Spishi
Spishi (kutoka Kilatini "species", yaani: aina, maumbile) katika biolojia ni jina la kutaja kundi la wanyama au mimea wa aina moja. Spishi ni kitengo muhimu katika uainishaji wa kisayansi.
Kwa kuhesabiwa katika spishi ileile haitoshi kama viumbe vinafanana sana, ni lazima waweze kuzaliana na kuwa na watoto ambao wanaweza kuzaa tena.
Kwa mfano, farasi na punda ni spishi mbili tofauti zinazoweza kuzaliana lakini watoto wao, wanaoitwa baghala, hawazai tena. Mbwa wote ni spishi moja, hata kama wanaonekana na maumbile tofauti kutokana na historia ya ufugaji wa kuteua sifa kadhaa tu kwa kuzaana. Lakini hata mbwa mkubwa kabisa anaweza kuzaliana na mbwa mdogo na watoto wao wanazaa tena.
Spishi za karibu hupangwa pamoja katika jenasi.
Mfano: mbwa, mbweha, mbweha wa Ethiopia na koyote wa Marekani wote ni spishi mbalimbali za jenasi inayoitwa "Canis".
Nususpishi
haririNususpishi ni aina ndani ya spishi moja inayoonesha tofauti za wazi na spishi kwa jumla. Viumbe vya nususpishi moja wanaweza kuzaa na viumbe vya nususpishi nyingine lakini hii haitokei kwa kawaida; mfano moja ni kwamba eneo la nususpishi lipo mbali kwa hiyo hawakutani.
Nususpishi inapewa neno la tatu ndani ya jina lake.
Jina la kisayansi
haririKila spishi inaweza kupewa jina la kisayansi kufuatana na kanuni za uainishaji. Hali halisi wanyama wakubwa wameshaainishwa karibu wote lakini bado kuna wadudu, viumbehai wa baharini na bakteria wengi ambao hawajaainishwa bado.
Jina la spishi huwa na maneno mawili: Kwanza jina la jenasi (linaloanza kwa herufi kubwa) halafu neno la pili la kutofautisha spishi (linaloanza kwa herufi ndogo). Maneno ya jenasi na spishi huandikwa kwa herufi italiki.
Kwa mfano jina la paka ni "Felis silvestris". Felis ni jenasi na paka yumo pamoja na wanyama wengine wanaofanana naye kama simba, tiger au chui. Ndani ya spishi la Felis silvestris kuna nususpishi kadhaa; kwa mfano paka wa porini wa Afrika Kaskazini (Felis silvestris lybica) anayeaminiwa kuwa asili ya paka wa nyumbani (Felis silvestris catus).
Makala hii kuhusu mambo ya biolojia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Spishi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |