Majina ya nyota kwa Kiswahili

Majina ya nyota kwa Kiswahili ni jumla ya majina 100 yaliyotumiwa katika utamaduni wa Uswahilini kwa kutaja nyota.

Msingi wa kiuchumi wa miji ya Uswahilini ulikuwa biashara iliyoendeshwa kwa kutumia jahazi kwenye Bahari Hindi. Mabaharia Waswahili walivuka Bahari Hindi hadi Uarabuni, Uajemi na Uhindini. Katika safari zao walitumia nyota ili kufuata njia zao baharini wakati wa usiku.

Majina mengi ya nyota yalipokelewa kutoka lugha ya Kiarabu iliyokuwa lugha ya kimataifa ya biashara, elimu na dini katika mazingira ya Bahari Hindi hadi karne ya 19. Waarabu wenyewe waliwahi kupokea majina mengi ya nyota kutoka kwa Wagiriki wa Kale. Hapa majina ya Kigiriki yalibadilishwa kwa njia zifuatazo:

  • kwa kuandika neno la Kigiriki kwa herufi za Kiarabu (ara. قنطورس kantawrus kwa gir. Κένταυρος kentauros, kwa Kiswahili Kantarusi)
  • kwa kutafsiri jina, mfano gir. Τοξότης toksotes (kwa maana mpiga mshale), lat. & ing. Sagittarius ilitafsiriwa kwa ar. القوس al-qaus (maana upinde), kwa Kiswahili Kausi (leo kwa kawaida huitwa Mshale).
  • kwa kutumia maelezo badala ya jina, mfano gir. Ὠρίων orion inamtaja mvindaji mkubwa katika mitholojia ya Kigiriki; Waarabu ambao hawakuwa na hadithi hii wala hawakumjua mhusika huyu walimwita الجبار al-jabar yaani jitu, Kiswahili Jabari.

Hivyo sehemu ya majina ya nyota kwa Kiswahili ni majina ya Kigiriki yaliyofika kupitia Kiarabu. Pamoja na asili ya Kiarabu, pia kuna majina kutoka Kifarsi (Kiajemi) na lugha za Kihindi.

Wasemaji wa kawaida wa Kiswahili wasio mabaharia mara nyingi hawakujua majina haya ambayo ni kawaida katika lugha nyingi kuhusu istilahi za pekee. Lakini majina ya makundinyota 12 ya Zodiaki yanayoitwa buruji za falaki pamoja na majina ya sayari zilisambaa zaidi kupitia unajimu.

Kwa jumla matumizi ya elimu ya nyota katika ubaharia yamepungua sana kwa sababu siku hizi mitambo inapatikana bila matatizo hivyo nahodha hahitaji tena nyota.

Elimu ya Waswahili imehifadhiwa hasa kwa njia ya kazi ya mwanaisimu Jan Knappert kutoka Uholanzi ambaye alikusanya istilahi hizi wakati wa miaka ya 1960 alipofanya safari za utafiti wa utamaduni wa Uswahilini. Aliorodhesha majina ya Kiswahili kwa makundinyota 50 pamoja na majina ya nyota 45. Orodha ya Knappert pamoja na makala kadhaa katika jarida za kitaalamu ni ushuhuda wa kimaandishi wa pekee ambako elimu hii ilikusanywa. Orodha yake haina majina ya nyota za kusini ambazo hazikujulikana kwa Waarabu. Inawezekana ya kwamba orodha yake ina mapengo kadhaa. Katika kamusi hii majina ya “nyota mpya”  (zilizojulikana kimataifa tangu safari za kuzunguka Dunia yote, yaani miaka 500 hivi) ambayo ni Kilatini yametafsiriwa kwa Kiswahili.

Marejeo

  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
  Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Majina ya nyota kwa Kiswahili kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.