Said Ngamba au Mzee Small (19552014) alikuwa msanii wa maigizo na vichekesho kutoka nchini Tanzania. Huenda akawa anaaminika zaidi kuwa mmoja wa wasanii wakongwe kwa nchi ya Tanzania, hasa katika fani ya uchekeshaji ambayo sasa inachezwa zaidi na vijana.

Mzee Small
Jina la kuzaliwa Said Ngamba
Alizaliwa 1955
Tanzania
Kafariki 7 Juni, 2014
Jina lingine Mzee Small
Kazi yake Mwigizaji
Rafiki Tupatupa
Mzee Majuto
Kingwendu
Watoto 5

Maisha na sanaa

hariri

Kwa historia fupi ya maisha yake, Mzee Small alizaliwa mwaka 1955 na kupata elimu yake ya msingi katika shule ya Mingumbi huko Kilwa mkoani Pwani. Mbali na kuwa mkongwe, pia Mzee Small kila unapozungumza naye huwa na kawaida ya kujitamba kuwa yeye ndiye msanii wa kwanza kabisa Tanzania Bara kuchekesha katika luninga.

Pamoja na kuwa yeye ndiyo mwanzilishi wa kuonyesha vichekesho kupitia luninga, lakini bado amesimama kufanya maigizo ingawaje alianza sanaa hiyo miaka 30 iliyopita na alipata kufundishwa na Bw. Said Seif ‘Unono’ (ambaye kwa sasa ni marehemu).

Mbali na kushiriki sanaa katika vikundi mbalimbali, pia Mzee Small amecheza sanaa katika vikundi vya mashirika kama vile Reli, NASACO na mengine mengi, ambayo kwa sasa hayajihusishi tena na shughuli hizo.

Kuanza kupata umaarufu

hariri

Mzee Small alianza kujulikana sana katika fani ya uchekeshaji hasa pale alipoibuka na mchezo unaojulikana kama 50, 50, 100, na ule wa Mjini Shule unaomwelezea mwanamke mmoja wa kijijini aliyeolewa mjini.

Mbali na kutamba na michezo hiyo, Mzee Small pia ni mcheshi na mwenye kupenda utani wakati wote, aliibuka na kichekesho kisemacho Nani Mwenye Haki, ambacho sasa ameamua kukiboresha zaidi.

Pia ameibuka na kitu kingine kiitwacho “Nani Kama Shule" huku akiwa amewashirikisha wakina Majuto, Kingwendu nawachekeshaji wengine wanaotamba sasa nchini Tanzania.

Kundi binafsi na usanii wake

hariri

Mzee Small anamiliki kundi lake la sanaa linalojulikana kama Afro Dance ambalo alilisajili mwaka 1994 kwenye Baraza la Sanaa la Taifa, BASATA, na kupata usajili rasmi mwaka huohuo wa 1994.

Pamoja na kuwa na uzoefu wa kisanaa, lakini bado hana mpango wowote ule wa kujiunga na kundi jingine, ila anachoweza kufanya ni kurekodi na wasanii wengine atakapoitwa kwa makubaliano maalum. Mzee Small alisema:

“Sina mpango wa kujiunga na kundi jingine wakati mimi nina kundi langu la Afro Dance, kama mtu au kikundi kinanihitaji ninachoweza kufanya ni kurekodi nao kwa makubaliano maalum, lakini sio kuchukuliwa kabisa na kundi hilo, “alisema Mzee Small.

Alisema kuwa kwa sasa anajitahidi kuboresha kazi yake na kuzisimamia katika mauzo, na wakati hana shughuli nyingi hujishikiza katika duka moja Kariakoo la Home Shopping Centre.

Mafanikio na maisha binafsi

hariri

Akizungumzia mafanikio aliyopata kutokana na vichekesho, Mzee Small alisema kwa utani “nimempata mke wandoa katika televisheni ambaye ni Bi. Chau.” Small akaeleza:

“Bi. Chau ni mke wangu wa ndoa katika televisheni na hakuna mtu anayempenda mkewe au mpenzi wake kama mimi na Bi. Chau tunavyopendana, kama wapo ni vizuri zaidi, “alisema Mzee Small.

Alisema kuwa mkewe, Bi. Fatuma hana tatizo lolote na Bi. Chau kwani anajua nini ninachofanya, hii ni kazi kama nyingine hivyo analielewa hilo.”

Akizungumzia kikweli kweli mafanikio yake yaliyotokana na uchekeshaji, Mzee Small alisema kuwa kwa sasa anaishi kwake na hana ugomvi na baba wala mama mwenye nyumba, “hilo kwangu halipo kwa sasa.”

“Mbali na kuishi kwangu, pia naendelea kupata mkate wangu wa kila siku na ninaweza kuwasomesha watoto wangu, mmoja yuko kidato cha tano, mwingine sekondari ya kawaida na wengine shule ya msingi, kwa pesa hii hii ya vichekesho, “alisema msanii huyo.

Mzee Small kwa sasa ana watoto watano, watatu wakiume na wawili wakike, ambapo anawasisitizia watoto wake kusoma na kama wanataka kujiingiza katika sanaa, “huo utakuwa ni uamuzi wao baada ya kumaliza masomo.”

Ushauri wake na sifa kwa wasanii wengine wa Tanzania

hariri

Mzee Small anatoa ushauri wake kwa wasanii chipukizi wanaoibuka, Mzee Small aliwataka kutobweteka na kubuni vitu vipya kila wakati ili vichekesho au maigizo yao yapendwe kila kukicha, sio kuridhika na walipofikia.

Pia aliwasifu akina Bambo, Kingwendu na wachekeshaji wengi ambao alisema wameonyesha vipaji vikubwa, “lakini sasa kinachotakiwa ni kwa mara kwa mara kubuni mbinu mpya ya uchekeshaji au uigizaji.

  Makala hii kuhusu mwigizaji filamu fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mzee Small kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.