Simba

mnyama mla nyama kama paka mkubwa

Kwa kundinyota inayoweza kuitwa "Simba" angalia hapa Asadi (kundinyota)

Simba

Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Mammalia (Wanyama wenye viwele wanaonyonyesha wadogo wao)
Oda: Carnivora (Wanyama mbua)
Nusuoda: Feliformia (Wanyama kama paka)
Familia: Felidae (Wanyama walio na mnasaba na paka)
Nusufamilia: Pantherinae (Wanyama wanaofanana na chui)
Jenasi: Panthera
Spishi: P. leo
(Linnaeus, 1758)
Ngazi za chini

Nususpishi 2:

Msambao wa simba
Msambao wa simba

Simba (jina la kisayansi: Panthera leo[1]; kwa Kiingereza lion) ni mnyama mkubwa mla nyama (carnivore) wa familia ya Paka[2] katika ngeli ya mamalia. Maana yake ni kwamba simba hufanana na paka mkubwa.

Siku hizi simba wako hasa Afrika kusini kwa Sahara.

Simba wa Asia walipatikana zamani kati ya Uturuki na Bangladesh lakini ni wanyama 300 pekee waliobaki katika hifadhi ya wanyama huko Gujarat nchini Uhindi.

Nususpishi nyingine zilikuwepo Ulaya na pia Afrika ya kaskazini lakini zote zimekwisha kwa sababu waliwindwa vikali.

Chakula chao ni nyama inayopatikana kwa kuwinda wanyama. Tofauti na paka wengine, simba huishi na kuwinda katika vikundi vyenye wanyama 10-20. Kila kundi lina eneo lake na kuitetea dhidi ya simba wengine. simba jike ndiye anayewinda na baada ya kumkamata mnyama, dume ndiye anayeanza kula na hasa uanza kula viu vya ndani kama vile utumbo, maini, ndipo jike na watoto wanafuata kwa kula.

Dume anafikia urefu wa mwili pamoja na kichwa wa sentimita 170 hadi 250; kimo cha mabegani ni cm 120. Dume mkubwa anaweza kuwa na uzito wa kilogramu 225. Jike ni mdogo wake akiwa na urefu wa 140 hadi 175 cm, kimo cha mabegani cha cm 100 na uzito wa kg 150.

Dume anatofautishwa kirahisi kutokana na Nywele refu za shingoni ilhali jike hana.

Jike anaanza kuzaa akifikia umri wa miaka 2-3. Baada ya kubeba mimba kwa miezi 3 1/2 anazaa wadogo 2-3. Wakati mwingine idadi hii inaweza kuwa hadi wadogo 6 lakini wanaozidi 3 kwa kawaida wanakufa mapema.

Utangulizi hariri

Simba ni miongoni mwa wale paka wakubwa wa jenasi Panthera, na mmoja wa familia ya Paka. Kwa kuwa baadhi ya simba dume wanazidi kg 250 kwa uzito, wanakuwa ndio paka wa pili kwa ukubwa baada ya tiger. [1]. Simba wa porini wanapatikana huko nchi za Nusu-Jangwa Sahara katika Afrika na Asia na kwa kiasi kidogo sana huko India, kisha kupotea katika Afrika ya Kaskazini, Mashariki ya kati na Magharibi mwa Asia nyakati za historia. Karibu miaka 10,000 iliyopita, simba walikuwa ndio wanyama wa nchi kavu waliotawanyika zaidi baada ya binadamu. Walipatikana hasa Afrika, Mashariki mwa Ulaya mpaka Asia, na Amerika kuanzia Yukon mpaka Peru.

Simba huishi kwa wastani wa miaka 10-14 mwituni, huku katika hifadhi huweza hata kufika zaidi ya miaka 20. Mwituni, simba dume ni mara chache kuishi zaidi ya miaka kumi, sababu ya majeraha wanayoyapata kwa kupigana na dume wengine mara kwa mara. [2] Hupatikana sana katika savanna na nyika, ingawa pia huweza kukaa kwenye misitu na vichaka.

Simba, tofauti na paka wengine, huweza kuchangamana kwa urahisi. Kundi la simba hujumuisha simba jike ndugu kadhaa na watoto na idadi ndogo ya simba dume wakubwa. Kundi la simba jike huwinda pamoja, hasa huwinda wanyama wenye kwato. Simba huwinda wenyewe japo mara kadhaa huonekana wakijilisha mizoga. Wakati simba kwa kawaida hawawindi Binadamu, wachache wameripotiwa kumla na hivyo kumwinda.

Simba ni miongoni mwa spishi iliyo hatarini kutoweka, na kuonekana kupungua kutoka kwa asilimia 30 mpaka hivi sasa kwa asilimia 50. Japo sababu kubwa ya kupungua huku haijulikani, kupungua kwa uoto na mwingiliano na binadamu huonwa kama sabau kubwa za kupungua kwao. Tangu enzi za Roma ya Kale, simba wamekuwa spishi kuu inayotafutwa kwa ajili ya maonesho kwenye [zoo] duniani, hasa tangu mwishoni mwa karne ya 18. Spishi za Asia ndizo zilizoathirika sana na suala hilo.

Uainishaji na mageuko hariri

 
Fuvu la kichwa la simba wa sasa huko Kruger National Park

Fuvu la kale zaidi la simba lilipatikana Laetoli, Tanzania, na ni la karibu miaka milioni 3.5 iliyopita. Wanasayansi kadhaa waliita mabaki haya Panthera leo. Rekodi hizi hazijathibitishwa sana na kinachoweza kusemwa ni kuwa zinakaribiana na zile za Panthera. Panthera aliyethibitishwa ni yule wa miaka milioni 2 iliyopita.

Spishi nyingine zilizokaribia Panthera ni: tiger, jaguar na chui. Tafiti za miumbo na chembe za uhai zinaonesha kuwa tiger ndio ilikuwa spishi ya kwanza kutokea miongoni mwa hizi za wakati huu. Miaka milioni 1.9 iliyopita jaguar alijitokeza, ambaye kutoka kwake ndiyo tunapata chui na simba. Simba na chui walitengana kamili miaka milioni 1.25 iliyopita.

Panthera leo alijitokeza Afrika miaka milioni 1.8 iliyopita, kabla ya kusambaa Afrika kwenye ukanda wa Holarctic. Kwa mara ya kwanza ilionekana Ulaya miaka 700,000 na huko Amerika miaka 300,000 iliyopita.

Tabia za maumbile hariri

 
Wakati wa kugombana na wengine, nywele za simba humfanya aonekane mkubwa.

Kati ya wanyama wote wa jamii ya paka, simba ndiyo mrefu (mabegani), na ndio wa pili kwa uzito baada ya tiger. Kwa miguu yake yenye nguvu, taya imara, na meno yake chonge yenye urefu wa sm 8, simba anaweza akamwangusha na kumuua myama mkubwa. Fuvu la kichwa la simba linafanana sana na lile la tiger, hivyo tofauti ya taya zao za chini ndio pekee hutumika kuwatofautisha.

Rangi ya simba hubadilika kutoka rangi ya manjano mpaka njano, nyekundu na kahawia ya kukoza. Sehemu za chini huwa na rangi angavu na kishungi cha mkia wake ni cheusi. Watoto wa simba huzaliwa na madoa meusi mwilini mwao, kama vile wale wa chui. Japokuwa madoa haya hupotea taratibu wakati wakikua, baadhi ya madoa haya huendelea kuonekana miguuni na sehemu za chini za mwili, hasa kwa simba jike.

Miongoni mwa jamii ya paka, simba ndio pekee wenye tofauti ya moja kwa moja ya muonekano baina ya dume na jike. Simba dume na simba jike huonekana tofauti kabisa. Pia wana kazi tofauti wanazofanya katika makundi yao. Kwa mfano, simba jike, wawindaji, hawana nywele shingoni kama ilivyo kwa simba dume. Huonekana kumzuia simba jike wakati anapokuwa ananyatia mnyama na kusababisha joto zaidi wakati wa kukimbiza windo lake. Rangi ya nywele za simba dume ni tofauti, kuanzia ile kama ya dhahabu mpaka nyeusi, na mara nyingi huwa nyeusi zaidi kadiri simba anavyozeeka.

Uzito wa simba wakubwa ni kati ya kg 150 – 250 kwa dume na kg 120 – 182 kwa jike. Simba huwa na ukubwa tofauti kulingana na mazingira na eneo, kusababisha tofauti mbalimbali za rekodi za uzito. Kwa mfano, simba wa kusini mwa Afrika wameonekana kuwa wazito mara tano zaidi ya wale wa Afrika Mashariki, kwa ujumla.

Urefu wa kichwa na mwili ni sm 170 – 250 kwa dume na sm 140 – 175 kwa jike; urefu wa bega ni sm 123 kwa dume na sm 107 kwa jike. Urefu wa mkia ni sm 90 – 105 kwa dume na 70 – 100 kwa jike. Nywele ndefu zaidi za simba zilirekodiwa huko Mucsso, kusini mwa Angola, Oktoba 1973; na simba mzito kuliko wote alikuwa ni yule mla watu aliyepigwa risasi huko Transvaal, Afrika Kusini: alikuwa na uzito wa kg 313. Simba wanaohifadhiwa huwa wakubwa zaidi na pengine wazito zaidi kuliko wale wa mwituni.

Biolojia na tabia hariri

Simba hutumia muda wao mwingi wa siku kupumzika kwa takriban saa 20 kwa siku. Japokuwa wanaweza kuamka muda wowote, lakini hali hiyo hutegemea zaidi cha kuchangamana. Kipindi hicho mara nyingi baina huwa usiku mpaka mapambazuko ambako hasa ndio muda wa kuwinda. Hutumia kwa wastani saa mbili kwa siku kutembea na dakika 50 kula.

Uwindaji na chakula hariri

 
Wakati simba jike kama huyu ana meno makali sana, mawindo yake daima huuwawa kwa kunyogwa.
 
Kundi la simba wanashirikiana kumwangusha nyati huko Okavango, Botswana.
 
Simba wanne wanamwangusha nyati katika mbuga ya Serengeti, Tanzania.
 
Simba huko Mto Savuti wanajulikana kwa kuwinda kwao hata tembo.
 
Wawindaji wa kundi wanamla pundamilia mahali walipomuulia.

Simba ni wanyama wenye nguvu ambao mara zote huwinda kwa makundi na kumkazania windo walilochagua. Hata hivyo hawajulikani sana kwa stamina yao, kwa mfano, moyo wa simba jike unajumisha tu asilimia 0.57 ya uzito wa mwili wake (wa dume ni asilimia 0.45 ya uzito wa mwili wake), wakati ule wa fisi ni karibu asilimia moja ya uzito wake. Hivyo basi, japokuwa simba anaweza kufikia mwendokasi wa km 81 kwa saa, wanaweza kufanya hivyo kwa mwendo mfupi tu na inawapasa kuwa karibu na mawindo kabla ya kuanza shambulio. Hutumia mwanya wa kupunguza uoni; kwa kufanya uwindaji sana nyakati za usiku. Humnyatia adui mpaka pale wamekaribia kwa walau mita 30 au pungufu. Kisha kukaribia huchagua mnyama aliye karibu. Shambulio huwa fupi na la nguvu; hujaribu kumkamata kwa kumkurupusha kwa kasi na kisha kumrukia. Mnyama huyo daima huuawa kwa kunyongwa. Mara kadhaa pia huweza kuuawa kwa kuzibwa mdomo na pua zake kwa taya za simba. Wanyama wadogo huuawa tu kwa kupigwa ngwala kwa mguu wa simba.

Kitoweo cha simba hujumuisha wanyama wengi wakubwa, hasa Nyumbu, nyati, impala, pundamilia, na Ngiri kwa Afrika na nilgai, wild boar na aina kadhaa za tandala huko India. Spishi nyingine huwindwa kutokana na upatikanaji wao.

Simba wakiwa wanawinda katika kundi kubwa wana uwezo hata wa kuangusha wanyama wakubwa lakini mara nyingi huwa hawashambulii wanyama wakubwa sana kama vile twiga kwa kuhofia kujeruhiwa pia.

Simba pia wana uwezo wa kushambulia wanyama wanaofugwa na binadamu; kwa mfano huko India ng’ombe wengi huwa chakula cha simba. Simba pia wanaweza kula wanyama wenzao wanaokula nyama kama vile chui, duma, fisi na mbwa mwitu. Pia wakati mwingine hula mizoga ya wanyama wengine waliouawa kwa majanga au na wanyama wengine, na huangalia sana mahali wapozungukazunguka tai, wakijua fika mahali walipo patakuwa na mizoga. Simba anaweza kula mpaka kg 30 kwa mlo mmoja; na kama hawezi kula windo lake lote, hupumzika kwa saa kadhaa na kisha kuendelea tena. Wakati wa mchana na joto kali, kundi la simba hukaa kivulini na dume mmoja au wawili kubakia kama walinzi. Simba jike anahitaji walau kg 5 za nyama kwa siku wakati dume ni kg 7.

Kwa sababu simba huwinda kwenye sehemu wazi, ambapo wanaonekana kwa urahisi na adui zake, uwindaji wa ushirikiano ndio husaidia na kufanikiwa, hasa kwa wanyama wakubwa. Ushirikiano huu husaidia pia kulinda mawindo yao kwa urahisi dhidi ya wanyama wengine, kama vile fisi, ambao mara moja hujua mzoga ulipo kwa kuangalia mahali ambapo tai wanaruka. Uwindaji mkubwa hufanywa na simba jike; simba dume waliopo kwenye kundi hawashiriki kwenye uwindaji mpaka tu pale wanapohitaji kuwinda wanyama wakubwa kama vile twiga au nyati. Wakati wa kuwinda kila simba jike ana nafasi ya kuwinda na kumpata mnyama, aidha kwa kunyatia kwenye na kisha kushambulia au kusogea umbali kidogo karibu na katikati mwa kundi na kumkamata mnyama huyo amwindaye kutoka kwa simba wengine.

Simba wadogo huonesha tabia ya kunyatia wanyama wakiwa na miezi mitatu tu, ingawa hawashiriki kwenye uwindaji mpaka wawe na umri wa mwaka mmoja. Huanza rasmi kuwinda wakiwa na umri wa miaka miwili.

Uzazi na mzunguko wa maisha hariri

 
Wakati wa kujamiana, dume hutoa shahawa mara 20 mpaka 40 kwa siku kadhaa.

Wengi wa simba jike huanza kuzaa wakiwa na miaka minne. Simba hawajamiani katika kipindi maalumu cha mwaka. Kama ilivyo kwa paka wengine, uume wa simba una kama miiba zilizogeukia nyuma. Wakati wa kuutoa, miiba hiyo hukwangua kuta za uke na kusababisha kuachiwa kwa yai. Akiwa kwenye joto, simba jike huweza kujamiana na zaidi ya dume mmoja, na wakati wa kujaamiana, ambao unaweza kuchukua siku kadhaa, wenza hao hujamiana mara ishirini mpaka arobaini kwa siku na mara nyingi hata huahirisha kula. Simba huzaliana vizuri kwenye hifadhi.

Simba jike hubeba ujauzito kwa siku 110, na kisha hujifungua watoto mmoja mpaka wane kwenye sehemu maalumu, mara nyingi mbali na lilipo kundi lake. Mara nyingi huwinda peke yake wakati watoto bado hawajiwezi, wakikaa karibu na watoto huzaliwa wakiwa hawaoni, mpaka baada ya wiki hivi.

Huwa na uzito wa kg 1.2-2.1 wakati wa kuzaliwa na huweza kuanza kutambaa baada ya siku moja mpaka mbili na kuweza kutembea nje baada ya majuma matatu. Simba jike huyo huwahamisha watoto wake mara kadhaa kwa mwezi, kwa kuwabeba mmojammoja kwa shingo zao, ili kuzuia harufu kujijenga kwenye malazi yao na hivyo kuvuta wanyama wengine wala nyama ambao pengine wangeweza kuwadhuru watoto.

Katika filamu ya picha za Walt Disney The Lion King, mhusika ni mwanasimba aitwaye Simba.

Picha hariri

Viungo vya nje hariri

 
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
  1. jenasi Panthera inajumuisha na wanyama wengine ikiwemo tiger wa bara la Asia, chui na puma
  2. hii familia inajumuhisha paka wote wanaopatikana duniani, wakiwemo wanaofugwa nyumbani, paka pori, tiger, simba, chui na wengineo.