Dira ni kifaa cha kutambua mwelekeo. Ni chombo muhimu kwa kutafuta njia baharini au kwenye ardhi pasipo na alama zinazoonekana kama vile jangwani.

Dira inayojaa kiowevu
Mielekeo ya dira ikionyesha kaskazini katika hali ya mkoozo

Dira sumaku hariri

Ndani ya dira ya kawaida kuna sindano ya chuma sumaku inayotazama muda wote kwa ncha ya kaskazini kwa sababu inaathiriwa na uga sumaku wa dunia.

Wachina walikuwa watu wa kwanza wanaojulikana kubuni dira wakati wa karne ya 11. Walitumia sindano ya maginetiti iliyoelea kwenye bakuli ya maji juu ya ubao au karatasi.

Kuna dira kavu ambako sindano ya sumaku inalala juu ya mhimili. Aina nyingine ambayo ni bora lakini ghali zaidi ni dira kiowevu ambako sindano inaelea ndani ya kiowevu cha mchanganyiko wa alikoholi na maji.

Chini ya sindano huwa na kadi yenye mchoro wa mielekeo ya dunia ya kaskazini - kusini - mashariki - magharibi.

Mtu anayeshika dira anajigeuza hadi ncha ya sindano inakaa juu ya alama ya kaskazini kwenye kadi ya dira. Sasa anaweza kujua mielekeo mingine iko wapi mahali anaposimama.

Mielekeo ya Dira hariri

Dira huwa na mielekeo mikuu 4 ambayo ni Kaskazini, Mashariki, Kusini na Magharibi.

Mielekeo ya kati hutajwa kama kaskazini-mashariki / kaskazini-magharibi na kusini-mashariki / kusini-magharibi (kwa Kiingereza Northeast NE/ Northwest NW na Southeast SE/ Southwest SW).

Inawezekana kutaja mieleko makini zaidi kwa mfano Kusini-kusini-magharibi (South-south-west SSW) au Magharibi-kusini-magharibi (west-south-west WSW).