Jua
Jua (alama: ) ni kitovu cha mfumo wa Jua wenye sayari nane, sayari vibete na magimba mengi madogo. Dunia ni sayari ya tatu katika mfumo huu. Jua ni nyota iliyo karibu na Dunia yetu kuliko nyota nyingine zote.
Umbo la Jua
Umbo la Jua linakaribia kuwa tufe kamili. Maada yake ni utegili yaani gesi ya joto sana inayoshikamanishwa na nguvu ya graviti.
Kipenyo cha Jua ni takriban kilomita 1,392,684 ambayo ni mara 109 ya kipenyo cha Dunia yetu. Masi yake ni mara 330,000 ya masi ya Dunia. Kwa ujazo Jua ni kubwa mara milioni moja kuliko Dunia.
Kikemia masi ya Jua ni hasa hidrojeni (73%) na heli (25%). Kiasi kinachobaki ni elementi nzito zaidi, kama vile oksijeni, kaboni, chuma na nyingine. Ingawa elementi nzito ni asilimia ndogo tu za masi ya Jua, kutokana na ukubwa wa Jua, elementi nzito zinalingana mara 5,000 na masi ya Dunia
Muundo wa Jua
Muundo wa Jua hufanywa na kanda tatu:
- Kiini ambako atomi za hidrojeni zinayeyungana kutengeneza heli kutokana na hali ya shinikizo na joto kubwa mno;
- Ukanda wa myuko (convection zone) ambako joto la kiini linaendesha mizunguko ya utegili inayopeleka nishati kutokana kiini kwenda angahewa ya Jua
- Ukanda wa angahewa ya Jua. Sehemu yake kubwa inaitwa tabakanuru (photosphere). Tabakanuru ni asili ya nuru na joto tunazopokea duniani. Sehemu ya nje ya angahewa ni "korona" inayoonekana tu wakati wa kupatwa kwa Jua.
Historia ya Jua
Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa Jua lilitokea takriban miaka bilioni 4.57 iliyopita katika wingu kubwa la molekuli za hidrojeni.
Kama nyota zote Jua linapitia ngazi mbalimbali katika maisha yake. Wataalamu wengi hukadiria kwamba baada ya miaka bilioni 5 ijayo akiba ya hidrojeni katika kitovu cha Jua itapungua. Halafu Jua litapanuka sana na kuwa jitu jekundu[1]. Katika hali hii inaweza kuenea hadi njia ya obiti ya Zuhura na hakuna nafasi tena kwa uhai kwenye Dunia kutokana na joto kali.
Wataalamu wanatofautiana katika makadirio yao kama upanuzi huu utasababisha pia kupotea kabisa kwa sayari za Utaridi, Mirihi na Dunia zikimezwa na kuingia ndani ya Jua.[2]
Baada ya miaka bilioni kadhaa ya kuwaka kama jitu jekundu, masi yake itakuwa imepungua itajikaza na kuendelea kwa muda usio mrefu kama nyota ndogo na hafifu. Kuna uwezekano mkubwa wa kwamba Jua litaendelea baadaye kama nyota kibete nyeupe (White Dwarf) itakayoendelea kuzimika polepole[3].
Mnururisho na upepo wa Jua
Jua linatoa mwanga, joto na mnururisho mwingine wa aina mbalimbali. Sehemu ya mnururisho huu unatoka kwa umbo la chembe kama protoni na elektroni ambazo kwa jumla hujulikana pia kama upepo wa Jua. Masi ya upepo wa Jua ni takriban tani moja kwa kila sekunde.[4] Asili ya nishati hii ni mchakato wa myeyungano wa kinyuklia ndani yake. Katika myeyungano huo hidrojeni inabadilishwa kuwa heliamu. Elementi nyingine zinatokea pia kwa kiasi kidogo. Badiliko kutoka hidrojeni kwenda heliamu inaachisha nishati inayotoka kwenye Jua kwa njia ya mnururisho.
Nishati ya mnururisho huu ni msingi wa maisha ya mimea na viumbe hai katika dunia. Nuru ya Jua inabadilishwa na mimea kwa njia ya usanisinuru kuwa nishati ya kikemia inayojenga miili yao itakayokuwa lishe tena ya mimea na wanyama.
Mambo yanayo athiri tabia ya nchi ya afrika mashariki
Jua la utosi,upepo,mwinuko,mvua,uoto,bahari na maziwa ni mambo yanayoathiri tabia ya nchi ya Afrika Mashariki.
Jua la utosi
Dunia yetu ina mistari ya kubuni inayowezesha kutambua maeneo mbalimbali kwa urahisi,mistari hiyo ni pamoja na mstari wa Ikweta,tropiki ya kansa na tropiki ya Kaprikoni Mstari wa Ikweta unaigawa dunia katika sehemu nbili za kaskazini na kusini,mstari huu una nyuzi 0 na unapita eneo la Afrika mashariki katika nchi za Kenya na Uganda.Mstari wa Tropiki ya kansa upo upande wa kaskazini mwa Ikweta. Mstari wa tropiki ya Kaprikoni Upo Kusini mwa Ikweta. Kipindi ambacho jua la Utosi lipo Tropiki ya kansa ,eneo La Kizio cha Kaskazini Huwa na joto,kwa kuwa hewa ikipata joto hutanuka hivyo huwa na mgandamizo mdogo wa hewa.Pepo huvuma kuelekea huko.
Upepo
Pepo hizi huvuma kutoka kusini-mashariki kuanzia mwezi desemba wakati jua la utosi linapokuwa tropiki ya kaprikoni kipindi hiki kizio cha kusini huwa na joto na Pepo huvuma kutoka kusini-mashariki.Pia hali hiyo husababisha mabadiliko ya upatikanaji wa mvua na hali ya joto katika eneo la Afrika Mashariki. Maeneo ya Ikweta yana tabia ya Kiikweta ya kuwa na mvua nyingi na joto jingi.Kusini na Kaskazini mwa eneo lenye tabia ya Kiikweta kuna tabia ya kitropiki yenye majira mawili makuu ya mwaka.Majira hayo ya mwaka ni masika na kiangazi.Lakini katika maeneo ya pwani majira ya mwaka hugawanyika katika sehemu nne ambazo ni vuli,kipupwe,masika na kiangazi.
Mwinuko
Afrika Mashariki ina mwinuko wa meta 0 kutoka usawa wa bahari hadi kufika meta 4600.Maeneo ya pwani mwinuko wake ni kuanzia meta 0 hadi meta 500 kutoka usawa wa bahari. Wastani wa jotoridi ni nyuzi za sentigredi 26.Joto hupungua kadiri unavyoelekea bara.Meta 1500 Kutoka usawa wa bahari ni nyuzi za sentigredi 22 ambapo ni wastani wa joto linalopatikana katika maeneo ya Tabora.Maeneo ya mlima mrefu kama kilimanjaro wenye urefu wa meta 5895 huwa na jotoridi la chini ya nyuzi za sentigredi 0
Maziwa na bahari
Maeneo yaliyo kandokando ya maziwa na bahari huwa na unyevunyevu na mvua nyingi.Mara nyingi maeneo yanayozunguka bahari na maziwa mfano Ziwa Viktoria na Bahari ya Hindi yana tabia ya nchi ya aina moja.Maeneo hayo kwa kawaida hupata mvua nyingi.
Uoto wa misitu
Maeneo yenye misitu hupata mvua nyingi kwani mawingu huweza kufanyika kwa urahisi.Misitu hiyo pia huifadhi unyevu usipotee ardhini kwa urahisi kwa njia ya mvukizo.
Pepo
Pepo za msimu za Kaskazini-mashariki Huleta Mvua kidogo katika eneo kubwa la kenya na kaskazini mwa Tanzania. Pepo huvuma sambamba na pwani.Pepo hizi pia huvuma kutoka sehemu kubwa ya nchi kavu katika nchi ya Ethiopia na Sudani kabla ya kufika eneo la Afrika Mashariki.
Angalia mengine kuhusu Sun kwenye miradi mingine ya Wikimedia: | |
Fafanuzi za Kiingereza kutoka Wiktionary | |
picha na media kutoka Commons | |
misaada ya kujisomea kwa Kiingereza kutoka Wikiversity | |
nukuu kutoka Wikiquote | |
matini za ushuhuda na vyanzo kutoka Wikisource | |
vitabu kutoka Wikibooks |
Marejeo
- ↑ Nola Taylor Redd, Red Giant Stars: Facts, Definition & the Future of the Sun , tovuti ya space.com, March 27, 2018, iliangaliwa Aprili 2018
- ↑ Klaus-Peter Schroder, Robert C. Smith , Distant future of the Sun and Earth revisited, Monthly Notices of the Royal Astronomical Society. 000, 1–10 (2008) Printed 3 February 2008
- ↑ Linganisha makadirio ya Schroder, Smith
- ↑ Carroll, Bradley W.; Ostlie, Dale A. (1995). An Introduction to Modern Astrophysics (revised 2nd ed.). Benjamin Cummings. p. 409. ISBN 0-201-54730-9.
Viungo vya Nje
- Nasa SOHO (Solar & Heliospheric Observatory) satellite
- National Solar Observatory Ilihifadhiwa 8 Aprili 2014 kwenye Wayback Machine.
- Astronomy Cast: The Sun
- A collection of spectacular images of the Sun from various institutions (The Boston Globe)
- Satellite observations of solar luminosity Ilihifadhiwa 11 Juni 2017 kwenye Wayback Machine.
- Sun|Trek, an educational website about the Sun
- The Swedish 1-meter Solar Telescope, SST
- An animated explanation of the structure of the Sun Ilihifadhiwa 10 Agosti 2011 kwenye Wayback Machine. (University of Glamorgan)
- Animation – The Future of the Sun
- Solar Conveyor Belt Speeds Up –NASA– images, link to report on Science
- NASA 5-year timelapse video of the Sun
- Sun in Ultra High Definition NASA 11 January 2015
- Album of images and videos by Seán Doran, based on SDO imagery
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Jua kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |