Kenneth Matiba
Kenneth Matiba (1 Juni 1932 – 15 Aprili 2018) alikuwa mwanasiasa wa Kenya aliyeibuka wa pili katika uchaguzi wa urais mwaka 1992.
Mwaka 2007 alitangaza kwamba alinuia kuwania urais kama mgombea huru. Aliibuka wa saba akipata kura 8,046.
Maisha
haririAlizaliwa mwaka 1932 huko Murang'a, Kenya[1]. Babake alikuwa mwalimu na pia Kenneth aliendelea kuwa mwalimu baada ya kumaliza masomo ya jiografia, historia na elimu jamii kwenye Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda.
1960 alianza kufundisha kwenye shule ya sekondari Kangaru, Embu lakini baada ya miezi 6 alihamishwa tayari kuhudumia katika wizara ya elimu huko Nairobi. Katika kipindi hiki cha mwisho wa ukoloni Waafrika wenye elimu walitafutwa kujaza nafasi za uongozi na mwaka 1963 alikuwa katibu mkuu kwenye wizara ya elimu.[2][3]
Mwanzo wa siasa
haririMatiba alipata nyadhifa ya juu katika serikali alipokuwa na umri wa miaka 31. Kabla ya Kenya kupata uhuru Disemba 1963, Matiba alikuwa katibu mkuu wa kwanza wa asili ya Kiafrika (Mei 1963). Matiba alifunzwa na Carey Francis, mwalimu mkuu wa Shule ya Upili ya Alliance. Francis ndiye aliyempigia Matiba debe kupata wadhifa huo. Mwaka 1964, Matiba aliteuliwa kuwa katibu mkuu katika wizara ya biashara, waziri wake akiwa Mwai Kibaki.
Matiba alizidi kufanikiwa katika kipindi cha baada ya Kenya kupata uhuru, akisaidiwa na kujuana kwake na familia ya Musa Gitau wa Kiambu. Musa Gitau alikuwa mmoja wa Waafrika wa kwanza kuwa mhubiri katika kanisa la Presbyterian. (Gitau ni babake vyaa Matiba). Gitau pia alikuwa na ushawishi mkubwa katika maisha ya Jomo Kenyatta, kwani alikuwa amemfunza katika PCEA Centre iliyoko Thogoto, Kikuyu. Katika mfumo uliokuwepo baada ya uhuru, kujuana na watu kulikuwa muhimu kwa ufanisi katika sekta ya umma na ya kibinafsi pia. Matiba alijitoa kwenye ulingo wa huduma za umma na kuingia katika sekta ya utalii, alipoanzisha Alliance Group of Hotels zinazopatikana kusini mwa pwani ya Kenya. Pia, aliwekeza katika shule za kibinafsi zikiwemo Hillcrest Preparatory (iliyoanzishwa na Frank Thompson) na Shule ya Upili ya Hillcrest.
Matiba alikuwa mwenyekiti wa Kenya Football Federation kutoka 1974 hadi 1978, na alishinda uchaguzi wa eneo bunge la Mbiri (lililobadilishwa jina na kuwa Kiharu) mwaka 1983. Alikuwa waziri wa usafiri na mawasiliano katika utawala wa KANU iliyoongozwa na Daniel arap Moi. Alijiuzulu mwaka 1988.
Ukerektwa wa kisiasa
haririKwa ushawishia wa Moi, Matiba pamoja na Charles Rubia walifungwa katika jela ya Kamiti mwaka 1990. Alipokuwa kizuizini, Matiba alinyimwa huduma za matibabu na kuugua maradhi ya kiharusi. Muda mfupi baadaye, Kenya ilirudi kwa mfumo wa demokrasia ya vyama zaidi ya kimoja na Matiba akaachiliwa huru.
Alikuwa mmoja wapo wa wanasiasa katika upinzani walioanzisha chama cha Forum for the Restoration of Democracy (FORD). Katika uchaguzi wa Disemba 1992, Matiba aliwania urais wa Kenya chini ya chama cha FORD-Asili. Ford-Asili ilianzishwa baada ya chama cha FORD kusambaratika. Moi alimpiku Matiba na kushinda uchaguzi huo. Matiba aliibuka wa pili. Katika uchaguzi wa maeneo bunge, alishinda kiti cha Kiharu. Matiba alisusia uchaguzi wa urais wa mwaka 1997 akisema kwamba hakungekuwa na demokrasia katika uchaguzi huo. Aliichoma kadi yake ya usajili wa kura. Matiba ana uhasama wa kisiasa wa muda mrefu na aliyekuwa rais wa Kenya Mwai Kibaki. Kabla ya uchaguzi wa Disemba 2002, Matiba alikuwa kiongozi wa chama cha Saba Saba Asili. Alikataa chama chake kujiunga na muungano wa NARC, ulioongozwa na Mwai Kibaki. Katika uchaguzi huo, Matiba hakuwania urais wala ubunge.
Kwa muda mrefu, Matiba amekumbwa na matatizo ya kiafya yaliyotokana na kufungwa kwake mwaka wa 1990. Biasha zake pia zimezorota. Alipokonywa umiliki wa hoteli zake na serikali (ingawa ulirudishwa kwake baadaye). Shule yake ya Hillcrest pia iliuzwa, ingawa baadaye alirudishiwa umiliki wake na kuiuza kwa kundi la kibiashara linaloongozwa na Fanisi. Alianzisha gazeti la The People. Lilianza kama gazeti linalochapishwa kila wiki mwaka 1992. Hatimaye mwaka 1998, lilianza kuchapishwa kila siku ingawaje ni gharama kubwa sana kwa Matiba. Mwaka 2008 Matiba bado ni mwenyekiti wa Saba Saba Asili na alijisajili tena kuwa mpiga kura.
Maisha ya binafsi
haririMwaka 2000, Matiba alichapisha kumbukumbu zake, Aiming High. Mwaka 2010, anaishi Riara Ridge, Rironi (karibu na Limuru) na mkewe Edith. Mwana wao Raymond aliwahi kuwa mwenyekiti wa bodi ya utalii ya Kenya (Kenya Tourism Board).
Tanbihi
hariri- ↑ Key events in the life of Kenneth Matiba Archived 18 Aprili 2021 at the Wayback Machine., tovuti ya hivisasa.com, iliangaliwa Aprili 2018
- ↑ Kenneth Matiba - A man of many firsts, tovuti ya nation.co.ke, iliangaliwa Aprili 2018
- ↑ The life of fallen multiparty hero Kenneth Matiba Archived 10 Mei 2019 at the Wayback Machine., tovuti ya jamhuri-news.com, iliangaliwa Aprili 2018
Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Kenneth Matiba kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |