Tungo sentensi ni kipashio cha juu kabisa katika tungo chenye muundo wa kiima (K) na kiarifu (A) ambacho hutoa taarifa kamili.

Aina za sentensi

Kuna aina kuu nne za sentensi nazo ni:

  • Sentensi sahili - vilevle huru
  • Sentensi chengamano - vilevile changanuzi
  • Sentensi ambatano - vilevile ambatani
  • Sentensi shurutia


(i) Sentensi sahili/huru

Hizi ni sentensi ambazo huundwa kwa kishazi huru kimoja ambacho hutoa taarifa kamili. Kishazi huru hicho kinaweza kuundwa na kitenzi kikuu peke yake.

(A) Kitenzi kikuu

Mfano:

  • Mama amepika chakula kitamu sana
  • Halima anaendesha gari kubwa
  • Bibi amebeba mtoto mgongoni
  • Abbas anaogelea mtoni
(B) Kitenzi kikuu kisaidizi - kitenzi kikuu (TS+(-) + T)

Mfano:

  • Watoto walikuwa wanacheza mpira (watoto = N, walikuwa = TS, wanacheza = T, mpira = N).
  • Riccardo alikuwa anataka kwenda Bagamoyo
  • Anna hakuwa anataka kwenda kuogelea mtoni
(C) Kitenzi kishirikishi (t)

Mfano:

  • Wanafunzi wamo darasani
  • Chakula ki mezani
  • Ulimi hauna mfupa
  • Mimi ndimi mwalimu wenu
  • Yeye yu chumbani
  • Judith ni mdogo

(ii) Sentensi changamano

Hizi ni sentensi ambazo huundwa kwa kishazi tegemezi kimoja au zaidi - pamoja na kishazi huru.

Mifano
  • Mtoto aliyepotea jana / ameonekana leo (upande wa kushoto ni kishazi tegemezi, wakati upande wa kulia ni kishazi huru)
  • Mayai yaliyokaangwa / ni matamu sana
  • Nyumba zilizojengwa bondeni / zitabomolewa
  • Bibi aliyepika chakula ambacho ni kitamu sana / ameungua mkono
  • Ng'ombe aliyepigwa risasi iliyomvunja miguu yote ya mbele / ameunguka zizini

(iii) Sentensi ambatano

Hizi ni aina za sentensi ambazo huundwa kwa vishazi viwili au zaidi pamoja na kiunganishi. Kiunganisho hicho ndicho hufanya kazi ya kuunganisha vishazi hivyo ili kuunda sentensi ambatano. Sentensi mbili huunganishwa pamoja kwa kutumia kiunganishi. Muungano huo unaweza kuwa kati ya:

(A) Sentensi sahili + sentensi sahili

Mifano:

  • Mwalimu anafundisha/ na /wanafunzi wanaandika
  • Mama analima/ na /Baba anapanda mbegu
  • Bibi anasoma kitabu na mama anapika chakula
(B) Sentensi sahili + sentensi changamano

Mifano:

  • Mtoto amepona / ingawa /dereva aliyemgonga amekimbia
  • Mwalimu anafundisha / japokuwa wanafunzi wanaongea
(C) Sentensi changamano + sentensi changamano

Mifano:

  • Ng'ombe aliyezaa amepotea / na / ndama aliyezaliwa amekufa
  • Mtoto aliyepotea ameonekana / ingawa /walioenda kumtafuta hawajarudi
  • Mayai yaliyokaangwa ni matamu sana / ingawa / kuku wote wamekufa
(D) Sentensi changamano + sentensi sahili

Mifano:

  • Dereva aliyesababisha ajali amekufa / lakini /abiria wote wamepona
  • Wanafunzi wote wanafaulu / ingawa / walimu wao wanamasikitiko
  • Nyumba nzuri zimejengwa bondeni / ingawa /zitabomolewa
  • Ng'ombe zimepigwa risasi / ingawa /miguu yote ya mbele haikuvunjika
  • Bibi amepika chakula / japokuwa /chakula siyo kizuri sana
Angalizo

Wakati mwingine alama ya mkato (,) hutumika kama kiunganishi katika sentensi ambatano.

(iv) Sentensi shurutia

Hizi ni aina ya sentensi ambazo huundwa kwa vishazi tegemezi. Vishazi tegemezi hivyo huwa na virejeshi ambavyo huwa na dhamira za masharti ambayo yamejikita katika mofimu za -ye, -nge, -ngeli, -ngali, na -ki- ya masharti. Mofimu hizi hazichanganywi. Kama utatumia mofimu ya -nge- upande wa kwanza, sharti (ni lazima) utumie mofimu -nge- upande wa pili.

Mifano:

  • -nge- <-------> -nge-
  • -ngeli- <-------> -ngeli-
  • -ngali- <-------> -ngali-
  • -ki- huwa upande mwingine.
Kwa sentensi
  • Angelikufahamu / asingelikupita
  • Angalikufahamu / asingalikupita
  • Angeniomba / ningempa
  • Tungepata bomba / tungekunywa maji safi na salama
  • Tukisoma kwa bidii/ tutafaulu
  • Wakija / nitawapeleka
  • Angeniuliza / ningemjibu
  • Angelitumia dawa / angelipona

Tazama pia

  Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Tungo sentensi kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.