Milima ya Mahale
Milima ya Mahale ni milima ambyo ni moja ya hifadhi katika nchi ya Tanzania. Hifadhi hii iko magharibi mwa Tanzania ikiwa inapakana na Ziwa Tanganyika. Hifadhi hii inaundwa na vilima vilivyojipanga na kufunikwa na misitu minene ikiwa na jumla ya kilometa za mraba 1613.
Kama ilivyo hifadhi jirani ya kaskazini ya Gombe, hifadhi ya milima ya Mahale ni makazi ya jamii adimu zilizobakia za Sokwe barani Africa. Katika hifadhi hii yenye misitu minene inayovuta mvua kwa wingi, kundi kubwa la Sokwe huonekana katika vilima na mabonde.
Mabaki ya matunda yaliyoliwa na kinyesi kibichi ni miongoni mwa vitu vinavyowaongoza wageni hadi kuwafikia viumbe hawa. Eneo hili pia linajulikana kama Nkungwe jina linalotokana na mlima mkubwa zaidi katika hifadhi hii. Ukiwa na urefu wa mita 2460, ni mrefu zaidi ya vilele sita vinavyotengeneza safu ya milima ya Mahale inayokinga miteremko yake katika Ziwa Tanganyika.
Pia katika milima hii utaona sehemu ya asili ambayo watu wa kabila la Watongwe walikua wakiabudu mizimu yao milimani, kisha kurudi ziwani na kujitumbukiza katika maji baridi na maangavu, ziwa lenye sifa ya kuwa na zaidi ya aina 250 za samaki.
Unaweza kufika katika hifadhi hii kwa kupitia Kigoma ambako kuna meli na wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ni kipindi cha kiangazi, kati ya Mei na Oktoba.
Marejeo
haririMajarida ya hifadhi za Taifa Tanzania
Tazama pia
hariri
Viungo vya nje
hariri- TANAPA
- Utalii wa Tanzania Ilihifadhiwa 13 Januari 2010 kwenye Wayback Machine.
- [[http://web.archive.org/20090401152956/http://www.mahalepark.org/ Ilihifadhiwa 1 Aprili 2009 kwenye Wayback Machine. Hifadhi ya Mahale]]
- [Mahale]