Galaksi ya Andromeda


Galaksi ya Andromeda (ing. Andromeda Galaxy, inajulikana pia kama Messier 31, M31 au NGC 224) ni galaksi kubwa iliyo karibu zaidi na galaksi yetu ya Njia Nyeupe. Umbali wake na Dunia ni takriban miakanuru milioni 2.5. Inaonekana katika eneo la kundinyota la Mara linaloitwa "Andromeda" kwa jina la kimataifa na hii ni chanzo cha jina lake. Ni sehemu ya kundi janibu la galaksi pamoja na Njia Nyeupe, Mawingu ya Magellan na takriban galaksi 40 nyingine.

Galaksi ya Andromeda (Andromeda Galaxy)
Galaksi ya Andromeda
Kundinyota Mara (Andromeda)
Mwangaza unaonekana +3.44
Umbali (miakanuru) milioni 2.5
Mwangaza halisi -21.5
Masi M☉ 1.5×1012
Majina mbadala Messier 31, M31, NGC 224

Ina mwangaza unaoonekana wa mag 3.4 na hivyo inaonekana kama nyota hafifu kwa mtazamaji. Hivyo ni kiolwa cha anga cha mbali kinachoonekana bila darubini.

Tabia

Umbali wa galaksi ya Andromeda hadi mfumo wa Jua letu ni takriban miakanuru milioni 2.5. Kipenyo chake cha jumla (pamoja na fungunyota za nje) ni takriban miakanuru milioni moja. Masi yake imekadiriwa kuwa mnamo masi za Jua 1.5×1012 au mara trilioni 1.5 ya masi ya Jua letu. Hivyo ni kubwa kuliko Njia Nyeupe iliyokadiriwa kuwa na M☉ 8×1011.

Kipenyo cha diski inayoonekana hukadiriwa kuwa miakanuru 140,000 hadi 220,000.


Marejeo