Lango:Lugha/Lugha ya mwezi/Mei 2009
Kiswahili ni lugha ya Kibantu yenye misamiati mingi ya kiarabu inayozungumzwa katika eneo kubwa la Afrika ya Mashariki. Lugha hii ina utajiri mkubwa wa misamiati na misemo na mithali na mashairi na mafumbo na vitendawili na nyimbo. Nayo inatumika katika mashule kufundishia elimu mbali mbali za dini na dunia, na kuna vitabu vingi vilivyotungwa kwa kutumia lugha hii, vikiwa vya hadithi au hekaya au riwaya
Lugha ilianza takriban miaka 800-1000 iliyopita katika mazingira ya vituo vya biashara vya pwani ambako wafanya biashara kutoka Uarabuni, Uajemi na Uhindi walikutana na wenyeji Waafrika. Lugha kuu ya kimataifa ya biashara hii ilikuwa Kiarabu.
Inaonekana ya kwamba lugha mpya ilijitokeza wakati wenyeji wa pwani waliokuwa wasemaji wa lugha za Kibantu walipopokea maneno mengi hasa ya Kiarabu katika mawasilaino yao. Kwa hiyo msingi wa Kiswahili ni sarufi na msamiati wa Kibantu pamoja na maneno mengi ya Kiarabu. Imekadiriwa ya kwamba theluthi moja ya maneno ya Kiswahili yana asili ya Kiarabu.