbali, wakajikuta wanaunda hisia za kimapenzi na kutaka kuishi pamoja kama mke na mume. Bahati mbaya, baba mzazi wa Amina, Mzee Ali, anataka maisha mema kwa binti yake. Kwa kulipinda hili, Mzee Ali anamtafutia binti yake mume, ambaye ni Yustus, kijana mwenye pesa na anayeonekana kujipendekeza mara kwa mzee Ali, lakini mbinafsi kupita maelezo.
Juma anaamua kulivalia njuga suala hili, kwa kuhakikisha anapigania penzi lake kwa hali na mali. Filamu inaanza Juma akiwa baharini anavua, ghafula anatokea Yustus akiwa katika boti yake yenye injini na si kupiga kasia na kumfanyia istizahi ili kumuingiza maboya. Baadaye wanaonekana kwenda kwa mchuuzi samaki ambaye ni Mzee Ali (baba wa Amina). Yustus anapeleka samaki wa nguvu, huku na kujitia kutoa samaki wa zawadi kwa mkwe jina. Punde anakuja Juma na vijisamaki vyake, lakini Mzee Ali anakataa kwa sababu ni wadogo hawana viwango vya mauzo yake. Kisimani anaonekana mama mzazi wa Yustus (Natasha au Suzan Lewis) anampigia chapuo kijana wake Yustus amuoe Amina huku salam za kuitwa mkwe zikipamba moto.
Dhahiri Yustus anamzidi kete Juma, lakini kwa bahati mbaya, Amina anakuja na salam za kumueleza Juma kama ni mjamzito. Suala hili linakuwa gumu kupatana kwa wawili wale hasa ukiangalia Amina bado anaishi kwa wazazi, Juma nae hana baba wala mama ni yatima na kipato chake jau. Nyumbani kwa kina Amina, Yustus anaonekana kutawala kaya ile, punde mzee Ali anamwita bintiye na kumruhusu aondoke na Yustus pembeni kwa mazungumzo ya faragha. Tukio hili Juma analiona na Juma mwenye hasira akamvamia Yustus kwa mikwara mizito kumzuia asijihusishe na Amina.
Bila mafanikio Juma anashindwana na Yustus kwa kila hali. Amina akiwa chumbani na Juma, anamweleza ya kwamba hali ya ujauzito inazidi kukua na hawezi kujificha tena. Juma anaamua kumwendea Mzee Ali, kumweleza ya moyoni. Mzee Ali bado aliendelea msimamo wake wa kutaka mali na si utu kama awali. Licha ya Juma kutoa ahadi ya kujituma ili ashinde penzi lake, bado Mzee Ali aliendelea kumkatisha tamaa. Huko Baa, Juma anamfuata Yustus na kuanza kumwomba mashindano ya kucheza pulu tebo, hii Juma anashinda. Lakini baada ya kumaliza, Juma anaenda mbali zaidi kwa kuwekeana ahadi za mashindano zaidi hata katika kuvua na kumgombania Amina. Juma anataka kila mmoja wao aoneshe uwezo halisi alionao na si hila. Atakayeshindwa, Amina atachagua pa kwenda na si mabavu tena. Wakiwa majini, huku nyumbani Amina anaunguka na kuwahishwa kituo cha afya cha karibu.
Majibu yanakuja alikuwa ana homa kali iliyopelekea mtoto kufariki. Kule baharini, Juma anafanikiwa kupata samaki mkubwa, lakini Yustus anamfanyia kwa kumtupia baruti katika mtumbwi wake ili apoteze maisha. Yustus anarudi nchi kavu na samaki mkubwa mmoja na wadogo wengi, anakutana na Mzee Ali na kuanza kuuliza habari za Amina. Ali anauliza Juma yu wapi, majibu ya Yustus yanamkatisha tamaa Mzee Ali na kumweleza hakuna sherehe mpaka Juma arudi. Punde Juma anatokea na samaki mkubwa kabisa, ikawa furaha kwa Mzee Ali. Kwa furaha, Mzee Ali anamwambia Juma lazima ukamuone Amina katika kliniki ya karibu. Huko kliniki, Amina anampa Juma taarifa juu ya kilichotokea katika homa yake. Anampa salam za masikitiko ya kwamba wamepoteza mtoto jambo lililotokana na kutohudhuria mapema kliniki pindi tu, unaposhika ujauzito. Waliombana misamaha na kusameheana. Filamu inaishia wawili hao wakiona ufukwenu mwa bahari ya Hindi na kuishi maisha ya furaha.
Washiriki
hariri- Hussein Mkiety - (Juma)
- Yusuf Mlela - (Yustus)
- Jokate Mwegelo - (Amina)
- Jafari Makati - (Ali)
- Susan Lewis - (Mama Yustus)
Marejeo
hariri- ↑ Chumo Ilihifadhiwa 8 Januari 2017 kwenye Wayback Machine. katika Bongo Cinema.com
- ↑ "Chumo katika tovuti rasmi ya filamu"". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2017-09-12. Iliwekwa mnamo 2017-09-14.
Makala hii kuhusu filamu fulani bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Chumo (filamu) kama waigizaji wake, hadithi au matoleo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |