Brexit (tamka Brek-sit) ni kifupi cha British exit from the European Union yaani mchakato wa Ufalme wa Muungano (Great Britain, "Uingereza") kuondoka katika Umoja wa Ulaya.

Kura ya maoni 2016 hariri

Tarehe 23 Juni 2016 kulikuwa na kura ya maoni katika Ufalme wa Muungano kuhusu swali la kubaki au kuondoka katika Umoja wa Ulaya ambako asilimia 51.9% walipigia kura hoja la kuondoka ilhali wengine walipendelea nchi kuendelea kama mwanachama wa Jumuiya ya Ulaya.

Kutokana na kura hii, serikali ya Ufalme wa Maungano ilitangaza nia yake ya kuondoka kwa kujulisha Umoja wa Ulaya rasmi kwenye tarehe 29 Machi 2017. Kufuatana na fungu 50 la Mkataba kuhusu Umoja wa Ulaya, baada ya tamko la nchi mwanachama kuwa inataka kundoka, kuna kipindi cha miaka miwili ambako mapatano kuhusu namna ya kuondoka yatajadiliwa, pamoja na mapatao kuhusu uhusiano wa nchi husika na umoja kwa miaka ya baadaye.

Kukwama kwa mapatano ya kuondoka hariri

Ufalme wa Muungano ulitakiwa kuondoka kisheria baada ya miaka miwili tarehe 29 Machi 2019 [1]. Serikali ya ya waziri mkuu Theresa May ilipatana na Umoja wa Ulaya kuhusu utaratibu wa kuondoka. Lakini tarehe 15 Januari 2019, 12 Machi na tena 29 Machi 2019 serikali ilishindwa kupata kibali cha bunge kwa mapatano yaliyoandaliwa.[2]

Tatizo kuu lilikuwa hali ya mpaka baina ya Jamhuri ya Eire (Ireland) na Eire ya Kaskazini (Northern Ireland). Hapo mapatano yalilenga kuepukana na "mpaka mgumu" baina pande mbili za kisiwa hiki lakini kwa mashariti ya Ufalme wa Muungano kubaki ndani ya eneo la ushuru la pamoja na Umoja wa Ulaya. Wapinzani waliogopa kuwa ama Ufalme wa Muungano ungepaswa kuendelea daima ndani ya utaratibu wa Umoja wa Ulaya au kutokea kwa mpaka baina ya Eire ya Kaskazini na sehemu nyingine za ufalme.

Baada ya kukosekana kwa wabunge wa kutosha wa kukubali pendekezo hili tarehe ya kuondoka ilibadilishwa baadaye kuwa 31 Oktoba 2019.[3]

Kuepukana na Brexit kali hariri

Muda wa nyongeza ulikusudiwa kuacha nafasi kwa mapatano ya utaratibu wa kuondoka. Bila mapatano ya aina hii Ufalme wa Muungano unabaki kama nchi yoyote nje ya Ulaya pamoja na haja ya kutimiza mashariti yote ya ushuru wakati wa kupokea au kutuma bidhaa Ulaya. Ilhali uchumi wa Uingereza uliwahi kukua kama sehemu ya Ulaya tangu 1973 bila kujali mipaka badiliko hili lilitazamiwa kuleta matatizo mazito. Bunge la Ufalme lilikataa mara kadhaa mfumo wa Brexit kali ("hard Brexit") bila kukubali mapatano yaliyoandaliwa na serikali ya May. Watetezi wa Brexit kali walionyesha matumaini kuwa nchi itafaulu kufanya mapatano mapya ya biashara na Marekani na nchi ya Asia.

Kuanguka kwa serikali ya May hariri

Waziri mkuu May alijiuzulu na Boris Johnson alichukua nafasi yake. Johnson alitangaza kwamba Ufalme wa Muungano utaondoka katika Umoja wa Ulaya ama kwa mapatano mapya au pia bila mapatano.

Tanbihi hariri

  1. "Brexit preparedness". European Commission. Iliwekwa mnamo 24 April 2018.  Check date values in: |accessdate= (help)
  2. https://www.bbc.co.uk/news/uk-politics-46885828
  3. Tusk, Donald (10 April 2019). "EU27/UK have agreed a flexible extension until 31 October. This means additional six months for the UK to find the best possible solution.". @eucopresident (kwa Kiingereza). Twitter. Iliwekwa mnamo 11 April 2019.  Check date values in: |date=, |accessdate= (help)
  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Brexit kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.