New Orleans
New Orleans ni mji wa Marekani katika jimbo la Louisiana. Ni mji mkubwa wa Louisiana ukiwa karibu na mdomo wa mto Mississippi unapoishia katika Ghuba ya Meksiko. Mji uko kati ya mto na ziwa kubwa la Lake Pontchartrain.
Hadi Julai 2005 ilikuwa na wakazi 454,863 ikaathiriwa vibaya na tufani "Katrina" iliyoharibu sehemu kubwa na idadi ya wakazi imepungua hadi kufikia 223,388 katika mwaka 2007.
Historia
haririMji ulianzishwa 1718 na Wafaransa kama bandari muhimu wa koloni yao ya Louisiana. Jina la "New Orleans" (tamka nyu orlins) ni tafsiri ya Kiingereza ya jina asilia la Kifaransa "La Nouvelle-Orléans" (tamka la-nuvel-orlean) au "Orleans mpya" kwa heshima ya mji Orleans katika Ufaransa.
1803 eneo lote la Louisiana pamoja na mji likauzwa na mtawala Mfaransa Napoleon hivyo kuja chini ya utawala wa Marekani. Wakati ule mji ulikuwa na wakazi 10,000. Chini ya utawala wa Marekani ukakua haraka ukawa mji mkubwa katika kusini ya Marekani.
New Orleans ilikuwa kitovu cha biashara ya watumwa walioingizwa Marekani. Wakazi walikuwa mchanganyiko wa Wafaransa, Wahispania, Wamarelkani wenye lugha ya Kiingereza na pia watu huru wenye asili ya Kiafrika pamoja na watumwa.
Katika karne iliyofuata ardhi ya New Orleans ilishuka chini polepole hivyo mji uliona mafuriko makubwa kutokana na tufani ya mwaka 2005.
Uchumi
haririBandari ya New Orleans hupokea mizigo mingi inayoendelea baadaye kupitia njia ya maji ya mto Missisippi. Vilevile mazao kutoka mashamba makubwa ya Magharibi ya Kati ya Marekani husafirishwa kupitia bandari ya New Orleans kote duniani.
Kuna viwanda vingi vya kusafishia mafuta ya petroli yanayopatikana katika Ghuba ya Meksiko. New Orleans ilikuwa pia mji wa utalii watu wakavutwa na majengo ya kihistoria ya zamani za Ufaransa. Haieleweki kama utalii unaweza kuendelea baada ya uharibifu wa tufanio Katarina.
Utamaduni
haririNew Orleans ni mahali ambako tamaduni mbalimbali zimekutana na kuchanganyika: Wafaransa, watu wa Karibi, watumwa wenye asili ya Afrika, Wahispania kutoka Meksiko na Waingereza.
Mji ni mahali pa muziki hutazamiwa kama mama wa muziki ya Jazz na pia staili ya "Rhythm and Blues" iliyokuwa msingi wa "Rock ’n’ Roll". Louis Amstrong aliyekuwa mpiga tarumpeta wa Jazz mashuhuri duniani alikuwa mkazi wa mji.
Kila mwaka wakati wa wikendi mbili mwisho wa Aprili na mwanzo wa Mei kuna sherehe ya Jazz. Mwezi wa Agosti kuna sherehe nyingine ya Jazz kwa heshima ya Louis Amstrong. Watu wengi hutembelea New Orleans hasa kwa sherehe ya Mardi Gras ambayo ni aina ya karnivali kabla ya kipindi cha kwaresima.
Viung vya nje
hariri- Tovuti Ilihifadhiwa 8 Novemba 2005 kwenye Wayback Machine.
Makala hii kuhusu maeneo ya Marekani bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu New Orleans kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |