Fahidhi
Fahidhi (lat. & ing. Phecda pia γ Gamma Ursae Majoris, kifupi Gamma UMa, γ UMa) ni kati ya nyota angavu katika kundinyota la Dubu Mkubwa (Ursa Major).
(Gamma Ursae Majoris, Phecda) | |
---|---|
Kundinyota | Dubu Mkubwa (Ursa Major) |
Mwangaza unaonekana | 2.4 |
Kundi la spektra | A0 V – K2 V |
Paralaksi (mas) | 39.21 ± 0.40 |
Umbali (miakanuru) | 83 |
Mwangaza halisi | 2.7 |
Masi M☉ | : A: 2.94 B: 0.79 |
Nusukipenyo R☉ | A: 3.04 B: ? |
Mng’aro L☉ | A: 65.3 B: 0.39 |
Jotoridi usoni wa nyota (K) | A: 9355 B: 4780 |
Majina mbadala | Phekda, Phegda, Phekha, Fekda, γ UMa, 64 Ursae Majoris, BD+54 1475, FK5 447, GC 16268, HD 103287, HIP 58001, HR 4554, PPM 33292, SAO 28179. |
Jina
Fahidhi ilijulikana kwa mabaharia Waswahili tangu miaka mingi wakifuata njia yao baharini wakati wa usiku kwa msaada wa nyota. [1]. Walipokea jina hili kutoka kwa Waarabu waliosema فخذى fakhidhi ingawa leo wanatumia zaidi الفخذة al-fakh-dha ambayo yote inamaanisha „ paja " [2]
Umoja wa Kimataifa wa Astronomia ulikubali jina la Kiarabu na kuorodhesha nyota hii kwa tahajia ya "Phecda" [3].
Gamma Ursae Majoris ni jina la Bayer; Gamma ni herufi ya tatu katika alfabeti ya Kigiriki lakini Fahidhi ni nyota angavu ya sita na hii ni mfano ya kwamba Bayer hakufuata mwangaza kamili wakati wa kuorodhesha nyota.
Tabia
Fahidhi iko kwa umbali wa miakanuru takriban 83 kutoka Jua letu. Hivyo iko karibu na nyota nyingine za Dubu Mkubwa Mizari (umbali wa miakanuru 8.5) na Merak (umbali miakanuru 11). Hii si kawaida kwa sababu mara nyingi nyota za makundinyota hazina uhusiano kati yao hali halisi, zinaonekana tu kama kundi la pamoja ingawa umbali kati yao ni mkubwa.
Mwangaza unaoonekana ni mag 2.4. Kwa darubini Fahidhi - Phecda ilitambuliwa kuwa nyotamaradufu. Sehemu hizi mbili zinaitwa Fahidhi A na Fahidhi B.
Fahidhi A ni kubwa kuliko Jua na joto sana; masi yake ni mara 2.6 masi ya Jua na nusukipenyo chake mara 3 na jotoridi kwenye uso wake unafikia nyuzi za K 9335. Nyota hii inajizungusha haraka kwenye mhimili wake. Tabia zake zinaonyesha ni nyota yenye umri mdogo wa takriban miaka milioni 300 pekee.
Fahidhi B inatambuliwa kwa vipimo tu, bado haikutazamiwa moja kwa moja. Ni ndogo kuliko Jua. Nusukipenyo chake bado haijulikani lakini masi yake ni takriban robo tatu ya Jua. Pia jotoridi yake ni chini ya Jua. Muda wa B kuzunguka A ni miaka 20.5[4]
Tanbihi
- ↑ ling. Knappert 1993
- ↑ yaani paja la dubu , Allen (1899) uk. 438 ; vivyo hivyo pia Davis (1944PA ) anayetaja jina asilia فخذ الدب الاكبر fakhidh ad-Dubb al-Akbar, the thigh of the Greater Bear.
- ↑ Naming Stars, tovuti ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia (UKIA), iliangaliwa Novemba 2017
- ↑ Gontcharov; Kiyaeva
Viungo vya Nje
- Constellation Guide:Ursa Major
- Ursa Major, kwenye tovuti ya Ian Ridpath, Star Tales, iliangaliwa Oktoba 2017
- Phecda (Gamma Ursae Majoris), kwenye tovuti ya Prof Jim Kaler, University of Illinois, iliangaliwa Oktoba 2017
Marejeo
- Allen, Richard Hinckley: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 437 (online kwenye archive.org)
- Eggl, S.; Pilat-Lohinger, E.; Funk, B.; Georgakarakos, N.; Haghighipour, N. (2012). "Circumstellar habitable zones of binary-star systems in the solar neighbourhood". Monthly Notices of the Royal Astronomical Society. 428 (4): 3104 online hapa
- Gontcharov, G.A.; Kiyaeva, O.V. (2010). "Photocentric orbits from a direct combination of ground-based astrometry with Hipparcos II. Preliminary orbits for six astrometric binaries". New Astronomy. 15 (3): 324. online hapa
- Knappert, Jan: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331